Monday, November 7, 2011

Street University Kutua Arusha

Wakati maandalizi kuelekea kwenye tamasha kubwa la ujasiriamali la Street University yakizidi kupamba moto, kila mtu ana hamu kubwa ya kuhudhuria ili kujifunza mambo mbalimbali. Katika tamasha hilo kubwa, wakazi wa Arusha na maeneo ya jirani watafundishwa namna ya kupata utajiri na mbinu za kufanikiwa maishani na wawezeshaji mahiri, Eric Shigongo na James Mwang’amba kupitia asasi yao ya Street University.


STREET UNIVERSITY NI NINI?

Street University ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa na vijana wawili wa Kitanzania, Eric Shigongo na James Mwang’amba mwaka 2008 wakiwa na lengo la kuwaongoza Watanzania kuelekea kwenye mabadiliko ya akili na kuwafikisha kwenye mafanikio ya kweli.

Wamesafiri ndani na nje ya Tanzania wakifanya semina kwa maelfu ya vijana kwa lengo la kuwakomboa kutoka kwenye utumwa wa akili ambao umewafanya wengi kuishi kwenye umaskini wakati walitakiwa kuwa mabilionea kwani wamejaa vipaji na nguvu iliyojificha ndani ambayo haijatumiwa. Safari hii ni zamu ya Arusha.

KUHUSU TAMASHA LA STREET UNIVERSITY

Tamasha la Ujasiriamali la Street University linatarajiwa kutimua vumbi Novemba 27, mwaka huu kwenye Viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuanzia saa 5 asubuhi. Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo, James Mwang’amba, dhima kuu itakuwa ni Kujikomboa na Kuondoa Umaskini Kupitia Biashara na Ujasiriamali.


MADA ZITAKAZOTOLEWA

Miongoni mwa mada zitakazotolewa kwenye tamasha hilo ni namna ya kujiajiri, kupata wazo la kibiashara, namna ya kuomba mikopo benki na jinsi ya kupata utajiri kwa muda mfupi. Kiingilio kitakuwa ni shilingi elfu tano (5000) tu ambapo pia kutakuwa na burudani kabambe kutoka kwa wasanii wa muziki wa injili na kizazi kipya Bongo, Christina Shusho, Bonny Mwaitege, Abass Hamis Kinzasa ‘20%’ , Glorious Singers, Dot Com Generation na wengine wengi.

Tamasha hilo linadhaminiwa na Kampuni ya Global Publishers Ltd kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi ya Watumishi wa Umma (PSPF), Triple A Radio (88.5 FM), Sunrise Radio (94.8 FM), Mambo Jambo Radio (93.0 FM), Radio 5 (94.8FM), Hoteli ya Kibo Palace, zote za Arusha na Chama cha Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA).

No comments: