Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe leo amepelekwa nchini India kwa matibabu zaidi ya ugonjwa wa ajabu uliomuanza kiasi cha miezi mitatu iliyopita kabla ya hali kubadilika siku za karibuni na hatimaye mwili wake kunza kuvimba na ngozi kuharibika.
Msemaji wa familia ambaye pia ni Mbunge wa Lupa Mh Victor Mwambalaswa amesema kwamba hali ya ngozi Dk Mwakyembe ni mbaya, japokuwa ana nguvu zake na fahamu na anaongea bila shida na anatembea mwenyewe.
Viongozi kadhaa akiwemo Waziri wa Ujenzi Dk John Pombe Magufuli walikuwepo Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar kumsindikiza Dk Mwakyembe, ambaye jana alitembelewa na Rais Jakaya Kikwete nyumbani kwake Mbezi Beach.
Kwa mujibu wa mke wa Dk Mwakyembe, Mama Linah Mwakyembe, daktari wa mumewe amesema mgonjwa anasumbuliwa na ugonjwa wa ngozi unaojulikana kitaalamu kama Exfoliative Dermatitis.
“Alianza kuugua muda mrefu kidogo, kama miezi mitatu iliyopita, hali hiyo ilikuwa inatokea na kupotea hadi sasa ambapo hali imekuwa mbaya zaidi,” alisema.
Alisema madaktari waliomfanyia uchunguzi kwa nyakati tofauti katika kipindi hicho walitoa majibu tofauti na kuongeza kuwa wapo waliosema hali hiyo ilisababishwa na kisukari na mwingine ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kulikuwa na chembechembe za sumu katika damu yake.
Kwa mujibu wa Linah, ngozi ya Dk Mwakyembe inawasha na inakuwa kama inatoa mba mwili mzima hadi kichwani.
No comments:
Post a Comment