Wednesday, August 24, 2011

Ikulu: Hatuna barua ya kujiuzulu Mwandosya






Ikulu imejibu uvumi na taarifa zilizoandikwa na gazeti moja kuwa Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, amejizulu, kwa kusema kwamba hakuna taarifa kama hizo.
Kadhalika Ikulu ilisema kwamba Waziri Mwandosya, hajaandika barua ya kuomba kujiuzulu wadhifa huo, kufuatia kuugua na kulazwa nchini India.
Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Premi Kibanga, aliliambia NIPASHE jana kuwa Ikulu haina taarifa hizo wala haijapokea barua iliyoandikwa na Profesa Mwandosya kutaka kuachia ngazi. Kumekuwepo na taarifa kwamba mapema wiki hii kuwa Profesa Mwandosya ambaye amelazwa katika hospitali ya Apollo nchini India ameamua kumwandikia Rais Jakaya Kikwete barua ya kujiuzulu ili apumzike kutokana na kusumbuliwa na maradhi.
Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, tangu juzi alikuwa akitafutwa kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa taarifa hizo, lakini jitihada zetu hazikuzaa matunda.

Hata jana mwandishi wetu alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza ripoti ya uchunguzi wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za hesabu za Wizara ya Nishati na Madini, Luhanjo hakuwa tayari kuulizwa maswali mengine zaidi ya ripoti hiyo.
Kibanga kupitia kwa katibu muhtasi wake, alisema kuwa taarifa za kujiuzulu kwa Profesa Mwandosya sio za kweli na kuongeza kuwa hata mke wa Waziri Mwandosya ameshazungumzia suala hilo.
Hadi sasa, Profesa Mwandosya ambaye aliwahi kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 bado amelazwa nchini India kutokana na kufanyiwa upasuaji wa kutokana na kusumbuliwa na uti wa mgongo kwa takribani miezi miwili iliyopita.
Hata hivyo, habari kutoka kwa ndugu wa karibu wa Profesa Mwandosya aliyezungumza na gazeti hili jana, alisema kuwa Waziri huyo anaendelea vizuri.
Kuhusu taarifa za kuandika barua ya kujiuzulu, alisema kuwa Profesa Mwandosya hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo kwa maelezo kuwa suala la msingi kwa sasa ni kupitishwa kwa bajeti ya wizara yake ambayo iliwasilishwa bungeni juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira, ambayo mjadala wake utahitimishwa leo.
Makadirio hayo yalikuwa yapitishwe jana jioni, lakini kutokana na kifo cha Mbunge wa Baraza la Wawakilishi (CCM), Mussa Khamis Silima, kilichotokea jana baada ya kupata ajali juzi mkoani Dodoma ambayo ilimuua mkewe, Bunge liliahirishwa hadi leo ili kutoa fursa kwa wabunge kuomboleza.
Chanzo hicho cha habari kilieleza kuwa kwa mujibu wa wataalamu wa afya, upasuaji aliofanyiwa Profesa Mwandosya unampasa kupumzika hospitalini kwa miezi mitatu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: