Tuesday, September 13, 2011

Tanzania yapokea msaada wa Mbolea yenye thamani ya Shilingi Bilioni 7 kutoka serikali ya Japan

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe akiwa ameshika mfuko wa mbolea aina ya DAP ambao ni sehemu ya msaada kutoka Serikali ya Japan kulia ni Balozi wa Japan Bwana Hiroshi Nakagawa, Makao Makuu ya Wizara, Temeke, Jijini, Dar es Salaam.

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe leo amepokea msaada wa mbolea aina ya DAP kutoka Serikali ya Japan kiasi cha tani 5,953 chini ya utekelezaji wa msaada kutoka nchi hiyo unaofahamika kama KR 2 wa mwaka 2010/2011.

Mbolea hiyo iliyotolewa na Serikali ya Japan imegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 7.3 sawa na Yeni Milioni 400 za Japan.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mbolea hiyo hapo Wizarani, Waziri Maghembe alisema kuwa sekta ya kilimo nchini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa upatikanaji wa mbolea.

Waziri Maghembe alisema licha ya changamoto hizo Serikali ya Tanzania imejizatiti katika kukabiliana na changamoto hizo ili Taifa liwe na uhakika wa chakula kwa kuongeza uzalishaji katika mazao ya chakula na biashara ili kupambana na umaskini wa kipato.

Akiongea wakati wa makabidhiano ya mbolea hiyo, Balozi wa Japan nchini Bwana Hiroshi Nakagawa alieleza kuwa, Serikali ya Japan kupitia mpango wa KR 2 imedhamiria kuwasaidia wakulima wa Tanzania ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula.

Waziri Maghembe aliishukuru Serikali ya Japan kwa mchango wao katika utekelezaji wa Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) na kuongeza kuwa mbolea hiyo itauzwa kwa bei nafuu ili kuiwezesha Serikali kupata fedha na kuahidi kuwa mbolea hiyo itasambazwa mapema ili iwafikie wakulima kwa wakati kupitia mpango wa Serikali wa kusambaza pembejeo za kilimo kwa mfumo wa vocha.

Waziri Maghembe alitumia fursa hiyo kumuaga Balozi huyo wa Japan Bwana Hiroshi Nakagawa ambaye atamaliza muda wake wa utumishi kama Barozi wa nchini ifikapo Septemba 30 mwaka huu. Waziri Maghemeb alimwakikishia kuwa Tanzania itatumia vyema misaada, utaalam na wataalam wake katika sekta ya kilimo na umwagiliaji ambao nchi hiyo imekuwa ikiisaidia Tanzania.

No comments: