Saturday, September 3, 2011

BREAKING NEWS..........NYUMBA 19 ZACHOMWA MOTO SUMBAWANGA MTU MMOJA AUWAWA

: IGP.Mwema
Na Francis Godwin
Nyumba 19 zimechomwa moto na mtu mmoja ameuwawa kwa kuchomwa moto kufuatia

tafrani kubwa kulipuka kwenye kijiji cha Ulumi tarafa ya Mwimbi wilayani

Sumbawanga mkoani Rukwa wakati kundi la wananchi likiwatuhumu baadhi ya wazee wa kijiji hicho kuhusiana na masuala ya kishirikina.

Mwandishi wa mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com kutoka mkoani Rukwa Elizabeth Ntambala anaripoti kuwa tukio hilo limetokea juzi kufuatia mwanamke mmoja Rista Nachula kufariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi ugonjwa wa kuvimba miguu na kuwa na dalili za kuchanganyikiwa akili, hali iliyopokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho hususan kundi la vijana walioamini kuwa amerogwa hivyo kuanzisha operesheni ya kuwasaka baadhiyawazeewaliowatuhumu kuwa ni wachawi.

Akizungumza kwa njia ya simu Tanzania Daima,Afisa Tarafa wa tarafa ya Mwimbi Bw.Godfrey Maufi alisema kuwa vurugu hizo zilisababisha kusimama kwa shughuli zote katika kijiji hicho na vijiji jirani huku baadhi ya wananchi wakikimbia nyumba zao kwa kuhofia kuchomwa moto ambapo Mzee Credo Msangawale (65) aliuwawa.

Maufi alisema hali ilikuwa mbaya mara baada ya mazishi ya marehemu Rista , ambako kundi la vijana walionekana kusikitishwa na kifo cha mwanamke huyo na kuanza kutoa maneno ya vitisho kwa baadhi ya wazee wa kijiji hicho ambao waliwashtumu kuwa ni washirikina, huku baahi ya wazee wakitoroka kijiji hicho.

Afisa Mtendaji wa kata ya Ulumi Florence Ntola alisema kuwa siku moja kabla ya mazishi ya mwanamke huyo usiku huo tayari kundi la wananchi walichoma nyumba tatu za baadhi ya wazee kijijini hapo na kuendeleza zoezi hilo siku iliyofuata , ambapo pia walimkamata Mzee Msangawale na kumpiga kisha kumchoma moto.

Tayari Mzee Msangawale alikuwa ameshatoroka kijiji hapo lakini anadiwa alirejea baada ya mtuhumiwa wa kifo cha mwanamke huyo kutoroka kijiji hapo, huku akijiamimni kuwa asingeweza kudhurika na kundi hli la vijana ambapo lilishatangaza vita dhidi ya wazee walitajwa kuwa ni washirikina.

“Baada ya kumkamata Mzee Msangawale walimbeba juu juu hadi nyumbani kwake ambako walimwambia aende akaone jinsi nyumba yake inavyofanywa na yeye mwenyewe ambapo walianza kuvunja nyumba yake na kumkamata yeye mwenye kisha kumrushia kwenye
moto” alisema Ntola.

Akiwa na gaagaa kwenye moto mjukuu wake alitokea na kumwokoa mzee huyo lakini kundi la wananchi hao walimdaka na kumrudisha tena kwenye moto ambapo walichukua gunia la maharage na kumkandamiza juu yake kisha kuwasha moto, hivyo kuungua vibaya hadi kufariki dunia.

Alisema baada ya kumwua mzee huyo kundi hilo likiwa na silaha mbalimbali za jadi kama vile mapanga , shoka ,visu, marungu walianza msako wa nyumba kwa nyumba za wazee wote waliowatuhumum kwa uchawi na kuanza kuzichoma nyumba zao moto huku wakiwatishia pia viongozi wa kijiji hicho kuwa hawataki wasikie sauti zao za kukemea vitendo hivyo na kudai kuwa iwapo watathubutu basi nao wataingizwa kwenye kundi hilo la watuhumiwa wa uchawi.

“Hali ilikuwa ni mbaya kijiji chote kilijaa moshi angani kana kwamba kuna vita na kundi la wananchi walijitokeza huku wakipiga madebe na filimbi na wengine wakibeba silaha na wengine walikuwa wakiimba nyimbo wakisema kuwa mwisho wa wachawi umefika na wamechoka na vitendo vya kishirikina” alisema Ntola.

Afisa Mtendaji huyo wa kata alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo ya kutishiwa aisha yao ilibidi viongozi hao wakae kando kwani awali walimkamata kijana mmoja ambaye wananchi waliwalazimisha kumwachia baada ya kuwatishia kubomoa ofisi ya Mtendaji wa kata na kuchoma nyumba zao moto hali iliyowalizimu kuwaarifu polisi wilaya juu ya matukio hayo ambapo polisi walifika majira ya usiku na kufanikiwa utuliza ghasia hizo.

Kufuatia vurugu hizo jumla ya watu saba wanashikiliwa na jeshi la polisi

kuhusiana na tukio hilo ambao aliwataja kuwa ni Ladslaus Motafali,Michael Mlipe, Gerade Kalyamo, Regnard Chupa, Damas Ntelanya, Gilberth Kazembe na Sosten Ngete.

Aidha alisema kuwa kuna kundi kubwa la vijana na baadhi ya wazee wametoroka kuelekea nchi jirani ya Zambia na vijiji vya mbali na eneo huku wengine wakihofia kukamatwa kuhusiana na vurugu hizo na wengine wakihofia kuuwawa na kundi la vijana wa kijiji hicho.

Kamanda wa polisi mkoani Rukwa Isuto Mantage alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kuongeza kuwa alimtuma Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Sumbawanga Mohamed Mbonde na kikosi chake kwenda kutuliza ghasia huku akithibitisha kuwa hali ya kijiji hicho hadi hivi sasa shwari.

No comments: