Wednesday, May 23, 2012

Mbunge Profesa Maji Marefu alazwa India

MBUNGE wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani, maarufu kama Profesa Majimarefu


Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani, maarufu kama ‘Profesa Majimarefu’, amelazwa hospitalini nchini India baada ya afya yake kubadilika.

Habari kutoka Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam, zinaeleza kuwa Ngonyani, amelazwa katika Hospitali ya Appolo, iliyoko katika mji wa Hyderabad, nchini India.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alithibitisha kuwa mbunge huyo ni mgonjwa na amelazwa nchini India.

Hata hivyo, alikataa kueleza maradhi yanayomsibu mbunge huyo kwa maelezo kwamba, jambo hilo ni siri kati ya mgonjwa na daktari wake.

Dk. Kashililah alisema Ngonyani alipelekwa India mwishoni mwa wiki iliyopita kwa uchunguzi zaidi wa afya yake.

Alisema kabla ya kupelekwa India, mbunge huyo alikuwa akitibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako alilazwa kwa siku kadhaa.

Kabla ya hapo, Ngonyani alilazwa mjini Dodoma wakati wa Mkutano wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

“Alianza kuumwa tangu alipokuwa (bungeni) Dodoma. Akalazwa Muhimbili, sasa amepelekwa India. Alipelekwa huko (India) mwishoni mwa wiki,” alisema Dk. Kashililah alipozungumza na NIPASHE.

Habari ambazo NIPASHE imezipata zinasema kuwa Maji Marefu anasumbuliwa na ugonjwa wa tumbo.

Mwaka jana wabunge na mawaziri kadhaa walipelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu.

Miongoni mwao ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ambaye alilazwa katika Hospitali ya Aga Khan na baadaye katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kabla ya kupelekwa India.

Awali Zitto alilalamikia maumivu ya kichwa, lakini alipopelekwa India alifanyowa upasuaji katika pua.

Mbunge wa Moshi Vijijini, Cyril Chami, ambaye alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, naye alikwenda India na kulazwa kwa wiki kadhaa, ingawa haikujulikana alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa gani.

Mwingine ni aliyekuwa Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, ambaye sasa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Asiye na Wizara Maalum). Profesa Mwandosya, ambaye pia ni Mbunge wa Rungwe Mashariki, alilazwa India kwa miezi kadhaa na kufanyiwa upasuaji wa mgongo.

Pia, yumo Mbunge wa Kyela, ambaye pia alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe (sasa Waziri wa Uchukuzi) aliyepelekwa India kwa matibabu ya ngozi.  
CHANZO: NIPASHE

No comments: