Na Magreth Kinabo – Maelezo
MSAJILI wa Vyama Vya Siasa nchini John Tendwa , amevitaka baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa , wanachama na washabiki wa vyama husika kuzingatia sheria za nchi na sheria nyinginezo
Aidha msajili huyo, amesema kuwa ni wakati mzuri wa kutenganisha mipaka ya vyama na mamlaka ya serikali kwa kutambua kwamba ipo mihimili mitatu ambayo ni Bunge, Serikali na Mahakama ambayo kila mmoja umepewa ukomo wake kimamlaka.
Kauli hiyo imetolewa leo na Tendwa kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, kufuatilia vurugu zilizojitokeza nchini ambazo zinasababishwa na baadhi ya watu hao.
“Vurugu hizi hazina tija kwa taifa na zinasababisha uvunjifu wa amani na kupelekea wananchi kutoshiriki katika shughuli za uzalishaji kwa kuwa muda wote wako kwenye mikusanyiko na wengine kuhofiwa kuathiriwa na matokeo ya vurugu hizo.
Aliongeza kuwa viongozi wa vyama vya siasa kuingilia uongozi na usimamizi wa mihimili hiyo ni kinyume na kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi, kitendo ambacho mamlaka husika lazima zikidhibiti.
Hivyo inapotokea mamlaka zikichukua hatua si busara kuanza kulalamika kwani kila mamlaka inao wajibu katika jamii.
“ Hivyo basi Msajili wa Vyama Vya Siasa hayuko tayari kuvumilia hali hii ya uvunjifu wa sheria ya usajili wa vyama vya siasa ambayo vyama vyote vina wajibu wa kuzingatia katika utekelezaji wa kila siku wa shughuli za vyama vyao,” alisisitiza.
Alisema endapo chama chochote kinaona hakikutendewa haki katika jambo lolote na muhimili wowote kama Bunge, Serikali au Mahakama ni vyema kufuata sheria, taratibu za kisheria kuwasilisha malalamiko yao sehemu husika.
No comments:
Post a Comment