Nape Nnauye
Frederick Katulanda, Mwanza
MKUTANO wa hadhara wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Magoneni, Kirumba jijini hapa, uliingia dosari baada ya kundi la vijana kuwazomea viongozi karibu wote wa chama hicho waliopanda jukwaani na kukifanya kikundi cha ulinzi cha CCM, Green Guard kutembeza kipigo hadharani.Katika mkutano huo, Nape alikuwa amefuatana na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, Katibu wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Nzega Dk Hamis Kigwangalla.
Baada ya kuanza saa 9: 55, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Shaibu Akwilombe ambaye pia ni Katibu wa Wilaya ya Ilemela alipanda jukwaani kuwatambulisha makada wa chama hicho waliokuwa katika msafara wa Nape kisha kumkaribisha Dk Kigwangalla kuzungumza.
Akizungumza katika eneo hilo ambalo ni moja ya ngome maarufu za Chadema, Dk Kigwangalla alisema katika zama za sasa hakuna chama kinachoweza kuwafikisha wananchi katika uchumi mwema zaidi ya CCM. Kauli hiyo ilionekana kuwakera baadhi ya wananchi hasa vijana walikuwapo katika mkutano huo ambao walianza kuzomea huku wengine wakiguna.
Kuona hivyo, Dk Kigwangalla alikatisha hotuba yake akisema yeye siyo msemaji wa mkutano huo. Akwilombe alirejea jukwaani, safari hii akionekana kujawa na hasira na kusema hatakubali kuona watu wakileta vurugu na kusema wanaofanya hivyo wanapima kina cha maji kwa kuweka mguu.
“Hata bila ya polisi hatuwezi kukubali fujo zitokee katika mkutano wetu… na sasa namkaribisha Lusinde kuwasha moto na wanaotaka kupima kina cha maji kwa mguu waone..,” alisema Akwilombe.
Lusinde aliposimama alisema kelele za kuzomea amezizoea na amejifunzia Tarime ambako alikuwa Katibu wa CCM hivyo hazimpi shinda.
“Hawa wanajifunza kutoka Tarime, wanaiga mambo ya utoto, huu mkutano siyo wako ni mkutano wa CCM wewe unakuwasha nini? Kama unaona huwezi kuvumilia mwana CCM usiende kwenye mkutano wa Chadema na kama mwana Chadema huwezi kuvumilia mkutano wa CCM usiende! Wanachofanya ni kwamba uvumilivu kwa vijana wa CCM unafika mwisho,” alisema.
Kauli hiyo ilikuwa kama kutia petroli kwenye nyasi zinazowaka kwani ilizidisha vurugu huku zomeazomea ikiongezeka baada ya hali hiyo kuendelea, Lusinde alisema: “Hii ni nchi yetu wote kilichotokea hapa (Kata ya Kirumba kuongozwa na upinzani), wanakijua, lakini lazima wajue hakuna watu wenye haki ya kuzunguka nchi nzima na wengine wakakosa.”
Ilipofika zamu ya Nchemba ambaye alikuwa Mratibu wa uchaguzi mdogo wa CCM, Igunga alisema Chadema kimeshindwa Igunga kihalali na kwamba anashangaa kusikia kikilalamika kuibiwa kura.
Alisema katika uchaguzi huo hakuna masanduku ya kura yaliyopotea wala kituo ambacho kura zake hazikuhesabiwa. Alidai kwamba kama Chadema kisingefanya hujuma, kisingepata kura zaidi ya 1,000.
Baada ya Nchemba iliwadia zamu ya Nape. Vurugu zilitokea mara mbili wakati kiongozi huyo machachari wa CCM alipokuwa akihutubia.
Nape alianza kwa kuwapongeza Nchemba na Lusinde akisema walipokuwa wakizungumza walikuwa wakikamata pua za wagonjwa wakorofi ili yeye aweze kuwanywesha dawa.
Wakati akihutubia, vijana wa Green Guard walianza kufanya doria kuwasaka wazomeaji na kijana wa kwanza alikamatwa na kushambuliwa na vijana zaidi ya saba kiasi cha kumfanya Nape kukatisha hotuba yake kumuokoa.
Hali ilichafuka tena pale aliposema viongozi wa upinzani hawana uchungu na nchi na kwamba CCM ni waungwana na ndiyo maana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu wake Mkuu, Dk Wilibroad Slaa hawajawahi kuguswa kwa risasi huku akiwahoji kuwa tangu siasa za vyama vingi zianze ni wapi ambako viongozi hao walifanyiwa hivyo? Hata hivyo, alijibiwa kwa nguvu na kundi la watu ... “Arusha.”
Majibu hayo yalisababisha vurugu nyingine kwani kijana mwingine alikamatwa na kuanza kupigwa na vijana hao wa CCM kabla ya gari la Polisi kuwasili na kuanza kuzunguka katika uwanja huo kulinda amani.
Mkutano huo unadaiwa kuwa ni wa maandalizi ya kampeni za kuwania kiti cha udiwani wa Kata ya Kirumba ambacho kipo wazi baada ya diwani wake, Novatus Manoko (Chadema) kufariki dunia.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment