Hii ndio hali ilivyo leo Mivumoni na hakuna kinachofanyika kuzuia uharibifu zaidi wa mazingira
Ni matumaini yetu kuwa unaendelea vema na Hongera kwa kazi nzuri ya kuihabarisha jamii ya watanzania kupitia Blog yako.
Ankal, sisi wakazi wa Mivumoni Block 5 and 6 zaidi ya kero nyingi tunazokabiliwa nazo kama ya maji na barabara. KERO kubwa hapa MIVUMONI sasa hivi ambayo imekuwa inaleta usumbufu na kelele ni ya wachimba mchanga katika maeneo yetu ambayo wameyageuza kuwa machimbo rasmi na kuhatarisha mazingira kama inavyoonekana.
Tulikwishatoa taarifa juu ya jambo hili polisi, serikali ya mtaa, kwa mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kwa DC mwezi June. Lakini hadi hivi leo mwezi August watu hawa wanaochimba mchanga wanaendelea kuchimba mchanga na wamediriki hata kututishia sisi wananchi wa eneo hili la Mivumoni.
Na miongoni mwa malori haya yamo pia yasiyokuwa na namba kwa kweli inashangaza kuona jambo hili la uharibifu likiendelea na wahusika ambao tayari wamepelekewa taarifa wakiwa hawajafanya kile ambacho kinahitajika ili kukomesha jambo hili la uharibifu wa mazingira na haswa katika makazi ya watu.
Hivi ni kwa nini katika jambo hili ambalo limekwishaleta madhara baadhi ya WATENDAJI wanashindwa kuchukua hatua za haraka na za kinidhamu kwa waharibifu hawa? Je Manispaa na wizara au ofisi inayoshughulika na mazingira ambazo tayari walikwishapewa taarifa wanafanya nini? Sisi wananchi na walipa kodi ambao hata kodi ya viwanja tunalipa ambavyo ndivyo vinavyoharibiwa inatushangaza sana kuona jambo hili bado uharibifu huu ukiendelea.
Sasa sisi wananchi tumeshaharibiwa mazingira yetu pamoja na barabara na sasa eneo hili limekuwa ni hatari maana halina barabara na pia transforma iliyoko katika eneo hili inakaribia kuharibiwa na wachimba mchanga hawa WASIOFIKIRI na wasiojua wapi pa kuchimba mchanga.
Ndugu Michuzi, tunaomba ututolee taarifa hii kwenye blog yako ili wahusika na UMMA uelewe jambo hili na kulifanyia kazi haraka.
Asante,
Sisi wananchi wa Mivumoni Block 5& 6
Habari Kwa hisani ya Michuzi Blog
No comments:
Post a Comment