Wednesday, August 17, 2011

HOTUBA YA KAMBI YA UPINZANI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA 2011/2012


Mbunge wa iringa Mjini-Chadema Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa
---
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHE. MCHUNGAJI PETER MSIGWA, (MB) WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA 2011/2012.


UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi rasmi ya Upinzani,nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuwasilisha Maoni na Mapendekezo ya Kambi yetu kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2011/2012, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(3) na (7) toleo la 2007.


Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumsifu, kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwenye nguvu na hekima tele kwa kunipa afya njema na kuendelea kunipigania kwenye kila jambo. Kama alivyomuwezesha Daudi kuibuka mshindi dhidi ya Goliath, jitu kubwa na lenye nguvu nyingi, ndivyo alivyoniwezesha mimi kushinda uchaguzi na kuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini. Kwa makusudi yake maalum, ambayo sina budi kuyatekeleza nikifuata uongozi wake, namshukuru kwa kunifanya sehemu ya Bunge hili la Kumi, ambalo binafsi naamini ni Bunge la Kimapinduzi.


Mheshimiwa Spika, kwa nafasi ya kipekee kabisa, namshukuru mke wangu mpenzi, Mama Kisa Msigwa, watoto wetu Jimmy, Peter Junior, Semione, Karren na mapacha wetu, Jacqueline na Jocelyn, kwa upendo na sala zao kwangu. Na huko waliko nawaomba wakumbuke kuwa; The value of our dignity in this World will never be determined by what we have accumulated, but rather for what we have contributed. Thamani ya utu wetu hapa duniani haitatokana na kile tunachokichuma katika jamii, bali itatokana na kile tunachojitolea kwa jamii. Naisihi familia yangu iendelee kuniunga mkono wakati wote ninapokuwa mbali, nikishughulikia kero na matatizo ya wananchi wa Iringa Mjini.


Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa dhati na kwa unyenyekevu mkubwa, nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Iringa Mjini kwa kunielewa, kuniamini na hatimaye kunipa heshima hii kubwa ya kuwa mbunge wao. Wazee wa Iringa Mjini, Vijana wa Iringa Mjini na akina Mama wa Iringa Mjini, kwa hiyari yao wenyewe waliamua kuchagua uadilifu dhidi ya ufisadi, umakini dhidi ya usanii, na walichagua haki dhidi ya dhuluma. Nawasifu, nawapongeza na ninawashukuru kwa ujasiri na ushujaa wao mkubwa waliouonyesha katika kipindi chote cha kampeni zetu na hasa wakati wa kulinda kura zao. Nawapenda, na Mungu awabariki sana. Sitawaangusha.


Mheshimiwa Spika, shukrani na pongezi zangu za dhati pia nazielekeza kwaviongozi wakuu wa CHADEMA, kwa kukiongoza vema chama chetu na kuwa tumaini pekee na la uhakika la Watanzania wengi. Mwanafalsafa mmoja maarufu wa karne ya 16, katika moja ya maandiko yake aliwahi kusema, `Weak leaders inspire their followers to have confidence in them. But Great leaders inspire citizens to have confidence in themselves.


Viongozi dhaifu huhamasisha kuaminiwa na wafuasi wao, lakini Viongozi makini huhamasisha wananchi wajiamini’,mwisho wa kunukuu.Leo Watanzania wamejitambua zaidi, wamejiamini zaidi na wamekuwa na ujasiri zaidi, hata kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano na maandamano ya kudai haki na maendeleo yao, kwa sababu wameguswa na harakati za kizalendo za CHADEMA, chini ya uongozi makini wa Kamanda Mkuu, Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe na Katibu Mkuu wetu Mhe. Dk. Willbrod Peter Slaa. Nawapongeza sana, CHADEMA mwendo mdundo, hakuna kulala mpaka kieleweke.


WIZARA YA MALIASILI NA UTALII


Mheshimiwa Spika, Dira ya Wizara ya Maliasili na Utalii inalenga kuwa na “Maliasili na Malikale zilizohifadhiwa vizuri, kusimamiwa na kutumika kiendelevu na kuwa na utalii unaowajibika”. Kwa dira hii na utajiri mkubwa wa maliasili na vivutio vya utalii tulivyo navyo, Wizara hii, ilipaswa kuwa mtaji mkubwa wa kuharakisha maendeleo ya nchi hii. Ilipaswa kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali katika kugharamia na kusukuma miradi mingi ya maendeleo ya wananchi.


Mheshimiwa Spika, kinyume chake, Watanzania wengi, ndani ya nchi hii, yenye utajiri mkubwa wa misitu na mbuga nyingi za wanyama, milima na mabonde ya kuvutia, pamoja na vivutio vingi vya utalii, wameendelea kuwa maskini hata baada ya miaka 50 ya uhuru wetu. Wizara ya Malisili na Utalii, iliyopaswa kuwa mtaji na chachu ya maendeleo yao, imekuwa ndiyo moja ya wizara dhaifu kabisa kwa ubadhirifu na upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali na maliasili zetu wakiwemo Wanyamapori.


Mheshimiwa Spika, Rais wa zamani wa Marekani, Theodere Roosevelt, aliwahi kusema, “si kweli kwamba tumeachiwa maliasili tulizonazo na mababu na mabibi zetu…. Ukweli ni kwamba tumeazimishwa maliasili hizi na watoto wetu na vizazi vijavyo”, mwisho wa kunukuu.


Ni kwa bahati mbaya kuwa Viongozi wa Serikali hii wamekuwa wakiishi kama vile wana haki ya kutumia maliasili hizi kadri watakavyo na kwa nguvu zao zote. Kizazi chetu hiki ni waangalizi tu wa mali hizi ambazo ni za watoto wetu na vizazi vijavyo. Kama waangalizi tuna wajibu wa kudai uwajibikaji katika matumizi ya maliasili zilizopo.


Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani kwa niaba ya Watanzania, inachukua wajibu huu kudai uwajibikaji katika matumizi ya raslimali za nchi hii; Kwani, kila mwaka, maliasili zetu zimekuwa zikifujwa kwa makusudi na viongozi na watumishi wa Serikali kwa kisingizio cha udhaifu wa kimfumo. Upembuzi wetu kuhusu ripoti na nyaraka za Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, umeonyesha kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2009/2010 pekee, Wizara hii ilifanya ukiukwaji mkubwa wa Sheria na Kanuni za Fedha, wa jumla ya shilingi bilioni 9.2 na kusababisha taifa lipate hasara ya moja kwa moja ya zaidi ya shilingi bilioni 1.
ENDELEA HAPA

No comments: