Wednesday, October 19, 2011

Nape Nnauye:Tofauti Kubwa ya Kipato ni Hatari Kwa Amani Ya Nchi

Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM Ndg. Nape Nnauye
---



Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM Ndg. Nape Nnauye amesema ipo haja sasa kujadili kwa kina namna ya kupunguza tofauti kubwa ya kipato iliyopo kati ya masikini na matajiri kwani ni hatari kwa amani ya nchi. Nape ameyasema hayo kwenye viwanja vya sokoni Igoma jijini Mwanza wakati akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara ulioandaliwa na Chama hicho katika ziara ya baadhi ya viongozi wa Chama hicho mkoani Mwanza. Nape alisema nchi nyingi duniani machafuko tunayoyaona ni matokeo ya kuachiwa kukua kwa tofauti kubwa ya kipato iliyopo kati ya masikini ambao ndio wengi kwa idadi na matajiri ambao kwakweli ni wachache. " ukiona mwenzio ananyolewa wewe tia maji!.. Heri kuziba ufa kuliko kujenga ukuta.



Ni muhimu leo wapenda amani wa nchi hii tujadili kwa kina namna bora ya kupunguza tofauti kubwa ya kipato nchini kwani ikiachwa hivi baada ya muda nchi hii itachafuka" alisema Nape. Aliwageukia vijana na kusema kuwa ikiwa vijana ambao ndio wenye nguvu kucha kuchwa wanabakia kulumbana juu ya siasa tu vijiweni bila kutafakari na kujituma kupunguza tofauti hii kubwa ya kipato kati ya masikini na matajiri nchini, wao ndio waathirika wakubwa kwani wataishi leo na kesho. Alisisitiza kuwa Tanzania sio masikini kwa rasilimali ilizonazo lakini mara kadhaa wamekuwa wanatokea watu si waaminifu wakipewa dhamana wanazitumia vibaya matokeo yake rasilimali inatumika kuneemesha watu wachache.



Akatoa wito kwa vijana kuwa, kwa maswala yanayohusu matumizi mabaya yarasilimali za umma lazima waende mbali zaidi ya mipaka ya itikadi, akiwataka washikamane na kutosahau kuwa wao wanadhamana ya leo na kesho. "Hivi uzalendo leo uko wapi? Unaweza kukuta Mtanzania tena kijana anashabikia watu kutumia watakavyo rasilimali za nchi hata kuhujumu nchi na bado akaonekana ni shujaa! Tusipoamua kubadilika tutakua tunabomoa nchi kwa mikono yetu wenyewe." alisema Nape kwa uchungu. Aidha Nape ameitaka wizara ya uwezeshaji chini ya Dr. Mary Nagu kuhakikisha wanaowezeshwa kwa sehemu kubwa ni vijana wazalendo wa kitanzania kwani hiyo ni njia moja wapo ya kupunguza tofauti kubwa ya kipato kati ya masikini na matajiri.



" lengo la wizara ile ni kuhakikisha wazalendo wa kitanzania wanawezeshwa kuumiliki uchumi wao, sasa isije wakawa wanaongezewa uwezo matajiri tu na vijana masikini wa kitanzania wanaachwa wakitoa macho, hiyo haitakuwa sawa! Tutaomba wizara itoe takwimu kila mara za Idadi ya wanaowezeshwa na ni kina nani" alisisitiza Nape. Naye Katibu wa NEC uchumi na fedha Ndg. Lameck Nchemba Mwigulu akisalimia wananchi wa jiji la Mwanza alihoji ugonjwa gani unawaingia watanzania leo kiasi kwamba muda wote wanawaza uchaguzi tu mpaka wamesahau hata kufanya shughuli za maendeleo.



" sikuhizi ni rahisi kukuta watumishi wengi hata serikalini wanajadili uchaguzi wa mwaka 2015 utadhani ni kesho, kama vile wameagana na Mungu watakua hai. Wanajadili kiasi cha kusahau hata kuwajibika. Nani katuloga sisi?" alihoji Nchemba. Huku akishangiliwa kwa nguvu na kelele za kufurahia ushindi wa CCM Igunga, Mwigulu alisema anashangazwa na kelele zilizopigwa na Chadema kuhusu ushindi wa CCM Igunga kwani taratibu zote zilifanyika kwa uwazi na ukweli kiasi hata kipofu angeweza kuona kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.



" nilistuka nilipowasikia baadhi ya viongozi wa Chadema wakilalamikia matokeo ya uchaguzi mdogo wa Igunga, lakini nashukuru kwa sasa wamenyamaza kwasababu wameona aibu kuendelea kulalamika katika mazingira yale" alisikika Nchemba. Aidha Nchemba alikemea utaratibu ambao umeanza kujengeka hasa kwa nchi masikini zinazoendelea,wa viongozi wengi wa kisiasa na vyama vyao kuudanganya umma kuwa kila wanaposhindwa uchaguzi basi haukuwa huru na haki, mpaka washinde wao ndio uchaguzi unakuwa huru na wa haki. Ziara hiyo ya viongozi wa CCM taifa kanda ya ziwa itaendelea kwenye wilaya ya Geita na Ukerewe, lengo likiwa ni kuamsha ari ya wanachama hasa baada ya uchagizi mkuu wa mwaka jana ambapo CCM inaonekana kuto fanya vizuri kama ilivyokua mwaka 2005.



Pamoja na Nape na Nchemba, msafara huo pia umeambatana na Mhe. Livingstone Lusinde ambaye ni Mbunge wa Mtera na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, pamoja na Katibu Msadizi Mkuu wa Idara ya Itikadi Ndg. Sixtus Mapunda.



No comments: