Mheshimiwa Spika,
- Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kulishukuru Bunge lako tukufu kwa kunipa fursa hii ya kutoa taarifa kuhusu hali ya biashara ya mafuta ya petroli hapa nchini.
- Kama tunavyofahamu, mafuta ya petroli ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu kwani viwanda, vyombo vya usafiri, na huduma nyinginezo nyingi hutegemea mafuta na bidhaa zake. Bei ya mafuta inapopanda, bei zingine nyingi hupanda kwa mfano bei za usafiri zinapanda, bei za vyakula zinapanda, bei za bidhaa za viwandani zinapanda; nakadhalika.
- Mheshimiwa Spika, tarehe 22 Juni 2011 Serikali, kupitia kwa Waziri wa Fedha wakati akihitimisha Hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/12, alitoa maagizo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuchukua hatua mbalimbali zitakazochangia kupunguza bei za mafuta. Hatua ambazo ziliagizwa kuchukuliwa ni pamoja na:
- Ukokotoaji wa thamani ya shilingi kwa kuioanisha na Dola ya Marekani (yaani Exchange rate);
- Kuondoa au kupunguza wigo wa asilimia 7.5 ambayo makampuni yaliruhusiwa kuwekwa ili kufidia baadhi ya gharama;
- kupitia upya misingi ya ukokotoaji wa viwango vya tozo mbalimbali za taasisi za Umma kwa lengo la kubakia na tozo stahili na kwa viwango stahili bila kuathiri majukumu ya udhibiti ma usimamizi yanayofanywa na Taasisi hizo;
- kupunguza tozo za kampuni za mafuta ikiwa ni pamoja na gharama za kibenki (yaani Financiang Charges); na
- Upotevu wa mafuta yanayosafirishwa kwenye meli na gharama ya ukaguzi (yaani inspection fee).
HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI
- Serikali kupitia EWURA ilianza mara moja mchakato wa kurekebisha Kanuni ya ukokotoaji wa bei za mafuta hapa nchini kwa lengo la kuleta unafuu wa bei kwa mlaji. Hatua ya kwanza ilikuwa kuandaa hoja (discussion paper) ambayo ilitoa mapendekezo ya maeneo mbalimbali yanayofaa kurekebishwa ili kupata maoni ya wadau wa sekta ya mafuta. Mapendekezo hayo yalizingatia maagizo ya Serikali pamoja wa ushauri mbalimbali wa wadau katika sekta ya mafuta hapa nchini.
USHIRIKISHAJI WADAU
- Mchakato wa kupata maoni ya wadau (taftishi) ulianza tarehe 4 Julai 2011 na kukamilika tarehe 26 Julai 2011. Kwa kawaida, mchakato huo ungechukua siku 81 lakini kutokana na unyeti wa suala hili, Mamlaka ililazimika kuufupisha hadi siku 23.
- Mkutano wadau uliitishwa tarehe 22 Julai 2011 ili kupitia rasimu ya kanuni pamoja na jedwali la uchambuzi wa maoni ya wadau lililoandaliwa na EWURA. Wadau walioshirikishwa katika taftishi hiyo ni pamoja na makampuni ya mafuta, Baraza la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na EWURA (Consumer Consultative Council), Baraza la Ushauri la Serikali, Taasisi za Umma kama vile TRA, TBS, WMA, TPDC, TPA, SUMATRA, na TIPER. Maoni mbalimbali ya wadau yalipokelewa na kuchambuliwa na EWURA ikiwa ni pamoja na kupata maoni ya wataalam kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Uchumi, Shirika la Maendeleo ya Mfuta Tanzania (TPDC), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, EWURA na Makampuni ya Mafuta.
- Tarehe 23 Julai 2011, EWURA iliitisha kikao cha wawakilishi wa wadau wakubwa ambao ni pamoja na CCC, TPDC, TPA, Wizara ya Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu na baadhi ya makampuni ya mafuta kupitia mapendekezo yaliyokuwepo na kutoa maoni ya mwisho kabla ya kuwasilishwa kwenye Bodi kwa maamuzi.
MAAMUZI YA EWURA
- Tarehe 26 Julai 2011, Bodi ya Wakurugenzi ya EWURA ilikaa na kupitia mapendekezo ya marekebisho ya vipengele mbalimbali vya kanuni ya kukokotoa bei ya mafuta. Maamuzi hayo ya Bodi yamepelekea punguzo la bei za mafuta kwa viwango vifuatavyo: Petroli TZS 202.37; Dizeli TZS 173.49; na Mafuta ya Taa TZS 181.37. Mabadiliko haya ya bei ni sawa na punguzo la asilimia 9.17; 8.31; na 8.70 kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa sawia. Kanuni hii ya kukokotoa bei za mafuta imeanza kutekelezwa kuanzia tarehe 03 Agosti 2011.
- Tarehe 3 na 4 Agosti 2011 makampuni ya mafuta yaliwasilisha kutoridhishwa na maamuzi yaliyofanywa na EWURA hususan kuhusu kupunguzwa kwa wigo wa asilimia 7.5; margins za makampuni ya mafuta, na gharama za kuchelewesha meli bandarini (demmurage charges).
- Kufuatia vikao hivyo vya Serikali, makampuni pamoja na EWURA siku ya Ijumaa tarehe 5 Agosti 2011, Mamlaka ya EWURA ilifanya marekebisho mengine katika vipengele vifuatavyo:
- Gharama za ucheleweshaji meli bandarini (demmurage charges) ziliongezwa kutoka wastani wa TZS 1.85 kwa lita hadi TZS 8.76 kwa lita.
- Viwango vya faida kwa kampuni za mafuta (OMCs margins) ziliongezwa kutoka TZS 108.69 kwa lita hadi TZS 110.57.
HALI YA UPATIKANAJI NA USAMBAZAJI MAFUTA BAADA YA KUANZA KUTUMIKA KWA KANUNI MPYA
- Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini imeendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bishara ya mafuta hapa nchini. Ufuatiliaji uliofanywa kwenye maghala ya kuhifadhia mafuta umedhihirisha kuwa kuna mafuta ya kutosha hapa nchini na pia kuna meli kadhaa ambazo zipo nje ya gati zikisubiri kupakua mafuta. Aidha, makampuni ya mafuta yameuza mafuta kwa wingi siku ya Ijumaa tarehe 5 Agosti 2011.
- Hadi Ijumaa tarehe 05.08.2011, kiasi cha mafuta yaliyokuwepo katika maghala ya baadhi ya makampuni ya mafuta yaliyokaguliwa ni lita milioni 191.813 ambayo inakidhi matumizi ya nchi kwa kati ya siku 8 hadi 67 kulingana na aina ya mafuta kama inavyoonekana kwenye jedwali Na. 1 hapa chini:
Jedwali 1: Mafuta yaliyoko Nchini tarehe 05 Agosti 2011
Maelezo | Mafuta ya Petroli | Mafuta ya Dizeli | Mafuta ya Taa | Mafuta ya Ndege | Mafuta Mazito |
Akiba iliyopo(lita) | 41,934,139 | 92,650,300 | 41,227,870 | 4,384,297 | 10,805,070 |
Wastani wa Matumizi kwa siku | 875,000 | 3,100,000 | 615,240 | 560,500 | 1,087,695 |
Makadirio ya siku za kutumika | 48 | 30 | 67 | 8 | 10 |
MAUZO YA MAFUTA KWENYE MAGHALA (JUMLA)
- Takwimu zilizowasilishwa EWURA na mkandarasi anayeweka vinasaba katika mafuta yauzwayo hapa nchini (GFI) na kuhakikiwa na wakaguzi wa EWURA zinaonesha kuwa kwa siku ya Ijumaa tarehe 5 Agosti 2011 mauzo ya mafuta kutoka kwenye maghala (depots) yalikuwa ni malori 329 kwa aina mbalimbali za mafuta, kwa ajili ya soko la ndani.
- Tarehe 3 Agosti walipakia malori 40 wakati tarehe 4 Agosti 2011 yalipakiwa malori 185. Kwa kawaida, wastani wa mauzo kwa siku ni takriban malori 250 hadi 300. Takwimu hizi zinadhihirisha kuwa kuanzia tarehe 5 Agosti 2011, mauzo ya mafuta yameongezeka na kufikia kiwango cha kawaida.
- Katika hali ya kawaida, makampuni mengi ya mafuta hayafanyi kazi katika siku za mapumziko. Kwa hiyo, siku ya Jumamosi tarehe 6 Agosti 2011, jumla ya malori 115 yalipakia mafuta.
MAUZO YA MAFUTA KWENYE VITUO (REJAREJA)
- Ukaguzi uliofanywa na EWURA kwenye vituo vya mafuta jijini Dar es Salaam na baadhi ya mikoa unaonesha kuwa vituo vingi vilianza kuuza mafuta kama kawaida. Ukaguzi huo pia umehusisha kupata takwimu za mafuta yaliyopo kwenye vituo ili kuhakikisha kuwa hakuna kituo kinachohodhi mafuta na kuacha kuuza. Kuna baadhi ya vituo vilikuwa vikisubiri kupata mafuta kwa vile walikuwa wameishiwa, hasa kwa sababu makampuni ya mafuta hayakuuza mafuta kwa kiwango cha kawaida siku ya tarehe 3 na 4 Agosti 2011.
- Makampuni mengi yaliendelea kupakia malori ya mafuta mpaka usiku 5 Agosti 2011 hivyo ilitarajiwa kwamba kungekuwa na usambazaji mwingi zaidi kwenye vituo kuanzia Jumamosi tarehe 6 Agosti 2011.
VIWANGO VYA BEI
- Ukaguzi uliofanywa na EWURA unaonesha kuwa bei za mafuta kwenye vituo vinavyouza mafuta zimezingatia bei kikomo zilizotolewa na Mamlaka ya EWURA tarehe 3 Agosti 2011. Ukaguzi huo umefanyika katika miji ya Arusha, Moshi, Dar es Salaam na Dodoma. Aidha, hakuna taarifa zilizopokewa na EWURA kutoka mji wowote kuhusu kukiukwa kwa bei kikomo iliyopo sasa.
HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA SERIKALI
- Mheshimiwa Spika, bidhaa za mafuta ya petroli inatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi katika nchi zote duniani. Upatikanaji wa uhakika wa mafuta na kwa bei stahili vitafanya uchumi wa nchi yetu kukua kwa kasi zaidi na kuwa endelevu.
- Serikali inachukua hatua zifuatazo ili kuhakikisha kuwa mafuta ya kutosha yanapatikana sehemu zote nchini.
- Serikali kupitia EWURA inafuatilia mwenendo wa usambazaji wa mafuta kutoka katika maghala ya makampuni ya mafuta kwenda kwenye vituo vya mafuta;
- Serikali kupitia EWURA itachukua hatua za kisheria kwa kampuni zilizokiuka masharti ya leseni na kusababisha uhaba wa mafuta kwenye vituo vya kuuza mafuta nchini;
- Leo Serikali kupitia EWURA imeipa leseni COPEC kampuni tanzu ya Serikali kupitia TPDC kuanza kufanya biashara ya mafuta mara moja; na
- Serikali kwa kupitia EWURA imekamilisha taratibu za uagizaji wa mafuta kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa mafuta yanapatika na kwa gharama nafuu zaidi wakati wote.
- Mheshimiwa Spika, kufuatia hali iliyojitokeza, EWURA imetoa Compliance Order kwa makampuni manne ambayo ni BP, Engen, Oilcom na Camel Oil, ambapo wanatakiwa watekeleze hatua zifuatazo:
- Mara moja wanatakiwa kuanza kutoa huduma katika maghala yao ikiwa ni pamoja na kuanza kuuza mafuta katika vituo vya rejareja ikiwemo vituo vilivyo chini ya miliki zao;
- Waache mara moja kitendo chochote kitakachosababisha upungufu wa makusudi wa mafuta ya petroli katika soko la Tanzania; na
- katika kipindi cha masaa 24 wajieleze kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria dhidi yao kwa kukiuka matakwa ya Sheria ya Mafuta pamoja na Sheria ya EWURA.
- Mheshimiwa Spika, baada ya kuisha kwa muda uliotolewa na EWURA, adhabu stahiki zitatolewa kwa wahusika ikiwa ni pamoja na kusitisha ama kufuta leseni.
- Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida na kwa mujibu wa Sheria, mtu asiporidhika na maamuzi ya EWURA anapaswa kukata rufani katika Baraza la Ushindani(Fair Competition Tribunal). Hatua hii haijafuatwa hadi sasa na Serikali ingeshauri kwamba masuala kama haya ni vema yakafuata taratibu za kisheria.
- Mheshimiwa Spika; naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment