Sunday, December 4, 2011

Benki ya Twiga kutumia miundombinu ya Benki Ya Posta kutoa huduma za kifedha


KATIKA jitihada za kuboresha huduma za kibenki na kusogeza huduma zaidi kwa wateja, Benki ya Twiga Bancorp Limited inaanzisha ushirikiano na Benki ya Posta Tanzania kutoa huduma ya kusafirisha pesa (monygram).

Akiongea na gazeti hili, katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (sabasaba) ambako benki ya Twiga inashiriki maonesho ya miaka 50 ya uhuru, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Twiga, Hussein Mbululo alisema katika juhudi za benki ya Twiga kuboresha huduma na kuzifanya kuwa za uhakika, benki hiyo imeamua kwa kanzia kutumia miundombinu ya benki ya Posta Tanzania kuwafikia wateja wake.

Amesema utaratibu huo utaanza kutumika mapema mwaka ujao.

“Kufuatia kuongezeka kwa ushindani katika biashara ya kutuma pesa, benki yetu imeamua kujizatiti kwa kutumia mtandao wa benki ya posta kufikisha huduma kwa wateja wote kote nchini, hii itasaidia kufanya huduma zetu kuwa nzuri na za uhakika,” alisema Mbululo.

Alisema utaratibu wa kutuma pesa kwa njia ya moneygram ni huduma ya pekee inayotolewa na benki ya Twiga na kwamba unamuwezesha mteja kutuma na kupokea pesa akiwa nje na ndani ya nchi.

Benki ya Twiga pia inatoa huduma za fedha kwa kutumia mtndao wa Umoja Switch Automatated Teller Machine.

Kwa mujibu wa Mbululo, benki ya Twiga ilianzishwa mwaka 1992, wakati huo ikiitwa National Bureau De Change.

Hata hivyo mwaka 1998, beni ya Twiga ilibadilishwa na kuwa benki isiyopokea amana lakini ikajikita zaidi katika kutoa huduma za kibenki.

Akielezea mafanikio ya benki hiyo, Mbululo alisema Twiga imekuwa benki pekee ya wazawa ambayo imeweza kustahimili changamoto mbalimbali katika ushindani pasipo kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Alisema mbali na kutengeneza faida kubwa kila mwaka, kufikia Sepemba, 2011 benki ilikuwa imepokea kiasi cha Sh 50 billioni kutoka kwa wateja na kutoa mikopo ya kiasi cha Sh 30 billioni.

Mbululo aaliongeza kuwa, benki ya Twiga ambayo kwa sasa ina matawi manne, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha inafanya mandalizi ya kufungua matawi zaidi katika mkoa wa Dodoma na Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mbululo alihaidi kuwa benki yake itaendelea kusimamia na kuwasaidia wajasiriamali wadogowadogo (SMEs) kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu naya uhakika kwani ndio hasa kichocheo cha ukuaji wa uchumi nchini.

Kwamujibu wa Mbululo benki inajipanga kuzidi kujiimarisha kwa kuboresha huduma mbalimbali ili kuendana na wakati na kuhimili ushindani kutoka kwa benki zaidi 40 za kibiashara hapa nchini.

Ameongeza kuwa, benki inawashauri na kuwataka wananchi kufungua na kutumia akaunti za watoto yaani ‘Twiga Kids Account na ile ya Holiday Account’ ambazo zimeanzishwa hivi karibuni kwa madhumuni ya kuwasaidia wazazi na walezi kuwawekea akiba watoto wao pamoja na kuweka fedha kwaajili ya safari za mapumzikoni na wakati huu wa siku kuu.

No comments: