Baharia Rashid Said Rashid wa meli ya Mv. Spice Islander, iliyozama na kuua takribani watu 240 huku wengine 619 wakinusurika visiwani Zanzibar juzi, amesema waligawa maboya ya kujiokoa kwa abiria na kuwavalisha watoto kisha kuwaondoa melini kupitia madirishani kabla ya kuzama.
Akizungumza na NIPASHE akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, jana, alisema kabla ya meli hiyo iliyokuwa na mabaharia 12 kuzama majira ya saa 7:00 usiku wa Ijumaa iliyopita eneo la Nungwi, waliomba msaada kwa meli nyingine iliyokuwa inapita lakini hawakufanikiwa.
Said ambaye ni mkazi wa Shangani, alisema baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya kabla ya meli kupinduka, abiria walimtaka nahodha atoe taarifa kwao kama meli inazama na alifanya hivyo.
“Tulijaribu kufanya kila jitihada ili kuokoa hali hiyo, lakini tulishindwa na tukaamua tuiache meli na kuanza kutoka, hapo tena kila mmoja alikwenda kwa upande wake,” alisema.
Hata hivyo, alisema hafahamu kama mabaharia wenzake na nahodha wapo salama au wamekufa kwa sababu mara ya mwisho aliwaona kabla ya chombo kupinduka na kuzama.
“Kwa kweli siwezi kusema kama ni uzembe au la umefanyika, lakini wakati inatokea hali hii tulipishana na meli ya MV Jitihada na kuwapa ishara ya kuzama, lakini hawakutusaidia,” alisema baharia huyo.
Alisimulia kuwa walichukua jitihada mbalimbali za kuwapa ishara, lakini hawakufanikiwa na hawezi kusema kama walidharau au hawakuwaelewa walichokuwa wakikitafuta kutoka kwao.
IDADI YA VIFO YAFIKIA 240
Hadi jana taarifa rasmi zilizema kuwa watu waliokufa katika ajali hiyo baada ya meli kuzama wamefikia 240.
Meli hiyo ilizama majira ya saa 7:00 usiku ilipokuwa ikitokea jijini Dar es Salaam kupitia Unguja ikielekea Pemba.
Takwimu hizo zilitolewa jana na Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, wakati akitoa maelezo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema, ambaye alifuatana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Devis Mwamunyange.
Mwema alisema Serikali imeamua kupeleka wazamiaji kutoka nje ya nchi kusaidia kuchunguza kujua kama ndani ya meli hiyo kuna maiti zilizobaki.
Alisema Serikali imeamua kuzika maiti 39 baada ya kutotambuliwa na wahusika na kwamba kazi hiyo ilifanyika usiku wa kuamkia jana katika eneo la Kama, Wilaya ya Magharibi Unguja.
Aidha, alisema meli hiyo ilizama ikiwa na tani 160 za mzigo, ambapo tani 65 zilipakiwa katika bandari ya Dar es Salaam, wakati tani 95 zilipakiwa katika bandari ya Malindi.
SERIKALI: MELI ILIPAKIA KUPITA UWEZO
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) imethibitisha kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba abiria kupita uwezo wake kabla ya kupinduka na kuzama.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, alisema meli hiyo ina uwezo wa kuchukua abiria 600 na mizigo tani 500.
Hata hivyo, kabla Jeshi la Polisi halijatangaza idadi ya watu 240 waliofariki, Waziri Aboud, alisema watu 619 wamepatikana wakiwa hai na 197 wamekufa.
Waziri Aboud alisema orodha ya abiria inaonyesha abiria 610 ndio waliopandia katika bandari ya Zanzibar na abiria 166 walipandia katika bandari ya Dar es Salaam wakiwemo watoto 65.
Hata hivyo, takwimu hizo zinajikanganya, wakati idadi ya awali ya waziri inaonyesha meli ilikuwa na watu 816, idadi ya pili inaonyesha walikuwa 841.
Aidha, alisema kwamba majeruhi mmoja anatarajiwa kuhamishiwa Dar ss Salaam kufuatia hali yake kuwa mbaya akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
“Hali yake sio nzuri atapelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi na kati ya watu 319 waliofikishwa hospitali ni watano tu ndio wanaendelea na matibabu,” alisema.
MAKABURI 134 YACHIMBWA
Waziri Aboud alisema Serikali imeshachimba makaburi 134 katika eneo la Kama ambayo yatatumika kuzika watu ambao hawatotambuliwa na ndugu zao.
Alisema kuna baadhi ya wananchi hawajawaona ndugu zao na kwamba Serikali itaendelea na operesheni ya kuwatafuta na kuwataka wananchi ambao wamewakosa ndugu zao watoe taarifa kwa wakuu wa wilaya na mikoa.
UWANJA WA MAISARA WAFUNGWA
Waziri Aboud alisema kuanzia jana kituo cha kutambua maiti cha Maisara kimefungwa na maiti zote zitakazopatikana zitazikwa katika maeneo walipopatikana kwa kuwa zitakuwa zimeharibika, lakini kumbukumbu zitawekwa kwa lengo la kuwatafuta jamaa zao.
DK. SHEIN KUONGOZA HITIMA LEO
Aboud alisema Serikali itasoma dua maalumu (Hitma) leo katika viwanja vya Maisara kuwaombea waliofariki na itaongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Hata hivyo, alisema pamoja na Serikali kutangaza maombelezo ya siku tatu, wafanyakazi wataendelea na kazi kama kawaida na dua hiyo itafanyika kuanzia majira ya alasiri na kuwataka wananchi kujitokeza.
NAHODHA ATOWEKA, MHANDISI MKUU ANAHOJIWA
Alisema nahodha wa meli hiyo, Said Kinyenyeta, hajapatikana, lakini fundi mkuu wa meli hiyo, Injima Mkune, anahojiwa na Polisi.
Waziri huyo, aliongeza kusema kuwa, Serikali tayari imeshaamua kuunda kamati ya kuchunguza tukio hilo na hatua kali zitachukuliwa iwapo kutabainika kuna uzembe umefanyika.
NSSF YATOA SH. MILIONI 13
Wakati huo huo, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamaii (NSSF) umetoa Sh. milioni 13, ambapo milioni 10 zitaenda serikalini na milioni tatu kwa shughuli ya hitma.
Fedha hizo zilikabidhiwa na Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu, ambaye alisema ,fuko huo imeguswa na msiba huo na kuamua kutoa mkono wa pole kwa wafiwa na waathirika wa tukio hilo.
Aidha, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar umetoa Sh. milioni 10 ambazo zilikabidhiwa na Ofisa Uhusiano wa mfuko huo, Raya Hamdani na Kampuni ya Simu za Mkononi ya TIGO imechangia chakula chenye thamani ya Sh. milioni tano.
SERIKALI YA MUUNGANO YATOA SH. MILIONI 300
Kadhalika, Aboud, alisema Serikali ya Muungano imetoa Sh. milisoni 300 na kufafanua kuwa zitakabidhiwa leo na kutumika kwa shughuli mbali mbali za kufanikisha msiba huo.
Wakati huo huo Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe, amesema jukumu la kusimamia usalama wa abiria na mizigo kwa vyombo vya usafiri baharini sio jukumu lake.
Alisema jukumu hilo ni la Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar, ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa sheria baada ya kuondolewa Mamlaka ya Usafiri Baharini na Nchi Kavu Tanzania (Sumatra)
Alisema kwamba mamlaka hiyo ndiyo iliyopewa jukumu kisheria kufanya ukaguzi wa abiria na mizigo kabla ya meli kuondoka bandarini Zanzibar.
“Nalaumiwa bure, kazi ya Shirika la Bandari ni kupakia mizigo na kupakua na sio vinginevyo,” alisema wakati akizungumza na NIPASHE na kuongeza:
“Sina chochote cha kusema kuhusu kuzidi abiria watafuteni wahusika Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar.”
Hata hivyo, juhudi za kumpata Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafirishaji Baharini, Vuai Haji, ofisini kwake hazikuzaa matunda kutokana na mara kwa mara simu yake ya kiganja kutopokewa.
MAALIM SEIF: SERIKALI ITACHUNGUZA
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema serikali itafanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha ajali hiyo.
Maalim Seif alisema hayo baada ya kushiriki maziko ya baadhi ya waliokufa katika ajali hiyo huko Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi Unguja.
Maalim Seif alisema idadi ya abiria waliokuwemo katika meli hiyo ilikuwa kubwa tofauti na idadi ya kitaalamu inayotakiwa kubebwa na chombo hicho.
Alisema suala hilo linahitaji kuangaliwa kwa umakini mkubwa kwa vile linaweza kuwa ndio chanzo cha kuzama kwa meli hiyo.
“Kwa ufupi, meli ilikwisha zama hata kabla ya kuondoka,” alisema Maalim Seif na kuongeza kwamba: “Pamoja na kuwa hii ni ajali ya Mwenyezi Mungu, serikali tutahakikisha sheria zinafuatwa ili kujua ukweli wa tukio hili.”
Alisema Sheria ya nchi ya Mamlaka ya Usafirishaji Baharini inawapa uwezo maafisa wa ukaguzi kuzuia chombo kuondoka kama kimezidisha abiria, lakini meli hiyo ilizidisha abiria na kuondoka kinyume cha sheria.
Alitoa wito kwa wananchi wasilazimishe kusafiri na meli ambazo zimeshafikisha idadi zilizoruhusiwa ili kuepukana na maafa yanayoweza kutokea.
Tangu kutokea tukio hilo, Maalim Seif, amekuwa akienda kuwapa mkono wa pole wafiwa na watu walioathirika na ajali hiyo.
Julai mwaka huu, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Hamad Masoud, aliwasilisha taarifa maalumu ya Serikali katika Baraza la Wawakilishi na kutetea vyombo vya usafiri baharini Zanzibar kuwa havihatarishi usalama wa abiria kwa vile sio vichakavu na kuvitaka vyombo vya habari kuacha kuwatisha wananchi baada ya meli saba kupata matatizo ya kiufundi wakati zikisafiri kati ya Pemba, Unguja na Dar es Salaam.
Juhudi za kumpata Waziri Masoud tangu kutokea tukio hilo hazikuzaa matunda kwani simu yake ya mkononi hakupatikana, kuna taarifa kuwa yuko nje ya nchi kikazi.
JK ATAKA DNA ITUMIKE
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameagiza sayansi ya vinasaba (DNA) itumike kusaidia zoezi la utambuzi wa miili ya watu waliopoteza maisha yao katika ajali hiyo.
Alisema Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama ilikuwa inakutana jana, Zanzibar, chini ya uenyekiti wake kutathmini hali ilivyo.
Vile vile, Rais Kikwete ametoa shukurani kwa wanakijiji cha Nungwi, vyombo vya ulinzi na usalama nchini pamoja na taasisi nyingine nchini kwa jitihada zao katika kuokoa maisha ya watu waliokumbwa na ajali hiyo.
Rais Kikwete ametoa agizo hilo la matumizi ya vinasaba jana wakati alipotembelea kituo na eneo la maafa la Nungwi kilichoko kwenye kijiji cha Nungwi.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini, Unguja, Pembe Khamis, alimweleza Rais Kikwete kuwa habari walizonazo ni kwamba meli hiyo ilianza kuzama kati ya saa sita na saa saba usiku Ijumaa.
Pembe Khamis alisema kuwa kituo hicho cha maafa cha Nungwi kilipokea miili 134 na majeruhi kiasi cha 78 na kwamba zoezi la kutafuta waliookoka na waliopoteza maisha katika ajali hiyo inaendelea leo.
Akiwashukuru madaktari na wataalamu wengine wa afya na sekta nyingine ambazo wamekuwa wanashiriki katika zoezi la uokoaji, kuhudumia waliokolewa pamoja na kuziweka katika hali nzuri maiti za watu waliopoteza maisha yao, Rais Kikwete, ambaye alikaa kwenye kituo hicho cha maafa kwa dakika karibu 40 amewaambia:
“Nawashukuru sana kwa kazi kubwa mliyoifanya, kwa yote mliyoyafanya na kwa moyo nzuri mliouonyesha. Mimi nimekuja kuungana nanyi kuwashukuru kwa kazi hiyo.”
Kuhusu kasi ndogo ya zoezi la utambuziwa maiti, Rais alisema kwa jinsi zoezi hilo linavyokwenda inawezekana kabisa kuwa siyo miili yote itatambuliwa na jamaa na ndugu zao kabla ya kulazimika kuizika na hivyo aliagiza itumike sayansi ya vinasaba kuweka kumbukumbu za waliopoteza maisha yao.
“Kila maiti ichukuliwe sampuli ya DNA (vinasaba) na ikitokea kuwa pengine ndugu zake wamechelewa kuja kuitambua basi akifika hata kama mwili tayari umezikwa aweze kutambua kuwa ndugu yake alipoteza maisha katika ajali ya meli hiyo.”
Hata baada ya kuambiwa na mtaalam wa utambuzi wa magonjwa na uchunguzi wa magonjwa na vyanzo vya kifo, Dk. Ahmad Makata, kuwa walikuwa wanaipiga picha miili yote na kuhifadhi nguo za wote waliopoteza maisha kama namna ya kuweka kumbukumbu, Rais Kikwete bado alielekezalekeza:
“Miili ya binadamu hubadilika na kuharibika haraka, kwa kasi kubwa na katika muda mfupi. Miili ile ya ajali ya Mv Bukoba ilibadilika na kuwa myeupe katika kipindi kifupi sana. Hivyo, naagiza tutumie vinasaba katika kuweka kumbukumbu. Si mnao wataalam wa vinasaba katika timu yenu?”
Ameongeza Rais Kikwete: “Tufanya DNA profile ya miili yote ambayo haijatambuliwa. Huko mbele, hii itasaidia kuepukana na kuwa na makaburi ya watu wasiotambuliwa kabisa kwa sababu inawezekana kuwa baadhi ya ndugu ya wale waliopoteza maisha katika ajali hiyo wanaweza kuchelewa kufika kufanya utambuzi kabla ya miili kuzikwa.”
Miongoni mwa waliompokea Rais Kikwete kwenye kituo hicho cha maafa ni pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama, wakiwemo Waziri wa Ulinzi na Kujenga Taifa Hussein Mwinyi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Barnard Membe, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment