Saturday, September 17, 2011

Waliozembea kuzama Mv Spice waanza kushughulikiwa


Na Nafisa Madai
IKIWA ni wiki moja baada ya kuzama kwa Mv. Spice Islander, tayari hatua za kuwajibishana zimeanza kuchukua nafasi yake.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa jeshi la polisi linamshikilia ofisa usalama wa Mamlaka ya vyombo vya bahari Silima Nyange Silima akidaiwa kuzembea katika kusimamia majukumu yake.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo umebainisha kuwa ofisa huyo ambaye usiku wa Septemba 9 mwaka huu, ndiye aliyekuwa dhamana wa kuzifanyia ukaguzi na kudhibiti idadi ya abiria wanaosafiri kwa meli zinazoelekea Pemba usiku wa siku hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vyombo vya Bahari Haji Vuai Ussi, alithibitisha ofisa huyo kushikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi.
Alisema kwa mujibu sheria za Mamlaka hiyo, ofisa huyo jukumu lake kubwa lilikuwa kudhibiti idadi ya abiria wanaopanda katika vyombo vinavyotoka nje ya bandari ya Zanzibar.
Alisema Nyange ambaye alikuwa zamu siku hiyo alitakiwa kuhakikisha idadi ya abiria wanaopanda katika meli ya Mv. Spice Islander wanakuwa idadi sawa na kwa mujibu wa uwezo wa meli hiyo.
Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa ofisa huyo alitakiwa kupiga ripoti kwa ofisa mkuu wa usalama wa Mamlaka, endapo angebaini kuwa meli hiyo ina idadi kubwa ya abiria na mizigo.
Alisema mbali ya hatua hiyo kama kungekuwa na ugumu wa kuwasiliana na ofisa mkuu alipaswa kuwasiliana na kitengo cha polisi bandarini ambacho ndicho chenye uwezo wa kuizuia meli hiyo isiondoke.
“Haya yote hakuyafanya, hakuna ripoti yeyote, hii inamaanisha hakuwajibika, aliruhusu meli iondoke bila ikiwa imejaza sana”, alisema Mkurugenzi huyo.


Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa alisema ni kweli kijana huyo anashikiliwa na wenziwe watatu na walitajiwa kufishwa mahakamani jana.


Mbali ya Simai Nyange wengine waliokuwa wakishikiliwa ni Yussuf Suleiman Issa kutoka katika kundi la wamiliki ambapo kwa siku hiyo alikuwa na dhamana ya kuhakikisha abiria na mizigo inakuwa salama.


Aidha mwengine ni Abdalla Mohammed Ali ambaye ni ofisa mkuu katika meli hiyo na kueleza kuwa jitihada za mtu wanne ambaye ni nahodha wa meli hiyo kumkamata zinaendelea.

“Baada ya kuwahoji, majibu yao tumebaini kuwa wamezembea na kwa hatua za mwanzo wanapaswa kwenda mahakamani”, alisema Kamishna Mussa.

No comments: