WATOKA NJE KUSUSIA MUSWADA WA MABADILIKO KATIBA, SPIKA ASEMA MUSWADA UNAPOTOSHWA
Neville Meena, Dodoma na Raymond Kaminyoge, Dar
WABUNGE wa Chadema na NCCR-Mageuzi jana walilitikisa Bunge baada ya kuungana kutoka nje ya ukumbi kupinga kile walichodai kuwa ni Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwadharau kwa kuwanyima haki zao kwa mujibu wa kanuni.Wakati wabunge hao wakitoka bungeni kugomea muswada huo, Chama cha Majaji Wastaafu Tanzania (Tarja), kimetoa tamko kupinga hadidu za rejea za tume itakayoratibu mchakato wa kuundwa kwa Katiba Mpya kutolewa na Rais.
Licha ya Spika Makinda kuukingia kifua muswada huo katika utangulizi wake kabla ya kuruhusu uwasilishaji wa hoja kwa pande zote akisema ulifuata kanuni za Bunge, haikusaidia kwani muda mfupi baada ya Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani, wabunge hao waliamua kuondoka.
Muswada huo wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011, ambao uliwasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani umepata pia upinzani kutoka kwa wanaharakati nchini ambao wametishia kufanya maandamano nchi nzima endapo wabunge watauridhia.
Tamko la Mbowe
Baadaye wabunge hao wa Chadema na NCCR Mageuzi katika tamko lililotolewa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe walisema: “Hatutashiriki katika mchakato wote wa mjadala wa muswada huu hadi mwisho na kesho (leo) tutaeleza hatua nyingine tutakazochukua.”
Mbowe katika mkutano na waandishi wa habari uliohudhuriwa na Wabunge wa NCCR Mageuzi, David Kafulila (Kigoma Kusini) na Felix Mkosamali (Muhambwe) alisema wamelazimika kutoka nje kutokana na Spika Makinda kuonyesha upendeleo wa wazi kwa Serikali kabla ya hata muswada huo kuwasilishwa.
“Spika ameonyesha upendeleo wa wazi kabisa kwa Serikali hata kabla ya muswada huo kusomwa na waziri, katika hali hiyo haki haiwezi kutendekeza. Hatuwezi kuunga mkono kitu ambacho kinapingwa na wananchi kote nchini,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Shughuli nyingine za mkutano huu wa Bunge zilizobaki tutashiriki lakini hili la kujadili muswada huu hatuko tayari na lazima tupange utaratibu wa kuwafikishia wananchi.”
Alisema upendeleo wa Spika pia ulijitokeza wakati wabunge zaidi ya watatu wa upinzani walipoomba mwongozo na yeye kukataa wakati kanuni zinawaruhusu kufanya hivyo.
“Spika anasema eti sisi tunawapotezea muda. Kuomba mwongozo si kupoteza muda, kanuni zinaturuhusu, kwa hili ametutusi lazima atuheshimu na afahamu kwamba hata sisi tumechaguliwa na wananchi,” alisema Mbowe.
Wabunge waliokataliwa na Spika walipoomba mwongozo ni Mkosamali, John Shibuda wa Maswa Magharibi (Chadema) na John Mnyika (Chadema).
Hata hivyo, wabunge wengine wawili wa NCCR Mageuzi, Mosses Machali (Kasulu Mjini) na Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) hawakuhudhuria kikao hicho na badala yake walibaki ndani ya ukumbi wa Bunge.
Ilikuwaje?
Hali ilianza kubadilika wakati Waziri Kombani alipomaliza kuwasilisha muswada huo, kwani Mnyika alisimama na kusema: “Hoja kuahirisha mjadala,” lakini Spika alimpuuza na kumwita Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana kutoa maoni ya kamati yake.
Wakati huo, Mkosamali alisimama kuomba mwongozo wa Spika lakini pia alikataliwa na Spika akisema huo haukuwa wakati mwafaka wa kuomba mwongozo kwani muda ulikuwa hauruhusu.
Chana alipomaliza kusoma maoni ya kamati, Shibuda naye alisimama kuomba kuhusu utaratibu lakini Spika hakumpa fursa hiyo, hivyo kumwita Lissu ili atoe maoni ya Kambi ya Upinzani.
No comments:
Post a Comment