Thursday, November 10, 2011

Hukumu ya Jairo kesho bungeni



Hatma ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, aliyesimamishwa kazi na Rais Jakaya Kikwete, ili kupisha uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge, itajulikana Ijumaa wiki ijayo ripoti hiyo itakapowasilishwa bungeni.
Ripoti ya kamati hiyo itawasilishwa bungeni Ijumaa, Novemba 18, mwaka huu na Kamati iliyochunguza sakata hilo chini ya uenyekiti wa Ramo Makani.
Taarifa hiyo iliwasilishwa juzi kwa Spika Anne Makinda, ambaye aliitangaza Agosti 26, mwaka huu ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa Bunge la Bajeti.

Wajumbe wanaounda kamati hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wake, Ramo Makani (Tunduru Kaskazini-CCM); Gosbert Blandes (Karagwe-CCM); Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema); Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF) na Martha Umbulla (Viti Maalum-CCM).
Kwa mujibu wa ratiba ya Mkutano wa Tano wa Bunge iliyotolewa bungeni mjini Dodoma jana, taarifa hiyo itawasilishwa baada ya kipindi cha maswali na majibu kabla ya kuahirishwa Bunge.
Taarifa hiyo huenda ikaibua mambo mengi na kuzua mjadala mkali kutoka kwa wabunge watakaopata fursa ya kuchangia.
Tayari kamati ya Nishati na Madini imekuwa na mfululizo wa vikao tangu juzi na jana, huku habari za uhakika zikisema moja ya mambo yanayojadiliwa ni sakata hilo na utekelezaji wa mpango wa dharura wa kumaliza tatizo la umeme.
Siku moja kabla ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo, Kamati ya Nishati na Madini imepangiwa kuwasilisha taarifa ambayo hata hivyo haikutajwa inahusu nini.
Juzi, wajumbe wa kamati hiyo walikutana hadi usiku wa manane na habari zinasema kikao hicho kilijikita katika sakata hilo na taarifa ambayo inatarajia kuiwasilisha. Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, baada ya Mwenyekiti Makani kuwasilisha taarifa hiyo, kamati ya Nishati na Madini itatakiwa kutoa maoni yake.
Mjumbe mmoja wa Kamati ya Nishati na Madini, aliiambia NIPASHE kuwa juzi walikutana hadi usiku wa manane kwa lengo la kuweka msimamo juu ya sakata hilo na taarifa itakayowasilisha.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, January Makamba, alipotafutwa hakupatikana kutokana na kuwa katika kikao cha kamati yake.
Ripoti hiyo ilikabidhiwa juzi mchana kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, mara baada ya kuahirishwa kwa kikao cha Bunge. Kamati Teule hiyo iliundwa ili kuchunguza uhalali wa Jairo kuchangisha fedha kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini ili kupitisha bajeti ya wizara hiyo bungeni.
Pamoja na hilo, kamati hiyo pia itawasilisha taarifa ya uchunguzi kubainisha endapo kitendo cha Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, cha kutoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya uchunguzi wa suala la fedha zilizochangishwa, hakikuingilia kinga na madaraka ya Bunge. Luhanjo anatuhumiwa kuingilia haki, kinga na madaraka ya Bunge na kumsafisha Jairo dhidi ya kashfa inayomkabili. Jairo anakabiliwa na kashfa ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanikisha kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Katika tuhuma hizo, Luhanjo anadaiwa kutamka mbele ya waandishi wa habari Agosti 27, mwaka huu, kwamba: “Alichofanya Jairo ni utaratibu wa kawaida kabisa...na kama Jairo ataweza kuwashtaki waliomdhalilisha ni yeye tu.”
Jairo alisimamishwa kazi Julai 21, mwaka huu, kupisha uchunguzi dhidi yake, baada ya kuwapo shaka ya mazingira ya rushwa, kutokana na uamuzi wake wa kuziagiza taasisi na idara zilizo chini ya wizara yake kila moja kuchanga Sh. milioni 50 ili kufanikisha makadirio ya wizara kupitishwa na Bunge.
Uchunguzi huo ulifanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa siku 10 na kuukamilisha.
Agosti 24, mwaka huu, Jairo alirejea kazini baada ya Luhanjo kuamuru hivyo kwa madai ya kutopatikana na hatia, na kupokewa kwa vifijo na nderemo na wafanyakazi wenzake wizarani hapo.
Hata hivyo, siku moja baada ya kurejeshwa kazini, Rais Jakaya Kikwete, alimsimamisha tena kazi.
Kamati hiyo teule yenye wajumbe watano, ilitangazwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, muda mfupi kabla ya kuahirisha Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi, Agosti 26, mwaka huu. Iliundwa baada ya wabunge kuridhia ufanyike uchunguzi huo.
Miongoni mwa kazi zake, ilikuwa ni pamoja na kuchunguza sakata lote la kumsafisha Jairo dhidi ya tuhuma zinazomkabili. Kamati hiyo ilifanya kazi kwa kuongozwa na hadidu rejea tano; ya kwanza ikiwa ni kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilishwa kwa uwasilishaji wa hotuba za bajeti za wizara bungeni.
Hadidu rejea hiyo ya kwanza itakuwa na vipengele vitatu; ambavyo ni kuchunguza uhalali wa utaratibu huo kisheria na kwa mujibu wa kanuni iwapo fedha hizo huwa zinakasimiwa katika bajeti husika pamoja na matumizi halisi ya fedha zilizokusanywa.
Hadidu rejea ya pili, ni kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu uchunguzi alioufanya kuhusiana na agizo la Jairo kuchangisha fedha taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha uwasilishaji wa bajeti ya wizara hiyo bungeni. Pia kuchunguza mfumo wa serikali kujibu hoja zinazotolewa bungeni na taratibu za kuliarifu Bunge matokeo ya utekelezaji wa hoja hizo. Nyingine ni kuchunguzwa usahihi wa utaratibu uliotumiwa na Luhanjo, kwa suala la Jairo na kubaini iwapo utaratibu huo umeathiri dhana ya haki na madaraka ya Bunge.
Ya tano, ni kuangalia nafasi ya mamlaka ya uteuzi kwa ngazi ya makatibu wakuu katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya anaowateua na kuangalia mambo mengine yoyote yanayohusiana na masuala hayo.
Wakati huo huo, ratiba ya Bunge inaonyesha kwamba Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, umepangiwa kujadiliwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumatatu ijayo.
Muswada huo uliondolewa bungeni katika mkutano wa tatu kutokana na shinikizo la wanaharakati na makundi mengine ya kijamii ambayo yalitaka utolewe muda wa kutosha ili wananchi wengi wapate fursa ya kuujadili.
Katika Mkutano wa Nne wa Bajeti, muswada huo ulipangiwa kuwasilishwa na kujadiliwa, lakini uliondolewa kwa maelezo ya kuwepo shughuli nyingi katika ratiba na serikali iliahidi kuwa itawasilisha katika Mkutano huu wa Tano.
Ratiba iliyotolewa jana na Bunge, inaonyesha kuwa muswada huo utawasilishwa Jumatatu baada ya kipindi cha maswali na majibu na kuendelea kujadiliwa hadi Jumatano Novemba 16, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: