Friday, October 7, 2011

Mapambano Makali Polisi, Raia Mgodini.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema.

MTU MMOJA ASADIKIWA KUFA KWA KUPIGWA RISASI YA USO NA POLISI.

POLISI wilayani Geita, mkoani Mwanza wamelazimika kutumia risasi za moto kupambana na wananchi zaidi ya 200 ambao ni wachimbaji wadogo wa madini ambao wanadaiwa kuvamia machimbo ya madini katika Kijiji cha Nyaruyeye, Kata ya Nyarugusu, ambayo yalifungwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo hali iliyofanya shughuli za kiuchumi na kijamii kusimama kwa muda.

Katika vurugu hizo, mtu mmoja aliyefahamika kama Jahaja Chandarua (27) alikufa baada ya kupigwa risasi na polisi sehemu ya paji la uso ambayo ilimpasua na kutokea upande wa pili, huku Mkuu wa Kituo cha Polisi Nyarugusu (OCS), Ibrahim akijeruhiwa kwa kupigwa na mawe sehemu ya mkono wake wa kulia na wananchi hao.

Vurugu hizo ambazo zilianza juzi saa 2:00 usiku ziliendelea hadi jana jioni na kufanya shughuli za kijamii na kiuchumi katika kata hiyo na vijiji jirani na machimbo hayo, kusimama kwa muda huku polisi wakiendelea kutumia nguvu kudhibiti wananchi hao.

Hiyo ni mara pili kwa wananchi hao kukosa uvumilivu na kuamua kuvamia machimbo hayo, kwani wiki moja iliyopita wananchi wengine zaidi ya 3,000 walivamia machimbo hayo kupinga kupewa mwekezaji huku wao wakishindwa kunufaika na rasilimali hizo za taifa.


Chanzo cha wananchi kuvamia
Tangu Serikali ilipofunga machimbo hayo, wananchi ambao walikuwa wakiyategemea kufanya shughuli zao za kiuchumi, wamekuwa wakiahidiwa kila mara kwamba, yangefunguliwa baada ya muda fulani, lakini imeshindwa kufanya hivyo.


Kutokana na danadana hizo, ndipo juzi usiku wananchi hao walipoamua kukusanyika na kuandamana hadi kwenye machimbo hayo ya Nyaruyeye na kuanza kupambana na polisi wanaolinda eneo hilo.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu, Thobias Ikangala alisema wachimbaji hao baada ya kufika eneo hilo walivunja uzio uliowekwa na mwekezaji kabla ya kutawanywa na polisi wanaolinda machimbo hayo na ndipo mapambano yalipoanza kati yao na polisi.

Uamuzi wa DC
Septemba 20 mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Philemon Shelutete aliyafunga machimbo hayo na kuwataka wachimbaji hao kuwa na subira wakati taratibu za kisheria zikifanyika.

Shelutete alisema hatua hiyo inalenga kutoa fursa kwa mmilki wa eneo hilo, Kampuni ya Mawemeru kukamilisha taratibu za kuingia ubia na Mdau Baraka na baada ya kukamilika kwa taratibu hizo, uchimbaji kwa kuzingatia sheria za madini ungeanza ikiwamo kuzingatia hali ya usalama na afya katika eneo hilo.
Katika vurugu hizo, inaelezwa pia watu ambao tayari walifukuzwa kutoka machimbo hayo wakishirikiana na baadhi ya wanakijiji hicho cha Nyaruyeye walivamia mkutano wa ndani wa viongozi wa Serikali ya Kijiji na kisha kumjeruhi mjumbe mmoja.

Taarifa zinasema kwamba, katika vurugu hizo wananchi hao walimvua shati Mwenyekiti wa Kijiji na Ofisa Mtendaji wake, kabla ya viongozi hao kuokolewa na polisi.Vurugu hizo pia zimetokea siku chache baada ya ofisa madini Wilaya ya Geita, Abdalah Sementa kutoa onyo kali dhidi ya wachimbaji hao kuacha chuki na kujenga makundi ya kuvuruga amani katika eneo hilo.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Rebaratus Barrow alipopigiwa simu kuzungumzia tukio hilo simu yake ilipokelewa na mtu mwingine aliyesema: kuwa, '' Mkuu yupo nje jaribu kupiga baadaye''.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita (OCD), Paul Kasabago alipotafutwa kwa simu, simu yake iliita bila kupokewa zaidi ya mara tatu.

Kufuatia kuwapo kwa vurugu hizo, hadi jana baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii zilikuwa zimesimama ikiwa ni pamoja wanafunzi kujifungia madarasani, huku walimu nao wakijifungia ofisini kuhofia usalama wa maisha yao. Wanafunzi walizuiwa na walimu wao kutoka nje ya madarasa kutokana na mapambano yaliyokuwapo ambayo yalitawaliwa na milio wa risasi na mabomu ya kutoa machozi.

Mapambano hayo kati ya polisi na raia katika migodi ya madini, si mara ya kwanza kuikumba nchi kwani tayari matukio kama hayo yanayosababisha mauaji yamekwishatokea wilayani Tarime eneo la Nyamongo ambako kuna mgodi mkubwa unaomilikiuwa na Kampuni ya Barrick.

No comments: