Tuesday, October 4, 2011

Taarifa kutoka shirikisho la soka nchini (TFF) leo

TAIFA STARS KUAGWA OKTOBA 6
Taifa Stars inatarajiwa kuagwa Oktoba 6 mwaka huu saa 4 asubuhi kambini kwao hoteli ya Chichi iliyoko Kinondoni, Dar es Salaam kabla ya kuondoka siku hiyo hiyo mchana kwenda Casablanca kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco.

Mechi hiyo ya mwisho ya mchujo kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani katika nchi za Equatorial Guinea na Gabon itachezwa Oktoba 9 mwaka huu katika mji wa Marrakech.

Wachezaji wanaocheza nje ya nchi ambao tayari wameripoti Taifa Stars ni Idrissa Rajab anayechezea Sofapaka ya Kenya, Mbwana Samata (TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada) na Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden).

Washambuliaji Abdi Kassim na Dan Mrwanda wanaocheza mpira wa kulipwa nchini Vietnam wao wanatarajiwa kuwasili nchini leo (Oktoba 4 mwaka huu) saa 8 mchana.

LIGI DARAJA LA KWANZA
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itakuwa na kikao na viongozi wa klabu zote 18 za Ligi Daraja la Kwanza. Kikao hicho kitafanyika Oktoba 10 mwaka huu saa 4 kwenye ofisi za Shirikisho.

Klabu ambazo timu zake zinashiriki Ligi Daraja la Kwanza itakayoanza kutimua vumbi Oktoba 15 mwaka huu ikichezwa katika makundi matatu tofauti ni AFC ya Arusha, Burkina Faso ya Morogoro, Majimaji ya Ruvuma, Mbeya City Council ya Mbeya, Mgambo Shooting ya Tanga, Mlale JKT ya Ruvuma na Morani ya Manyara.

Nyingine ni Polisi ya Dar es Salaam, Polisi ya Iringa, Polisi ya Morogoro, Polisi ya Tabora, Rhino Rangers ya Tabora, Samaria ya Singida, Small Kids ya Rukwa, Tanzania Prisons ya Mbeya, Temeke United ya Dar es Salaam na Transit Camp ya Dar es Salaam.

Majimaji na Small Kids ndizo pekee ambazo bado hazijalipa ada ya ushiriki ya sh. 200,000. Klabu hizo zimetakiwa kulipa ada hiyo kabla ya Oktoba 10 mwaka huu ambayo ndiyo siku ya kupanga ratiba.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments: