Wednesday, September 7, 2011

WATOTO 400 WAPOTEA ZANZIBAR SIKU YA IDI MWAKA HUU

Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi- Zanzibar

ZANZIBAR JUMATANO, SEPTEMBA 7, 2011. Zaidi ya watoto 400 wenye umri kati ya miaka mitano na 17, walipotea mjini Zanzibar katika kipindi cha siku nne za maadhmisho ya Siku Kuu ya Iddi El Fitri ya kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Taarifa ya Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, imesema kuwa karibu watoto wote waliokuwa wamepotezana na ndugu na jamaa zao wakati wa sherehe hizo, walifikishwa katika vituo mbalimbali vya Polisi mjini Zanzibar na kufanyiwa utaratibu wa kurejeshwa makwao.

Akizungumzia matukio yaliyojitokeza katika kipindi hicho, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa ongezeko la upotevu wa watoto hao ilikuwa kubwa mno ikilinganishwa na siku kuu nyingine kama hizo katika miaka iliyopita.

Kamanda Azi amesema kuwa Polisi walilazimika kumhoji kila mtoto ili kujua anakoishi na pale ilipowawia vigumu watoto hao kujitambua pia walihojiwa ili kutaja shule ama madrasa wanazosoma jambo ambalo lilirahisisha kila mtoto kurejeshwa makwao.

Amesema watoto wengi hawakufahamu maeneo waliotoka kwa majina lakini walizitaja shule na madrasa wanazosoma jambo ambalo alisema lilirahisisha katika kuwafikisha watoto hao makwao kwa urahisi.

Amesema wakati wa siku kuu hiyo Polisi pia walifanikiwa kukamata kiasi kikubwa cha mihadarati na pombe ya moshi maarufa kama Pombe ya Tende na kuharibu mapipa 12 yaliyokuwa yakitumika kupikia pombe hiyo.

Kamanda Aziz amesema pia kuwa Polisi waliyakamata magari 148 yakiwemo ya abiria na mizigo kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo ya kutozingatia matumizi salama ya barabara na madereva wake na wamiliki wa vyombo hivyo wameanza kufikishwa mahakamani.

Siku Kuu ya Iddi El-Fitri, ndiyo Siku Kuu kubwa kuliko zote katika Visiwa vya Unguja na Pemba na husherehekewa kwa muda wa siku nne au zaidi ikilinganishwa na siku kuu nyingine visiwani humo ambapo watoto na watu wazima huonekana mitaani na katika maeneo mbalimbali ya burudani katika viwanja vya wazi wakiwa na mavazi mapya na ya heshma.

No comments: