Monday, October 17, 2011

KUMI NA MOJA MBARONI MKOANI SINGIDA.




Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida Celina Kaluba akitoa taarifa ya kutiwa mbaroni kwa wachimbaji wadogo wa madini wa kijiji cha Sambaru jimbo la Singida mashariki kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha). (Picha na Nathaniel Limu).


Na.Nathaniel Limu


Jeshi la Polisi mkoani Singida linawashikilia watu 11 kwa tuhuma ya kuingia katika eneo la mgodi wa dhahabu mali ya kampuni ya Shanta Mining uliopo katika kijiji cha Sambaru wilayani Singida bila kuwa na kibali halali cha kuingia humo.


Kamanda wa polisi mkoani Singida Celina Kaluba amesema watuhumiwa hao wamekamatwa Oktoba 9 mwaka huu.


Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Gulas Mahiga(29) mkazi wa Bariadi, Mohamed Saidi (34) mkazi wa Mang’onyi, Maduhu Luhende (39) mkazi wa Bariadi, Steven Wambura (32) mkazi wa Bunda na Boniface Mbola (27) mkazi wa Misughaa.


Kaluba amewataja wengine kuwa ni Emannuel Lugumbika (31) mkazi wa Bariadi, Mwita Mtatiro (31) mkazi wa Musoma, Joseph Mtuti (27), Makenga Mduhu( 27) Emannuel Sawa (53) wote wawili ni wakazi wa Mwanza na Dotto Petero (28) mkazi wa Misigiri.


Akifafanua amesema Oktoba 8 mwaka huu walipata taarifa kwamba kuna kundi la watu limevamia eneo la mgodi wa dhahabu mali ya Kampuni ya Shanta Mining.


Amesema Polisi walipofika eneo hilo , waliwakuta wananchi hao wakiendelea kuchimba dhahabu na walipowataka waache kuchimba katika eneo hilo ambalo sio lao, wananchi hao walianza kufanya vurugu na kuanza kurusha mawe.


“Kitendo cha wananchi hao kurusha mawe, kilisababisha askari D.9800 Sajenti Ally kujeruhiwa mkono wa kushoto. Vurugu hizo zilidhibitiwa na polisi lakini mara kwa mara zilionekana kujirudia kutokana na wananchi hao kutokubali kuondoka katika eneo hilo ”amesema.


Kaluba amesema Oktoba 9 mwaka huu saa mbili asubuhi, kundi hilo la watu lilirudi tena katika mgodi wa Shanta Mining huku likihamasishana kwa kupiga kelele na kuanza kuwatupia mawe askari polisi.


“Kulikuwa hakuna namna nyingine isipokuwa polisi kuwarushia bomu la machozi na kufyetua risasi za moto hewani ili kuwatanya. Baada ya hapo, ndipo watuhumiwa 11 waliweza kukamatwa”,amesema Kaluba.


Kamanda Kaluba amesema baada ya upelelezi kukamilika, watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayowakabili.

No comments: