Monday, September 12, 2011

Taharuki Zanzibar


Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nungwi ambao wamejitolea kuokopa watu waliopata ajali katika meli ya MV Spice Islanders iliyotokea juzi usiku
MAMIA HAWAJULIKANI WALIPO, KIKWETE AONGOZA KIKAO KUKABILI MAJANGA
Waandishi Wetu, Dar na Zanzibar
MJI wa Zanzibar na viunga vyake, jana uliendelea kuwa katika taharuki na simanzi kubwa kutokana na baadhi ya familia kuwakosa ndugu zao waliokuwa wakisafiri kwa meli ya MV Spices Islander ambayo ilipinduka, kisha kuzama katika eneo la Nungwi kati ya Visiwa vya Unguja na Pemba.
Wakati familia kadhaa zikisubiri majaliwa ya ndugu zao wanaoaminika kwamba walikuwa kwenye meli hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), jana ilitangaza kwamba waliopoteza maisha ni watu 197 na kwamba watu 619 wameokolewa wakiwa hai.


Taarifa hiyo ya SMZ iliyotolewa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed inathibitisha kwamba meli ya MV Spices Islander ilikuwa na zaidi ya abiria 610 ambao ni uwezo wake. Kwa takwimu za waziri huyo, imethibitika kwamba ilikuwa imebeba abiria 816.



Rais Jakaya Kikwete jana aliwatembelea wakazi wa Nungwi kuwapa pole kwa msiba huo mkubwa kwa taifa na kwa mujibu wa Waziri Aboud, mkuu huyo wa nchi alitarajiwa pia kuongoza kikao cha Baraza la Taifa la Ulinzi na Usalama kujadili maafa hayo.


Kadhalika, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal pia aliwatembelea wakazi wa Nungwi na pia kuwapa pole wafiwa na walionusurika katika ajali hiyo mbaya.


Aboud alisema kati ya waliokufa, 158 walitambuliwa na kuzikwa na jamaa zao wakati maiti 39 hawakutambuliwa hivyo kuzikwa na Serikali katika eneo la Kama, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.


Alisema Serikali pia imeandaa makaburi mengine 134 kusubiri maiti ambao wanaendelea kuokolewa kutoka baharini.


Alisema SMZ imewasiliana na wakuu wa Mikoa ya Tanga, Pemba na Mombasa ili wasaidie upatikanaji wa maiti ikiwa wataonekana katika fukwe za maeneo hayo. “Kesho jioni (leo) tutakuwa na swala ya pamoja kwa ajili ya kuwatakia heri ndugu zetu,” alisema Aboud.


Watu wapotea
Jana kulikuwa na mamia ya wakazi wa Zanzibar waliokuwa wakifuatilia kwa karibu kazi ya utafutaji wa maiti katika Kijiji cha Nungwi karibu na eneo ambalo meli hiyo ilizama juzi alfajiri.


Baadhi ya wananchi walilalamika kutowaona ndugu zao ambao wanadai kwamba walikuwa katika meli hiyo iliyokuwa ikitoka Unguja kwenda Pemba.


Mmoja wao ni Seif Mohamed Ally ambaye alisema watoto wawili wa dada yake walikuwa ndani ya boti hiyo lakini tangu ajali hiyo itotee hawajawaona wakiwa hai au vinginevyo.


“Japokuwa naelewa kilichotokea ni mipango ya Mungu lakini nasikitika kusema kuwa ndani ya boti hiyo kulikuwa na watoto wawili wa dada zangu tumefanya jitihada ya kuwatafuta katika kundi la majeruhi na marehemu bila mafanikio,” alisema Ally.


Mkazi mwingine wa Unguja, Salama Ali Said alisema hajafanikiwa kuwaona watoto wake wawili ambao aliwataja kuwa ni Abdallah Hamad Abdallah na Amour Hamadi ambao ni wakazi wa Wawi, Pemba.


Mwingine ni Ally Hussein ambaye alisema familia yake inawatafuta Hashiruna Ally Suleiman ambaye alikuwa safarini pamoja na watoto wawili ambao ni Amina na Raudhati ambao walikuwa wakisafiri kwenda Kinowe – Konde, Pemba.


Mkazi mwingine wa Zanzibar, Saleh Ali alisema familia yake imewapoteza ndugu zao wanane ambao ni Hamad Bakari Hamad, Rahma Zahoro Faki, Salum Saleha Ali, Mkali Hamad Bakari, Abdul Wahid, Suleiman Bakari, Hidaya Issa Suleiman na Juma Hamad ambao bado hawajapatikana... “Sasa tunasubiri kudra za Mwenyezi Mungu... walikuwa wakienda Wingwi, Pemba.”


Mkazi mwingine wa Unguja, Juma Swalehe alisema kwenye meli hiyo walikuwamo watoto wake wanne na hadi jana mchana hakuna aliyekuwa amepatikana.


Wengine ambao hawajapatikana ni wajukuu wawili wa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki ambao ni Sakina Mohamed na Maimuna Mohamed.


Mbali ya hao wengine ambao hawajapatikana ni Fatma Mohamed, Asha Mussa, Maimuna Mussa, Raya Abdallah wakazi wa Mtembwe, Ali Seif Salim na Ali Seif Sunda (Pandani, Penda), Halima Ali Humud (Vikokotoni, Unguja) na Abdulkader Baucha.


Tamko la SMZ
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Serikali itafanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha ajali ya meli hiyo.


Maalim Seif alisema ni dhahiri kuwa idadi ya abiria waliokuwamo ndani ya meli hiyo ni kubwa zaidi ya ile iliyoelezwa jambo ambalo linaweza kuwa sababu ya kuzama kwake na kusababisha maafa hayo makubwa katika historia ya Zanzibar.


Alisema hayo baada ya kushiriki katika maziko ya abiria kadhaa katika Makaburi ya Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi Unguja.Aidha, SMZ ilitoa tamko kwamba itawachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kufanya uzembe uliosababisha kuzama kwa meli hiyo.


Waziri Mohamed Aboud alisema kamati maalumu itaundwa ili kuchunguza ajali hiyo na ikibainika kuwa kulikuwa na uzembe, “sheria itachukua mkondo wake”.


Kuhusu nahodha wa meli hiyo, alisema mpaka sasa hajapatikana na haieleweki iwapo yuko hai au amefariki dunia. Alisema mhandisi wa meli hiyo amenusurika na anahojiwa na vyombo vya usalama.


Hata hivyo, waziri huyo alisema Serikali haifahamu mmiliki wa meli hiyo. “Sisi hatumjui mwenye kumiliki meli hii la ukweli lazima tuliseme, Shirika la Bandari ndilo lenye taarifa zote.”


Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) imesema meli hiyo inamilikiwa na Salimu Said Bacwash kupitia Alhubra Shipping Company Limited.


Waziri Aboud alisema SMZ kwa kushirikia na Serikali ya Muungano inachukua hatua kushughulikia suala hilo pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha majanga hayo hayatokei tena.


“Natoa siri leo kwamba kamati ya kitaifa ya Ulinzi na Usalama inakaa kikao chake, kujadili masuala haya chici ya Mwenyekiti Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete,” alisema Waziri Aboud.


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa mchango wake wa Sh300 milioni kutokana na ajali hiyo. Kadhalika, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umetoa Sh13 milioni, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Sh10 milioni na Kampuni ya Simu ya Tigo imetoa chakula cha msaada chenye thamani ya Sh5 milioni kwa ajili ya kusaidia familia zilizoguswa na maafa hayo.


Hofu Tanga
Mji wa Tanga umezizima tangu kutolewa kwa habari za kuzama kwa meli hiyo huku wakazi wenye asili ya Visiwa vya Pemba wakihaha kutafuta ya kwenda kuwatambua jamaa zao.


Baadhi yao wamekuwa wakifanya mikutano usiku na mchana kutafakari hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuchangishana nauli.


“Hapa tupo kwa ajili ya kuchangishana fedha ili tuweze kumuwezesha Adam Amin ambaye mdogo wake aitwaye Safia Amini alikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya meli hiyo alikuwa anakwenda shule baada ya kumaliza likizo” alisema mmoja wa wakazi hao, Rashidi Ali.


Pia kumekuwa na ongezeko kubwa la magari kutoka Mombasa, Kenya ambayo yamekuwa yakiwafikisha Tanga abiria kwa ajili ya kusafiri kwenda Zanzibar kupitia Dar es salaam.


Wingi wa abiria wanaokwenda Zanzibar kupitia Dar es Salaam umesababisha msongamano wa abiria kutokana na ufinyu wa nafasi katika mabasi yanayosafiri kati ya Tanga na Dar es Salaam.


Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa ameitaka Serikali kuwachukulia hatua kali wahusika huku akiilaumu kwamba imeshindwa kujifunza kutokana na ajali mbaya ambazo zimekuwa zikitokea nchini.


"Ajali hii imetusikitisha. Kifo ni jambo la kusikitisha sana, nasikitika kuona Serikali imeshindwa kujifunza kutokana na ajali mbaya ambazo zimekuwa zikitokea na kupoteza mamia ya Watanzania wasiokuwa na hatia," alisema.


Dk Slaa alisema Serikali imeshindwa kujifunza kutokana na ajali mbaya ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba mwaka 1996 na kuua watu wengi."Naomba kutumia fursa hii kuiambia Serikali kwamba iwasake wahusika wote walioruhusu meli hii kuendelea na safari, taarifa zinasema ilizimika mara nane na hakuna msaada wowote uliotolewa.”


Habari hii imeandikwa na Talib Ussi, Zanzibar; Burhani Yakub na Salim Mohamed, Tanga; Boniface Meena, Igunga na Furaha Maugo Dar


Mwananchi

No comments: