Tuesday, October 18, 2011

Mtoto Sesilia Arudi Tanzania Bila Matumaini ya Kuwa Mwalimu


Mtoto Sesilia Edward,alipowasiliwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa New Delhi Nchini india
Mtoto Sesilia Edward,akiwa hospitali ya Fortis iliyopo New Delhi, tarehe 27 septemba mwaka huu


Mtoto Sesilia Edward akiwa wodini nchini india


Mtoto Mwenye ugonjwa unaofanana na Mtoto Sesilia ambae alilazwa wodi moja nae nchini india

----
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



Tarehe 18 Oktoba 2011



Mtoto Sesilia Edward, mwenye umri wa miaka 14 ambaye alisafirishwa kwenda nchini India, katika hospitali ya Fortis iliyopo New Delhi, tarehe 27 septemba mwaka huu, kwa ajili ya matibabu ya moyo, amewasili salama nchini.



Baada ya kupokelewa alipofika nchini India, Sesilia alianza kufanyiwa uchunguzi wa kina na kujulikana kuwa chemba ya juu ya kulia ya moyo wake, imekuwa kubwa kupita kawaida, huku chemba ya chini ya kulia ikiwa ni ndogo kupita inavyotakiwa kuwa, jambo lililopelekea uvujaji katika valvu iitwayo Tricuspid pamoja na kuonekana kwa kimiminika (maji maji) katika tumbo pamoja na mapafu.



Tatizo kama hili lililomkumba Sesilia, liitwalo kwa jina la kitaalamu kama Endomyocardical Fibrosis, hutokea mara chache. Taarifa za madaktari nchini India, zinaeleza kuwa hatua ya kiafya aliyofikia Sesilia katika tatizo hili ni mbaya, hivyo imepelekea kushindwa kutibika kwa ugonjwa huu hivyo atahitaji uangalizi mkubwa kwa kutumia dawa na sio kwa upasuaji wowote ule wa moyo.



Kwa dawa ambazo Sesilia ameanza kutumia mpaka sasa, ameweza kupungua kwa kilogramu tano, anajisikia nafuu zaidi, na afya yake inaimarika. Ugonjwa kama wa Sesilia umesharipotiwa kutokea kwa watoto katika maeneo ya Zanzibar, Pemba, kisarawe Tanzania na Kerala- kusini mwa India. Dokta Srah Matemu kutoka Hospitali ya Regency amesema kuwa watoto zaidi ya asilimia 20% wanaofanyiwa upasuaji katika hali kama ya Sesilia huwa hawaponi na hivyo madaktari wa hopitali ya Fortis waliamua kutomfanyia operesheni hiyo.



Aidha, tatizo hili limehusishwa na ulaji uliopitiliza wa mihogo yenye sumu iitwayo Cyanide inayopelekea kuvuja na mishipa kusikotakiwa na kudhoofu katika mishipa ya moyo. Katika miaka mitano iliyopita,Sesilia alikuwa akitumia mlo wa muhogo mara tatu kwa siku, amekiri katika kipindi hicho chote, ni mara chache sana amekuwa akila vyakula vingine kama uji,ugali,au wali . (Sesilia ni mzaliwa wa Kisarawe na amesihi kijijini hapo kwa miaka takribani 13).



Sesilia ataendelea na matibabu na uangalizi zaidi katika hospitali aliyokuwa akitibiwa awali, hospitali ya taifa Muhimbili, huku hospitali ya Regency ikijitolea kumsaidia matibabu ya kupunguza maji na dawa mbalimbali kwa garama nafuu..



Ili kuepuka kutokea kwa tatizo kama hili kwa watoto wengine, Wazazi wanashauriwa kuwa waangalifu katika kupanga milo ya watoto.Uzidishaji wa chakula cha aina moja unaweza kuleta madhara kwa afya ya mtoto kama madhara ya mihogo. Pia kipindi wanapoona watoto wao hawako sawa kiafya, wawahi hospitali kwa ajili ya matibabu ili kuepuka kukomaa kwa tatizo kunakoweza kupelekea ugonjwa kutotibika. (Dr. Sarah Matemu)



Kipindi cha Mimi na Tanzania, kinatanguliza shukrani zake za dhati kwa timu nzima ya Africa Media Group, iliyoshiriki kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha zoezi la uhamasishaji wa uchangiaji wa pesa kwa ajili ya safari na matibabu ya Sesilia ambayo yamefanyika nchini India.



Pia shukrani ziifikie hospitali ya Fortis Escorts Heart Institute, ambao ilijitolea kwa kupunguza bei ya matibabu ya Sesilia, bila ya kuisahau hospitali ya Regency Dar es Salaam, chini ya uongozi wa Dk. Kanabar kwa kumuandaa Sesilia kimatibabu kwa mda wa wiki moja kabla ya kumsafirisha India kwa ikiwa ni pamoja na daktari kutoka nchini aliyewasindikiza, aitwaye Dk. Ali Amour kutoka hospitali ya Mnazi mmoja.



Shukrani pia zinatangulizwa kwa uongozi mzima wa Lions Club, kwa kufanikisha kwa kuandaa mipango ya matibabu yote ya Sesilia na hospitali, nchini India ambayo yalifanyika kwa bei ya chini kuliko ambavyo hata raia wa India angeweza kutibiwa.



Zaidi ya yote, Mimi na Tanzania inapenda kuwashukuru kwa hali na mali watanzania wote walioguswa na mtoto Sesilia, na kujitokeza kwa kumsaidia kifedha, mavazi na hata kwa sala ikiwa ni pamoja na mahitaji mengine yoyote binti huyu aliyokuwa akihitaji.Moyo wa upendo na huruma mlioonyesha kwa mtoto huyu ni zawadi isiyosahaulika katika maisha yake na wanaomzunguka. Tusiache kuwasaidia na kubadilisha maisha ya ndugu zetu wahitaji kama hawa. Shukrani!



Usiache kutizam kipindi cam Mimi na Tanzania Jumapili tarehe 22 Oktoba, saa 1:30 jioni – Chanel Ten, kumsikia Dokta Sarah akielezea nini Hatima ya Mtoto Sesilia.



Vyomba vya Habari Tanzania, tumejaribu, tumeweza na yaliyotokea kwa mtoto Sesilia ni kazi ya Mungu. Fedha zilizobaki zitahifadhiwa katika account ya Mlezi wake chini ya uangalizi ili kumsaidi motto Sesilia kupata matumizi muhimu kama Dawa, kitanda kizuri kumsaidia Mgongo, Kiti maalum cha kukalia na chakula chake ambachohutayarishwa tofauti na vyakula tunavyokula.



Hoyce Temu
Mtayarishaji an Mtangzaji
Mimi na Tanzania







No comments: