Tuesday, September 27, 2011

Taarifa zaidi ya Ajali ya Roli iliyyo tokea mkoani Mbeya


Na Esther Macha, Mbeya
MAJERUHI  30 waliopata  ajali  ya Lori waliolazwa katika hospitali teule ya wilaya ya Mbeya Ifisi kati ya 38 waliofikishwa hospitalini hapo juzi baada ya ajali mbaya iliyoua watu 14 wakitokea Mnadani Mbuyuni wilaya ya Chunya mkoani hapa wanaendelea vizuri.
Wakizungumza na mtandao huu jana hospitalini hapo baadhi ya majeruhi hao walisema hali zao kiafya zimeendelea kuimarika baada ya juhudi kubwa za waganga na wauguzi wa hospitali hiyo kuendelea kuwapa matibabu kwa ukaribu kwa kila mmoja wao.

Akizungumza na mtandao huu  Mmoja wa majeruhi wa  hao Bw.Simon Mwaipopo ambaye amelazwa katika hospitali hiyo, alisema anamshukuru Mungu kwa kunusurika katika ajali hiyo ambapo alitanabaisha kuwa hata waliopona ni kwa uweza wa Mungu pekee.

''Mimi binafsi namshukuru Mungu nimepona na hapa hospitalini tunaendelea kupewa huduma kwa karibu sana na wauguzi pamoja na madaktari jambo ambalo tunaamini baadhi yetu tutapona haraka na kuruhusiwa kurudi nyumbani'' alisema .

Majeruhi mwingine Bi.Hilda Jomba ambaye alivunjika mkono wake wa kushoto alisema anaamini atapona baada ya kuendelea kuhudumiwa kwa karibu na wauguzi wa hospitali hiyo bila kumnyanyapaa.

Alisema kuwa wauguzi wanaendelea kuwahudumia vizuri na  kwamba katika ajali hiyo anachokumbuka  ni kuwa  ilikuwa majira ya saa 12 kuelekea kwenye saa moja hivi ndipo  walipopinduka na gari  walilokuwa wamepanda "alisema .

Kwa upande wake Muuguzi mkuu wa Hospitali hiyo Bi. Rhoda Kasongwa alisema alipokea majeruhi 39 na maiti watatu ambapo maiti wote watatu walitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao.
Alisema kwa upande wa majeruhi, watatu walipelekwa hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa matibabu zaidi na watatu waliruhusiwa kurejea nyumbani baada ya hali za Afya zao kuimarika.

Muuguzi huyo aliwataja maiti waliofikishwa katika hospitali hiyo na kuchukuliwa na ndugu zao kuwa ni pamoja na Emelia Mwangove (40), Glasiano Kalinga Nyambizi (37) na Msafiri Tinda (35).

Ajali hiyo ilitokea eneo la Msangamwelu kwa kulihusisha lori aina ya Fuso lenye namba za usajili T 532 AJF na kuthibitishwa na Jeshi la Polisi kupitia kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya Bw. Anacletus Malindisa.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa polisi Mkoani MBeya Bw.Anacletus Malindisa. alisema kuwa hali za majeruhi waliobaki hospitalini hapo zinaendelea vizuri na ndugu wengine bado wanaendelea kutambua miili  ya ndugu zao.

No comments: