Wednesday, May 16, 2012

Serikali yaanza kudhibiti matumizi ya mashangingi


Viongozi wanaopenda matanuzi katika magari ya kifahari ya serikali sasa ukomo umefika baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuzuia vibali vya ununuzi wa mashangingi ambapo wakurugenzi wote waliopo katika ofisi yake wameanza kutumia magari aina ya RAV4 ukiwa ni mkakati wa kubana matumizi ya Serikali.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema hayo wakati akihojiwa na kituo cha Televisheni cha ITV katika kipindi cha dakika 45.
Alisema Serikali imeanza kutekeleza mpango wake wa kubana matumizi yasiyokuwa ya msingi tangu Waziri Mkuu alipozuia vibali vya ununuzi wa mashangingi na kama ni lazima kununua gari kinatolewa kibali cha kununua gari aina ya Double Cabin au Hard Top.
“Gari lenye gharama ya Sh. milioni 200 Waziri Mkuu amefuta ambapo kwa muda mrefu sasa magari mengi yenye thamani kubwa hayanunuliwi, lakini pia matumizi ya mafuta kwa ajili ya kurandaranda yamepungua sana,” alisema Lukuvi.
Alimtolea mfano Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba ameanza kutekeleza agizo la serikali ambapo wakurugenzi wote wa ofisi hiyo wameanza kununua magari ya RAV4 ambayo gharama yake ni pungufu ya asilimia 20 ya gharama ya shangingi.
Lukuvi alisema magari hayo ya kifahari yakishafikia kilometa 100 matengenezo yake kwa mwezi yaweza kuwa karibu Sh. milioni 10 na yanapokuwa makongwe matumizi yake yanakuwa gharama kubwa.
Aliongeza kuwa serikali inatarajia kuona maofisa kuanzia wakurugenzi au makatibu wakuu kila mmoja anaangalia mbinu na mikakati ya kupunguza gharama kwenye sekta yake bila kusubiri kupewa maelekezo ili kuokoa fedha ambazo zitapelekwa kwenye shughuli za maendeleo.
Lukuvi alifafanua kuwa matarajio ya serikali ni kuona katibu mkuu na mkurugenzi wanabana matumizi hadi kwenye halmashauri na kuwataka wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa wawabane wakurugenzi ambao baadhi yao wanasafiri sana nje ya vituo vyao vya kazi.
“Ukienda kuchukua vitabu vya wageni unashangaa mkurugenzi hajaenda hata vijiji viwili, lakini anatoka nje ya wilaya kila siku,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments: