Tarehe 21 Julai, mwaka huu, 2011, Katibu Mkuu Kiongozi Bwana Phillemon
Luhanjo, akitumia madaraka yake ya Mamlaka ya Nidhamu ya Watumishi wa
Umma, alitangaza hatua ya kumpa likizo ya malipo Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Bwana David Kitundu Jairo, ili kupisha uchunguzi
aliokuwa ameuagiza ufanyike dhidi yake.
Bwana Luhanjo
alichukua hatua ya kumsimamisha Bw. Jairo kufuatia tuhuma zilizokuwa
zimeelekezwa dhidi yake na baadhi ya wabunge wakati wa mjadala kuhusu
Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2011/12
katika kikao cha Bunge kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2011.
Katika
mjadala huo, baadhi ya wabunge walihoji uhalali wa Wizara kuomba
michango ya fedha kutoka kwenye Taasisi zilizoko chini ya usimamizi
wake ili kusaidia Bajeti ya Wizara hiyo kupita kwa urahisi.
Kufuatia
hatua hiyo ya kumsimamisha kazi Bw. Jairo, Katibu Mkuu Kiongozi
alimwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bwana
Ludovick Utouh kufanya ukaguzi maalum na uchunguzi wa awali juu ya
tuhuma hizo.
aliwasilisha Ripoti yake kwa Katibu Mkuu Kiongozi, na tarehe 23,
Agosti, 2011, Katibu Mkuu Kiongozi akiambatana na Bw. Utouh alitangaza
mbele ya waandishi wa habari matokeo ya ukaguzi huo maalum na uchunguzi
wa awali juu ya tuhuma dhidi ya Bw. Jairo.
Katika
Ripoti yake mbele ya waandishi wa habari, Bw. Utouh alihitimisha:
“Ukaguzi maalum haukuthibitisha kuwepo kwa usahihi wa tuhuma
zilizotolewa dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw.
David Kitundu Jairo.”
Kufuatia Ripoti hiyo ya Bw. Utouh,
Katibu Mkuu Kiongozi naye aliwaambia waandishi wa habari: “Matokeo ya
uchunguzi huo ni kwamba tuhuma zilizotolewa Bungeni tarehe 18 Julai,
2011, hazikuweza kuthibitika.
"Kutokana na matokeo haya
ya uchunguzi wa awali, mimi kama Mamlaka ya Nidhamu ya Katibu Mkuu,
Nishati na Madini, Bwana David Kitundu Jairo, sitaweza kuendelea na
hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma (notice) na Hati ya Mashitaka
kwa sababu Bwana David Kitundu Jairo, hajapatikana na kosa la kinidhamu
(disciplinary offence) kwa mujibu wa Taarifa ya Ukaguzi Maalum.”
Alihitimisha:
“Kufuatia matokeo ya taarifa hii ya awali na kwa mamlaka niliyonayo
kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya Utumishi Umma ya Mwaka 2002 na kanuni
zake za Mwaka 2003, NINAAMURU BWANA DAVID KITUNDU JAIRO AREJEE KAZINI
KUANZIA SIKU YA JUMATANO, TAREHE 24 AGOSTI, 2011.”
KURUGENZI
YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU, inapenda kutoa ufafanuzi kuwa baada ya
kupokea taarifa ya uchunguzi ya CAG na uamuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi
kuhusu suala hilo asubuhi ya tarehe 25 Agosti, 2011, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliamua kuwa
Ndugu Jairo asirudi kazini mpaka kwanza yeye Rais atapoamua namna gani
ya kurudi kazini, lini na wapi.
Katibu Mkuu Kiongozi
alifikisha uamuzi huo wa Rais kwa Ndugu David Jairo ambaye mapema
asubuhi ya siku hiyo alikuwa ameripoti kazini. Ndugu Jairo alitii
uamuzi huo wa Rais.
Tunapenda kusisitiza kuwa
Mheshimiwa Rais hajawa kigeugeu kwa sababu alifanya uamuzi mmoja tu
baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi. Na uamuzi huo
aliufanya kabla ya Bunge kulizungumzia suala hilo na hivyo uamuzi huo
wa Rais haukutokana na shinikizo la Bunge.
Pamoja na
kumweleza Katibu Mkuu Kiongozi, Rais pia alimfahamisha Waziri Mkuu
kuhusu uamuzi wake huo asubuhi hiyo ya tarehe 25, 2011.
Aidha,
tunapenda kufafanua zaidi kwamba Katibu Mkuu Kiongozi ametimiza wajibu
wake ipasavyo kama Mamlaka ya Nidhamu kwa Katibu Mkuu kwa mujibu wa
Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa
Rais, kwa upande wake, ametumia madaraka yake kama Mamlaka ya Ajira ya
Katibu Mkuu. Hakuna suala la kujichanganya wala ukigeugeu ndani ya
Serikali kuhusu suala hili.
Imetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
No comments:
Post a Comment