Katibu  wa machimbo ya Taru Cavin Kamtwela, akilalamika kwa waandishi wa habari  katika mkutano huo, jinsi wanavyotakiwa kumpisha mwekezaji.
Dhahabu ikiandaliwa
Wachimbaji wadogo wakikusanyika kwenye eneo la machimbo ya dhahabu, katika kijiji cha Taru, wilayani Singida.
Hii ni Guest house ya eneo hilo la machimbo
Wachimbaji wa dhahabu wakionyesha mawe yenye dhahabu, ambayo yametokana na kulipuliwa na baruti chini ya ardhi.
Mmoja  wa wachimbaji wadogo akilalamika juu ya vitendo wanavyofanyiwa na  serikali kwa kushirikiana na Shanta Mining, ili waondoke eneo hilo. 
Wachimbaji hawa hupata mlo wao kwa kina mama kama hawa, waliopo katika maeneo hayo ya mgodi nao wakijitafutia riziki yao 
Singida  
Novemba 10,2011. 
WACHIMBAJI  wadogo wa dhahabu katika vijiji vya Taru na Sambaru, wilayani Singida,  wamepinga kuondolewa kwa nguvu kwenye eneo lao, ili kumpisha mwekezaji  wa madini, kutoka nje ya nchi, kampuni ya Shanta Mining Ltd.  
Walitoa msimamo huo juzi, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye machimbo hayo katika kijiji cha Taru,  kujadili eneo lao wanalotaka kuporwa ili kuipisha kampuni hiyo,kufungua mgodi mkubwa wa dhahabu.  
Walieleza  kusikitishwa na hatua ya serikali kumkumbatia mwekezaji huyo, badala ya  wachimbaji wadogo kumilikishwa wao eneo hilo, ili wapatiwe vibali  halali, kwa ajili ya kuendesha kazi zao kisheria.  
Wakizungumza  katika mkutano huo, mwenyekiti wa kitongoji cha Taru Emmanuel  Sawa,katibu wa wachimbaji hao Cavin Kamtwela na mchimbaji Said Hamad  Sabodo,walidai kuvumbua eneo hilo, baada ya kutolewa kwa nguvu eneo  linguine, ambalo pia walielezwa kumpisha Shanta.  
Kutokana  na mgogoro huo, wameomba msaada kutoka kwa mashirika, asasi za kiraia,  watu na wanaharakati wanaojishughulisha na utetezi wa haki za binadamu,  kwenda ili kujionea hali halisi na baadaye wasaidie katika mapambano  hayo.    
Kamishina  msaidizi wa madini kanda ya kati ambayo ofisi zake zipo mkoani Singida,  Manase Mbasha alisema kuwa, wachimbaji hao wakiondoka kwenye eneo hilo,  watapatiwa lingine, baada ya kumpisha mwekezaji huyo.  
Afisa  madini huyo alifafanua kuwa, eneo linalotarajiwa kutumika kwa ajili ya  kufungua mgodi, linajumuisha vijiji vya, Sambaru, Taru na Samumba,  katika halmashauri ya wilaya ya Singida.  
Kwa  mujibu wa Mbasha, mwekezaji huyo ameomba leseni tatu kwa ajili ya  kufungua mgodi, na tayari amemaliza shughuli za utafiti tangu oktoba  mwaka huu, kazi aliyoianza mwaka 2003. 
Na Elisante John 
No comments:
Post a Comment