Na Anna Nkinda – Maelezo
12/07/2011 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wanawake kujenga mazoea ya kubadilishana ujuzi wa kazi jambo ambalo litasababisha vizazi vijavyo kuwa na utaalamu wa kutosha na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha na kuinua kipato cha familia.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ameyasema hayo leo wakati akiongea na wanawake walioshiriki mafunzo ya kusindika vyakula yaliyoandaliwa na WAMA walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumshukuru na kumuonyesha bidhaa ambazo wanazizalisha.
Aliendelea kusema kuwa kwa kuwafundisha wenzao kutakuwa na wigo mpana wa kuzalisha bidhaa bora na kupata masoko ya kutosha kwani kuna wanawake ambao hawana ujuzi wa kuzalisha lakini ni washawishi wazuri katika kutafuta masoko ya bidhaa husika.
“Hivi sasa mnajua jinsi ya kusindika vyakula jambo linalotakiwa ni kujipanga kwa pamoja ili muweze kujitangaza na kutafuta masoko ya bidhaa zenu, muwe na lugha nzuri kwa kufanya hivyo mtapata wateja na faida ya kutosha”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alimalizia kwa kusema kuwa hivi sasa ni wakati wa wanawake wa kusonga mbele kimaisha na kuachana na tabia ya kutegemea kufanyiwa kila kitu na waume zao na wakitaka kufanikiwa katika kazi ni lazima wawe na moyo wa kujituma.
Akiongea kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa wanafunzi wa mafunzo ya usindikaji Bertha Natai alisema kuwa wameweza kuhudhuria mafunzo hayo ya siku tano ambayo yalitolewa wezi wa tano mwaka huu na kufaulu na tayari wameshaanza kutengeneza siagi ya karanga na juisi ya nyanya.
“Ni kazi nzuri na imeweza kuwasaidia kina mama kunyanyuka kimaisha hivi sasa tumeunda umoja wetu ambao uko chini ya WAMA na tumeshaanza kuwaelimisha wenzetu ili nao waweze kutengeneza bidhaa kama hizi na kupata pesa ambazo zitawasaidia kimaisha”, alisema Natai.
Jumla ya wanawake 30 walihudhuria mafunzo hayo ya kusindika vyakula ambayo yalitolewa na SIDO kwa vikundi vya wanawake 14 ambavyo viko chini ya usimamizi wa WAMA kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la watu wa Marekani (USAID) kutoka wilaya za Ilala, Kinondoni, Temeke na Mkuranga.