Thursday, October 27, 2011

SIMBA HAINA IMANI NA MWAMUZI ODEN MBAGA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SIMBA SPORTS CLUB (SSC) imetatizwa na hatua ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kumteua mwamuzi Oden Mbaga kuchezesha mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Yanga Jumamosi ya Oktoba 29 mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa Oden Mbaga ndiye mwamuzi aliyechezesha pambano la mwisho la watani wa jadi katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu uliopita.
Pambano hilo nusura lisababishe vurugu baada ya Mbaga kukataa bao la wazi la Simba lililofungwa na Mussa Hassan Mgosi katika dakika ya 73 ya mchezo huo uliochezwa Machi mwaka jana.

Alibadili maamuzi yake na kukubali baada ya ama kulalamikiwa na washabiki na wachezaji wa Simba au kwa kujionea mwenyewe picha za marudio zilizoonyeshwa na kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini zilizothibitisha kuwa goli hilo lilikuwa halali.

Udhaifu huo wa kimaamuzi ungeweza kusababisha maafa makubwa uwanjani.
Ndiyo maana, Simba imetatizwa na uamuzi wa TFF kumteua tena Mbaga kuchezesha mechi hiyo, pamoja na makosa yake ya wazi aliyoyafanya katika mechi hiyo kubwa.

Simba Sports Club haina imani tena na Oden Mbaga kutokana na historia yake katika mapambano yaliyopita dhidi ya timu yetu.

Kwa taarifa hii, Simba SC inapenda kuutangazia umma kuwa japo haina imani na Mbaga, haitasusia pambano hilo kwa namna yoyote ile lakini inapenda kuweka wazi msimamo wake huo kuhusu mwamuzi huyu.

Ni matumaini yetu kuwa ujumbe huu utamfikia Oden Mbaga mwenyewe na wote waliohusika katika kumpanga awe mwamuzi katika pambano hilo.
Tunatanguliza shukrani.
Ezekiel Kamwaga
Msemaji
Simba SC

No comments: