Friday, July 29, 2011

‘Hatuhusiki mgogoro Chuo cha Ustawi’ - NACTE


Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) limesema mgogoro wa kielimu unaoendelea katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) unatokana na Menejimenti ya Uongozi wa taasisi hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

NACTE imesitishwa udahili wa wanachuo wapya katika program zote za ngazi ya shahada (NTA level 8) mpaka taasisi hiyo itakapokamilisha taratibu za kupatiwa ithibati mpya.

ISW ilipata ithibati kamili Novemba 30,2005 ambayo hukaa kwa miaka mitano kabla ya kupatiwa nyingine ikiwa chuo au taasisi husika itaomba na kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa masharti ya ithibati inayomalizika.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa NACTE, Primus Nkwera alisema hatua ya kusimamisha udahili wa wanachuo wapya ulitokana na NACTE kubaini upungufu wa ubora wa viwango katika fani ya Menejimenti ya Rasimali Watu hivyo kutoa maelekezo ya marekebisho kwa ISW.

Alisema NACTE ilibaini mapungufu hayo Machi 16, 2009 na kutoa maelekezo ya marekebisho ambapo kutoka Machi 2009 hadi kufikia Agosti 2010 taasisi hiyo ilikuwa haijafanya marekebisho yoyote hivyo NACTE walitoa maagizo ya kusitishwa kwa udahili wa wanachuo wapya mpaka taasisi hiyo itakapotekeleza taratibu husika.

Nkwera alisema kumekuwa na taarifa za kupotosha kuhusu mgogoro unaoendelea ndani ya taasisi hiyo ambapo alibainisha NACTE kutohusika na kwamba mgogoro huo unashughulikiwa na vyombo vingine ikiwemo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

“ Kwa upande wetu tunatimiza majukumu yetu ipasavyo kwa vyuo vyote tunavyosimamia na kuhusu taasisi ya Ustawi tulichofanya ni kusimamisha udahili wa wanachuo wapya katika ngazi ya shahada na hiyo imetokana na uongozi wa chuo hicho kushindwa kutimiza masharti ya kupatiwa ithibati mpya kama miongozo yetu inavyowataka”,

“Kumekuwa na mlolongo wa matukio chanya na hasi ndani ya taasisi hiyo na baadhi ya taarifa zimekuwa zikipotosha kuhusu chanzo lakini kiukweli NACTE hatuhusiki kwani hayo ni nje ya mamlaka yetu ya kikazi na tukijaribu kujiingiza basi kazi itatushindwa”, alisema Nkwera.

Aliongeza kuwa NACTE ilitoa maagizo ya kusitishwa kwa udahili huo tangu Agosti 19 mwaka jana na kwamba tayari Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Katibu Mkuu wake imeanza kulishughulikia suala hilo.

Kwa muda mrefu sasa ISW imekuwa katika migogoro isiyokwisha ambapo baadhi ya matukio yanayoikabili ni pamoja na kesi mahakamani,migomo ya walimu na wanafunzi na kasi ndogo ya utekelezaji wa maagizo ya NACTE.

NACTE ni chombo cha kiserikali kilichoanzishwa mwaka 1997 ikiwa na lengo la kusimamia na kuratibu mafunzo yatolewayo na vyuo visivyo vyuo vikuu na vile visivyo chini ya VETA.Kwa sasa NACTE inasimamia vyuo 250 vya serikali na binafsi kwa nchi nzima.

No comments: