Tuesday, October 4, 2011

Igunga: CCM 50.56%, Chadema ni 44.32%





Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imemtangaza mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Dallaly Kafumu, kuwa mbunge wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kikisema kitakwenda mahakamani kupinga ushindi huo.
Akitangaza matokeo hayo jana mchana, Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Protace Magayane, alisema Dk. Kafumu alishinda kwa kura 26,484 sawa asilimia 50.56.
Alisema mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye, alipata kura 23,260 sawa na asilimia 44.32 wakati mgombea wa CUF, Leopard Mahona, aliambulia kura 2,104 sawa na asilimia 4.01.

Wagombea wengine na kura zao katika mabano kuwa ni Stephen Mahui wa AFP (235), Hassan Lutegeza wa Chausta (183), Said Cheni wa DP (76), John Maguma wa Sau (83) na Hemed Dedu wa UPDP (63).
Alisema idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika daftari la wapiga kura walikuwa ni 171, 019 na waliopiga kura walikuwa ni 53,672 halali 52,487 na zilizoharibika 1,185.
Magayane alisema kuchelewa kutangazwa kwa matokeo kulitokana na kuchelewa kuletwa kwa matokeo kulikosababishwa na mvua zilizonyesha.
Alisema matokeo hayo kutoka katika vituo vya kupigia kura yalianza kujumulishwa saa 4:30 juzi usiku. “Pili huu mfumo ambao tunatumia wa result management system stage zote lazima uzipitie huwezi kutumia shortcut, lakini hatujachelewa kwa sababu Tume ilitupa mpaka tarehe nne (leo) na sisi tumetangaza leo (jana) bado tuna siku nzima ya kesho (leo) kwa hiyo tumewahi,” alisema Magayane.
KASHINDYE AGOMEA MATOKEO
Alisema wagombea saba walikubali matokeo hayo, lakini mgombea wa Chadema Kashindye alikataa kusaini fomu hiyo baada ya kuona idadi ya kura alizozipata katika uchaguzi huo uliofanyika juzi.
KAFUMU AOMBA USHIRIKIANO
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Dk. Kafumu aliwataka wagombea wenzake kushirikiana nao kwa kufanya mkutano wa pamoja utakaozungumzia maendeleo ya Igunga.
“Kwa sababu maendeleo hayana chama ni ya watu wote. Mwenendo wa kampeni ulikuwa sio rafiki sana, walikuwa wakitumia maneno na matusi kidogo na walitumia watu kusema watu kama mimi. Walitumia kusema kuhusu madini na mimi niliona si rahisi sana,” alisema. Alisema changamoto yake kubwa ya kwanza ni kukabiliana kwa nguvu zote na tatizo la maji ambapo alisema atahakikisha kuwa yanapatikana katika maeneo yote ya Wilaya ya Igunga.
Alisema atasema bungeni kuhusiana na madini kwa kuwa wengi wana mtazamo hasi kutokana na kuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na madini.
MTATIRO: TUMEKUBALI MATOKEO
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, alisema uchaguzi huo ulikuwa wa fedha zaidi na kwamba wao kama chama wamekubaliana na matokeo hayo.
Alisema wamejifunza vitu vingi na kwamba maamuzi ya wananchi hawawezi kuyapinga.
“Uchaguzi wa pesa, tunafikiri kama siasa za nchi hii zikiendelea namna hii maana yake mbele ya safari Watanzania watakuwa katika wakati mgumu sana kwa sababu tulikuwa na mgombea mzuri na tulifanya kampeni nzuri sana na tumefika kila eneo, lakini tunajua maamuzi ya wananchi hatuwezi kuyapinga,” alisema.
Pia alisema uchaguzi huo uligubikwa na propaganda nzito na kwamba wao walizushiwa kuwa ni CCM `B' na kuwa kuna kazi kubwa ya kufanya upande wa demokrasia.
MAHONA: WATU WALICHAGUA FEDHA
Kwa upande wake Mahona, alisema kuwa watu walichagua fedha katika uchaguzi huo mdogo badala ya kuchagua kiongozi.
“Mimi sikati tamaa, kwanza umri wangu unaniruhusu, mimi nashauri civic education (elimu ya mpigakura) iongezwe kwa hawa watu kwa sababu watu wanapoteza dhima nzima ya kuchagua kiongozi, badala ya kuchagua kiongozi wanachagua fedha,” alisema.
CHADEMA KUPINGA MAHAKAMANI
Naye Ofisa Uchaguzi wa Chadema, Basil Lema, alisema matokeo ya uchaguzi huo ni ya mzaha na inaonyesha kwamba CCM haiko tayari kufanya siasa za ushindani wa haki.
“Kwanza kumekuwa na hatua mbalimbali ambazo Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi na Takukuru wamecheza rafu nyingi kwa ajili ya kukipendelea CCM sasa haya hatuna mahali pa kushtaki, ukienda polisi wataachiwa, ukienda Takukuru hawafuatiliwi, wanawekwa `pending' njia pekee ni kurudi kwa wananchi sasa,” alisema.
Alisema watapinga matokeo hayo mahakamani na watapata jukwaa la kusemea vitu ambavyo wanavipinga.
CCM WASHANGILIA KWA MAANDAMANO
Baada ya Dk. Kafumu kutangazwa mshindi, viongozi wa chama hicho walitoka katika eneo la Halmashauri wakiwa katika maandamano makubwa ya magari hadi katika ofisi za CCM za wilaya.
CCM, CHADEMA WAPAMBANA
Wakati huo huo, vijana wa CCM, wakiwa na mishale, mikuki, mapanga jana walipambana na wafuasi wa Chadema waliokuwa wakilipiga gari la CCM mawe.
Tukio hilo lilitokea jana asubuhi wakati wafuasi hao walipohamasishwa kwenda katika Ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi kusubiri matokeo ya uchaguzi huo wakiamini kuwa wameibuka washindi dhidi ya CCM. Hata hivyo, polisi waliokuwa wamebeba mabomu ya machozi na risasi za moto, walifika katika eneo hilo nje ya Hoteli ya Peak mahali walipofikia viongozi wa ngazi za juu wa CCM, akiwemo Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, Makamu Mwenyekiti Bara, Pius Msekwa na Wabunge.
Vijana hao baada ya kupata habari ya vijana wa Chadema kutaka kuvunja vioo vya gari lao, walitoka wakiwa na mishale, mikuki na mapanga yaliyonolewa na kuanza kukimbizana.
NIPASHE ilishuhudia mmoja wa wafuasi wa Chadema akiwa na damu mgongoni baada ya kupigwa na ubapa wa mapanga hayo.
Baada ya muda kidogo, wafuasi wa Chadema walikwenda kujikusanya nje ya uzio wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kwa ajili ya kusubiri matokeo ya kura hizo.
Hata hivyo, polisi waliokuwa katika maeneo hayo waliwasihi zaidi ya mara nne kusogea kuelekea katika eneo ambalo lilizuiwa kwa utepe maalum.
POLISI WATUMIA MABOMU YA MACHOZI
Wafuasi hao waliokuwa wakiimba `peoples power' (nguvu ya umma), waliendelea kusogelea utepe huo, kitendo ambacho kiliwalazimisha polisi kufyatua mabomu ya kutoa machozi.
Polisi walilazimika kupeleka magari ya zimamoto katika eneo hilo, baada ya wafuasi hao kuwasha moto karibu na majengo ya halmashauri.
Hata hivyo, matokeo hayo yalitangazwa katika hali ya utulivu na amani huku idadi ya watu waliokuwa wakiingia katika uzio ikiratibiwa polisi.
WATU 39 MBARONI
Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia nchini (FFU), Kamishna Mwandamizi wa Polisi, Tresphory Anaclet, alisema watu 39 walikamatwa katika matukio ya kufanya ghasia katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.
Pia alisema watu wawili kati yao ambao wadaiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema, walikamatwa kwa kosa la kuhamasisha wanachama wa chama hicho kuandamana.
Wakati huo huo, vurugu nyingine ziliibuka jana jioni baada ya vijana waliokuwa wamebeba mapanga na sime kuvamia ofisi za Chadema huku wakiwa wamevaa sare za CCM na kushika bendera za chama hicho.
Vijana hao waliokuwa katika gari lililokuwa likishangilia ushindi, walivamia katika ofisi za Chadema za Wilaya ya Igunga, hali iliyowafanya vijana wa Chadema kuchukua mawe na kuanza kuwarushia.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alipiga simu polisi ambao walifika katika eneo hilo wakiwa na gari moja aina Land Crusser pick up.
Mara baada ya polisi kufika, vijana hao wa CCM walianza kuwarushia mawe askari, na polisi kurusha mabomu katikati ya mji wa Igunga. Watu walilazimika kukimbia hovyo wakikwepa mabomu hayo huku vijana hao wa CCM nao wakikimbilia katika mitaa ya katikati ya mji wa Igunga kuwakwepa askari.
Kamanda wa Polisi Mkoa Tabora, Anthony Ruta, hakupatikana kuthibitisha tukio hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: