Saturday, August 13, 2011

Mwenyekiti wa CCM apigwa risasi

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, Juma Dewiji, amenusurika kufa baada ya kupigwa risasi na mtu asiyejulikana.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 2:00 usiku nyumbani kwa Dewji eneo la Urasa takriban kilomita tano nje ya mji wa Urambo.
Dewji aliliambia NIPASHE kwenye makazi yake mengine katika Kijiji cha Mwongozo jana kuwa alishambuliwa kwa kupigwa risasi muda mfupi baada ya kurejea nyumbani kwake kwa ajili ya kufuturu kutoka katika kamati za Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Urambo ambalo lilikutana jana mjini Urambo.
Mwenyekiti huyo akizungumza baada ya kutoka katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo alikokimbizwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kupatiwa mabibabu, muda mfupi baada ya kupigwa risasi, alisema alipigwa risasi hiyo na mtu ambaye hakumfahamu.

Akisimulia tukio hilo huku akisema hajui sababu za kutendewa unyama huo, alisema mtu asiyejulikana alimrushia risasi ya kwanza ikamkosa kichwani na ya pili ikimpata begani.
Dewji alieleza kuwa mtu aliyempiga risasi alifika nyumbani kwake akiwa katika gari dogo, lakini hakuzishika namba za gari hilo.
Hata hivyo, Dewji alisema baada ya mtu huyo kumshambulia kwa risasi na kutoweka, wananchi walisikia milio ya risasi na kufika nyumbani kwake kisha walipiga simu polisi ambao walifika muda mfupi na kuokota risasi mbili zilizogonga ukuta pamoja na maganda yake.
Alisema wakati anapigwa risasi, alikuwa amejilaza katika mkeka nje ya nyumba yake na kwamba hapakuwepo na mtu yeyote kwani wote walisambaa baada ya kufuturu.
Alisema polisi ndio waliookoa maisha yake kwa kumpeleka katika Hospitali ya Wilaya Urambo ambapo alipewa matibabu na kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Alisema hakuna mtu anayemhisi kuhusika na tukio hilo kwa sababu katika maisha yake hajawahi kugombana wala kuwa na uhasama na mtu yeyote.
Hata hivyo, alisema pengine msimamo wake wa kutetea haki za wananchi katika masuala ya kudhulumiwa fedha na mali na hasa katika kilimo, unaweza kuwa moja ya sababu.
Baadhi ya wananchi waliofurika nyumbani kwake kumjulia hali kutokana na mkasa uliompata, walilaani kitendo hicho.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Anthony Rutta, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa upelelezi umeanza kwa ajili ya kuwanasa waliohusika kufanya uhalifu huo.
Tukio hilo limetokea wakati CCM ikitarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wake katika ngazi mbalimbali mwakani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: