KAMANDA WA POLISI WA MKOA WA MBEYA ADVOCATE NYOMBI AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI HIVI KARIBUNI KUELEZEA MATUKIO MBALIMBALI MKOANI HUMO.KUSHOTO AFISA UPELELEZI MKOANI MBEYA ANACLETUS MALINDISA.
WATOTO wawili wamemcharanga mapanga na kumuua Baba yao mzazi ametambulika kwa jina la Dickson Jira (57) wakigombea urithi.
Tukio hilo limetokea Novemba 4 mwaka huu katika Kijiji cha Ichesa wilayani Mbozi mkoani Mbeya majira ya saa Kumi na moja Jioni.
Wakizungumza na mwandishi wetu, mashuhuda wa tukio hilo la mauaji walisema watoto hao hawakuwa na maelewano na Baba yao mzazi baada ya kuwagawiwa urithi wa mashamba ya kahawa ambayo watoto hao baadaye waliyauza.
Walisema kuwa baada ya kutokea kutokuelewana na mzazi wao ndipo wakapanga njama za kutekeleza adhima yao ovu ya kumuua kwa kumkatakata kwa Mapanga kisha kutorokea kusikojulikana.
Akithibitisha juu ya mauaji hayo Diwani wa kata ya Myovizi Sunday Shulla alisema kutokana na tukio hilo la kinyama, wananchi watashirikiana na Jeshi la polisi kuhakikisha watuhumiwa hao wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Wakati huo huo, mfanyabiashara wa zao la Kahawa (Buni) Abisai Simbaya (35) ameachiwa huru katika mazingira ya kutatanisha baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi katika kituo kidogo cha kata ya Iyula akiwa na noti bandia zenye thamani ya Shilingi milioni tatu.
Tukio hilo lilitokea Novemba Mosi mwaka huu katika eneo hilo la Iyula ambapo inadaiwa kuwa mtuhumiwa alikamatwa akiwa na shilingi milioni sita, milioni tatu zikiwa halali na nyingine zikiwa za bandia.
Mfanyabiashara huyo wakati akilipia Kilo elfu nne za Kahawa aliyonunua kwa wakulima wa kijiji hicho ndipo alipokamatwa na Polisi ambao katika hali isiyokuwa ya kawaida Polisi hao waliteketeza kwa moto noti zote kituoni hapo.
Kaimu kamanda wa polisi mkoani Mbeya Anacletus Malindisa alipohojiwa kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo alisema kuwa hakupata taarifa zozote juu ya sakata hilo na kwamba atalifuatilia ili kujua undani wake.
No comments:
Post a Comment