Wednesday, August 10, 2011

Neno La Leo; Dhiki Ya Mafuta Na Kisa Cha Mwenye Koroboi!


Ndugu zangu,

SAA tano hii ya usiku nimetoka kuhemea mafuta. Nimeyakosa. Iringa yote haina mafuta, hata mafuta ya taa. Kesho Jumatano alfajiri nimepanga safari muhimu kuteremka kwetu bondeni. Ni bonde la Usangu kule Mbarali, Mbeya.

Na safari yenyewe imeanza kuwa ngumu kabla sijaianza. Mafuta yaliyomo kwenye ’ Chuma chakavu’ niendeshacho ni robo tenki. Nikiwa na bahati yatanifikisha Mafinga tu, baada ya hapo? Inshallah, EWURA inajua!

Na katika dhiki hii ya mafuta, kuna Watanzania wanaolala gizani. Kisa? Si umeme wa TANESCO maana hawajawahi kuwa wateja wa Tanesco kwa vile gharama za umeme hawazimudu. Hawa ni watumiaji wa koroboi na wateja wa kuaminika wa mafuta ya taa. Ni Watanzania wenzetu wa kule Kihesa, Mlandege, Nyamagana, na kwingineko.

Na mafuta ya taa nayo yamekuwa ghali kwao. Kuna wakati wanalala giza si kwa kupenda, bali hawana elfu mbili na mia mbili za kununulia lita ya mafuta ya taa.

Naam, Dr Remmy aliimba;
” Maisha yamekuwa magumu, nashindwa la kufanya
Kila kitu cha shida, kulala kwa shida
Kula kwa shida, Kuvaa kwa shida,”

Dr Remmy angekuwa hai angeongeza; ”Umeme sina, na mafuta ya taa ni shida!”
Ndio, na nikiwa njiani kurudi nyumbani bila mafuta nikakumbuka kisa cha zamani sana. Ni cha bwana mwenye koroboi iliyokaukiwa mafuta. Bwana yule hakuwa na pesa ya kununulia mafuta. Giza nalo halisubiri mafuta ya taa. Bwana yule akaumiza kichwa kufikiri ni kwa namna gani angeisitiri familia yake na giza la usiku huo.

Akamtuma mwanae aende dukani kwa Mpemba. Akamwelekeza mwanawe; ” Ukifika dukani mwambie Mpemba akujazie kwanza mafuta ya taa kwenye koroboi. Akimaliza mwambie baba amesema atalipa kesho.”

Mtoto yule akaenda zake dukani na akafanya kama alivyoagizwa. Mpemba aliposikia kuwa pesa yake italipwa kesho, basi, kwa hasira akachukua koroboi n a kumimina mafuta yake.

Mtoto akarudi nyumbani. Kwa vile utambi wa koroboi ulishaloana mafuta ya taa, basi, mzazi yule akachukua kiberiti na kuwasha koroboi ile. Ikawaka na kutoa mwanga uliotosha kuepuka aibu ya kula mlo wa jioni gizani.

Naam, na nchi yetu nayo imekumbwa na dhiki ya mafuta. Matajiri wenye makampuni yao ya mafuta si kama Mpemba yule mwenye duka. Hawa matajiri wa mafuta wamekuwa wakali kweli. Na tatizo letu kama nchi hatuna hata koroboi yenye utambi.

Na hata tungekuwa nayo, matajiri hawa wa mafuta wangehakikisha wanamimina mafuta yao na kukamua utambi wa koroboi ya nchi yetu mpaka tone la mwisho la mafuta yao.

Ndio, tukome ’ kukomaa’ na ubishi wetu, au?

Maggid,
Iringa, Jumanne, Agosti 9, 2011

No comments: