Saturday, August 27, 2011

SPIKA ANNE MAKINDA AUNDA TIMU YA KUMCHUNGUZA JAIRO


SPIKA wa Bunge, Anne Makinda ameunda kamati ya watu watano kuchunguza 
mambo kadhaa yanayohusiana na sakata la Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na
Madini, David Jairo, kukusanya shilingi bilioni moja kwa ajili na
kufanikisha uwasilishaji wa bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha
2011/2012.

Makinda ameiagiza kamati hiyo ifanye kazi kwa muda usiozidi wiki
nane na anatarajia kwamba itafanya kazi kwa kuzingatia Katiba ya nchi,
sheria na taratibu, na itatoa haki kwa watu wote.

Amewataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Mbunge wa Tunduru
Kaskazini, Ramo Makani (CCM), Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes (CCM),
Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (Chadema), Mbunge wa Gando,
Khalifa Suleiman Khalifa(CUF), na Mbunge wa Viti Maalum, Martha Umbula
(CCM).

Makinda amewaeleza wabunge kuwa, kamati hiyo inapaswa kuchunguza
utaratibu uliotumika kukusanya fedha kwa ajili ya kufanikishwa
kupitishwa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, sanjari na uhalali wa
utaratibu huo kisheria na kikanuni.

Kamati hiyo inapaswa pia kuchunguza kama fedha zilizokusanywa
zinakasimiwa katika bajeti husika, na ichunguze matumizi halisi ya fedha
zilizokusanywa.

Makinda ameiagiza kamati hiyo ichunguze taarifa ya Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu uchunguzi kuhusiana na
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini kukusanya fedha katika idara
zilizo chini ya Wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha kuwasilisha bajeti
ya Wizara hiyo.


Kamati hiyo pia inapaswa kuchunguza mfumo wa Serikali kujibu hoja
zinazowasilishwa bungeni, na kubaini kama utaratibu huo unaathiri dhana
ya madaraka ya Bunge.


Makinda kaagiza pia kwamba, kamati iangalie nafasi ya mamlaka ya
uteuzi kwa ngazi ya makatibu wakuu katika kushughulikia masuala ya
kinidhamu kwa anaowateua na pia kuangalia mambo mengine yoyote
yanayohusiana na mambo hayo.



Amewasifu wabunge kwa kufanya kazi nzuri katika mkutano wa Bunge
uliokwisha leo mjini Dodoma, na kwamba walivumiliana, walisikilizana na
kufanya kazi pamoja.

Am esema, Bunge hilo lilipoanza lilianza kama Ze Comedy, lakini
linaelekea kuwa imara, na litafanya kazi ipasavyo kuisimamia Serikali.

Amewataka wabunge wasiwe na chuki au uadui na wanaoongoza vikao vya Bunge, kwa kuwa hakuna aliye na chuki na yeyote.

“Chuki na hila mziache hapa, na ziozee humu…mkiwa hapa mwenzio
akisema usijenge uadui.. kwa waliokwazwa naomba tusameheane” amesema
Makinda kabla ya kusitisha shughuli za Bunge hadi Novemba 8 mwaka huu. 

No comments: