Thursday, November 10, 2011

Polisi yaweka ulinzi mkali kuhofia maandamano ya Chadema katika jiji la Dar es Salaam leo

Wananchi waliofika katika ofisi za chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la ubungo kwa ajili ya kuanza maandamano ya amani ambayo yaliahirishwa kufuatia majadiliano yanayoendelea mjini Arusha baina ya jeshi la polisi na viongozi wakuu wa chama hicho, wakimueleza Mkuu wa Operesheni toka Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni aliyefahamika kwa jina la Y. J. Mrefu sababu za kutaka kuandamana.
Baadhi ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliofika kwenye ofisi za chama hicho jimbo la ubungo wakiwa na bango lao,ikiwa baada ya maandamano waliyotaka kuyafanya kuahirishwa.
Askari wa Jeshi la Polisi wakiwa wamewakamata baadhi ya vijana ambao ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa wamekaidi amri ya kutofanyika kwa maandamayo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo jijini Dar.


Mmoja wa wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akionyesha ishara ya chama hicho huku akiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi.
Ulinzi mkali ulitawala eneo lote la Ubungo leo.

Picha/Habari Na Francis Dande

Jeshi la polisi nchini leo limeweka ulinzi mkali katika maeneo ya Kimara pamoja na maeneo waliyodhania kuwa wafuasi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wangekusanyika kwa lengo la kufanya maandamano ambayo yamepigwa marufuku katika taarifa iliyotolewa na Kamishina wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja.

Wakiwa kwenye Magari yenye namba PT 1412,PT 2118, PT1848 na PT1447 askari wa jeshi hilo kikosi cha kutuliza ghasia walionekana wakiwa wanaenda mbele na kurudi nyuma katika eneo hilo la kimara kona kabla ya kuelekezwa na viongozi wao kusogelea ofisi za chama hicho ambapo wanachama wake waliweka uzio wa kamba kuzuia watu kuingia katika ofisi hizo bila ya ruhusu maalumu.

Katika eneo hilo la ofisi watu waliokuwa wamekusanyika katika ofisi hizo walisikika wakiimba nyimbo za kuhamasishana kabla ya Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, John Heche kuwaambia kuwa maandamano yameahirishwa kupisha majadiliano yanayoendelea baina ya jeshi hilo na uongozi wa Chadema Taifa.

Baada ya maelezo hayo toka kwa Heche wanachadema waliokuwa katika eneo hilo walianza kutawanyika kurudi katika shughuli zao za kawaida, kabla ya askari wa jeshi hilo waliokuwa katika gari namba PT 1447 Kuwakamata vijana watatu waliokuwa wameshika bendera ya chama hicho pamoja na kitabu cha muongozo wa katiba kwa raia wa Tanzania kilichotolewa na taasisi ya Policy Forum.

Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Suleiman Kova alisema kuwa kwa sasa hana taarifa zozote za kukamatwa kwa wafuasi wa CHADEMA na kutoa maelekezo kwa mwandishi wa habari hizi afike katika kituo cha polisi cha Urafiki kwa taarifa zaidi.

1 comment:

Anonymous said...

i dont belive this!y hawa vijana wamekamatwa tena jamani!