Saturday, May 19, 2012

Tanzania kuwa moja ya nchi za mwanzo barani Afrika, kunufaika na mpango wa pamoja wa Kilimo

:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania itakua moja ya nchi za mwanzo barani Afrika, kunufaika na mpango wa pamoja wa Kilimo kwa nia ya kuongeza na kulinda usalama wa chakula na lishe kwa watu wake.

Rais Barack Obama wa Marekani aliyasema hayo jana (18.5.12) katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano kuhusu Kilimo na usalama wa chakula (Global Agriculture and Food Security) lililoandaliwa na kituo cha Masuala ya Kimataifa, Chicago Council on Global Affairs jijini Washington.

"Nimeona kuwa kuna umuhimu pia wa kuangalia changamoto zinazoikabili dunia, changamoto ya usalama wa chakula, tutatangaza ushirikiano mpya na nchi tatu zitakua za mwanzo kuanza ushirikiano huu ambao tutatangaza kwenye kushughulikia usalama wa chakula" Rais Obama amesema hayo mbele ya viongozi wa Afrika, ambao nchi zao zitakua za mwanzo kunufaika na uhusiano huo ambazo ni Ethiopia, Ghana naTanzania.

Rais Obama amesema ushirikiano huu mpya utatangazwa rasmi katika Kikao cha Nchi 8 tajiri zenye viwanda duniani maarufu kama G8 unaofanyika tarehe 19 May, 2012 katika makazi ya kupumzikia Rais wa Marekani na wageni wake maarufu kama Camp David.


Kikao hicho cha nchi tajiri duniani kimeweka katika agenda yake swala la chakula duniani kutokana na umuhimu wake katika kipindi hiki.

“Tumeliweka suala la kupiga vita njaa, Marekani ina wajibu wa kupiga vita njaa na pia suala la usalama wa chakula ni suala la kiuchumi" amesema na kuelezea kuwa Bara la Afrika linaweza kujitosheleza kwa chakula na pia katika kuuza nchi za nje.

Ushirikiano huu utakaotangazwa na Nchi 8 tajiri utahusisha serikali, watu binafsi na wafadhili ambapo mwito umetolewa kwa nchi tajiri kutimiza ahadi zao.

Kikao cha kila mwaka cha Nchi 8 tajiri zenye viwanda duniani ambazo ni Canada, ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Urusi, zingine ni Uingereza na Marekani.

Katika kikao cha mwaka huu, Tanzania imealikwa kuhudhuria kikao hicho kutokana na mpango wake wa Kilimo Kwanza, ambapo nchi tajiri zimeuchukua kama mfano ambapo juhudi na mikakati iliyomo katika Kilimo Kwanza, itatumika na kuendeleza nchi zingine barani Afrika.

Rais Obama amesema nchi hizi tatu za kwanza zimechaguliwa kunufaika na ushirikiano huu kwa vile zimeonyesha kufikia katika Kilimo na usalama wa chakula.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete, tayari yuko jijini Washington kuhudhuria kikao hicho ambapo anategemewa kuelezea matarajio na muelekeo wa Tanzania katika ushirikiano huu.

Akizungumza katika kongamano hilo la siku moja, Rais Kikwete ameelezea umuhimu wa ushirikiano huu unaohusisha serikali, wafanya biasharabinafsi na wafadhili.

"Tunahitaji msaada zaidi katika Kilimo na pia Kilimo hakiwezi kuachwa kwenye mikono ya serikali na wafadhili peke yake, hata Sekta binafsi ina mchango mkubwa" amesema na kuelezea kuwa amefarijika sana, ana matumaini na anategemea yanayozungumzwa yatatimizwa"

Mkutano wa G8 pia utahudhuriwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ambapo Mwenyekiti wake, Rais Yayi Boni wa Benin anatarajia kuhudhuria pamoja na Rais John Mills wa Ghana na Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi.

Rais Kikwete ataondoka Marekani Jumapili usiku kurudi Dar-es-Salaam.

Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi.
Washington.

No comments: