Friday, August 19, 2011

Mkurugenzi Mkuu Wa Wanyamapori Asimamishwa Kazi


Na Godfrey Mushi,Dodoma

SERIKALI imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Wanyamapori nchini, Obed Mbangwa na watumishi wengine wawili wa Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuruhusu kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma za kutoroshwa kwa wanyamapori 116 na ndege 16 kwenda nje ya nchi.

Wanyama hao wanadaiwa walikamatwa katika hifadhi za taifa na kutoroshewa nje ya nchi Novemba 26 mwaka 2010 kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Kufuatia sakata hilo,Waziri wa Maliasili na Utalii,Ezekiel Maige alitoa taarifa hiyo wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia bajeti ya makadirio na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2011/2012.

Maige, alisema serikali imeona ni vizuri imsimamishe kazi Mbangwa na watumishi wengine wawili kwa ajili ya kupisha uchunguzi kufanyika kuhusiana na tukio hilo.

Jana, Mbunge wa Simanjiro (CCM) Christopher Ole Sendeka alimlipua Mkurugenzi huyo kwamba alifanya madudu ambayo hayawezi kuvumilika na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya mtumishi huyo ambaye ni afisa wa ngazi ya juu ya Wizarani.

“Kuanzia leo tarehe 18 Agosti mwaka huu,tumeamua Obed Mbangwa na watumishi wengine wawili wa Wizara yangu wasimamishwe kazi lakini ataendelea kulipwa mshahara wakati akipisha uchunguzi kuhusu tuhuma za utoroshwaji wa wanyama hao,” alisema Waziri Maige huku akisisitiza kuwa amekasirishwa sana na kwamba anayo hasira kuliko kipindi chotealichokuwa katika utumishi wa umma.

Kuhusu madai ya kuwepo kwa mipango ya wawekezaji kupewa kibali cha kujengwa Hoteli ya nyota tano (Five Star) katika mapito ya faru,Waziri Maige alisema kuwa hata serikali nayo haita kubali hoteli hiyo ijengwe katika eneo hilo.

Madai ya eneo hilo kujengwa Hoteli ya nyota tano yaliibuliwa juzi jioni mjini hapa na mbunge wa Jimbo la Ngorongoro,(CCM) Kaika Telele baada ya kudai kwamba Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM, Pius Msekwa amevuka mipaka ya madaraka yake ya Uenyekiti wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) na anatumia jina la Rais Jakaya Kikwete vibaya kuwapatia wawekezaji maeneo ya kujenga hoteli katika hifadhi hiyo.

Telele alisema kuwa waliwahi kuomba eneo hilo ili wajenge shule ya sekondari kwa ajili ya wanafunzi wa jamii ya kimasai lakini walizuiwa kwakuwa ni eneo la hifadhi ambalo ni mapito ya faru lakini Msekwa alikuja na kusema ametumwa na JK kufanya anayoyafanya,hatumwogopi hata kidogo,

Alisema na kuongeza: “Hatuwezi kuvumilia jambo hilo hata kidogo anatumia hata umakamu Mwenyekiti wake wa CCM kufanya hayo anayoyafanya,Waziri tunaomba tume kwa ajili ya kuchunguza suala hili na kama una uwezo uvunje bodi na kuchagua nyingine.

No comments: