Tuesday, September 6, 2011

Yahusu Kushambuliwa Kwa Mawe Gari la Katibu Mkuu Wizara wa Fedha, Uchumi na Maendeleo ya Mipango wa Zanzibar

Gari la Katibu Mkuu Wizara wa Fedha, Uchumi na Maendeleo ya Mipango wa Zanzibar limeshambuliwa kwa mawe na Ali Salim Ali(49) Mkazi wa Fuoni Mjini Unguja ambaye anaidai Serikali ya Mapinduzi Zanzibar baada ya kufanya kazi ya ujenzi wa jengo katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi wa Wizara hiyo, Ramadhan Senga amesema mtu huyu awali, alikwenda Ofisi ya Katibu Mkuu Khamis Mussa kutaka kumuona,lakini hakuwepo Ofisini,lakini wanadhani alikuwa na dhamira ya kutaka kumfanyia jambo baya.
Senga amesema baada ya kumkosa Katibu Mkuu, alianza kulishambulia kwa mawe gari analotumia Katibu Mkuu Khamis Mussa lenye namba za usajili SMZ 6460 aina ya Toyota Prado mali ya Wizara ya Fedha,Uchumi na Maendeleo ya mipango Zanzibar.
Mkurugenzi huyo amesema gari hilo lilishambuliwa sehemu za vioo kabla ya mtuhumiwa kukamatwa na Polisi.


Akizungumzia kadhia hiyo, Mkurugenzi Senga amesema Wizara yake sio muhusika mkuu wa madai ya mtuhumiwa huyo ambapo Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ndio wanaohusika na madai ya mtuhumiwa ambaye alifanya kazi ya ujenzi katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema kazi aliyofanya ni kujenga jengo la Serikali katika Wilaya ya Micheweni karibu miaka mitatu iliyopita ambapo hakuweza kulipwa fedha zake kwa wakati na ndipo alipofungua kesi Mahakamani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kamishna Msaidizi, Aziz Juma Mohammed amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema upelelezi wa tukio hilo unaendelea na ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani.


No comments: