Tuesday, December 20, 2011

Mh. Gallawa atembelea idara ya mahakama Mkoani Tanga na akutana na changamoto mbali mbali

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni Mstaafu Chiku Gallawa (katikati) akisalimiana na Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mkoa wa Tanga,RMA Chuma, mara alipofika kutembelea idara ya mahakama mkoani Tanga.
Mkuu wa mkoa wa tanga Luteni Mstaafu Chiku Gallawa akiweka saini kwenye kitabu cha wageni alipofika kwenye ofisi ya Jaji Mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Tanga, jaji Mussa Kipenka, wengine katika picha ni Mkuu wa wilaya ya tanga,Dkt Ibrahim msengi, msaidizi wa Mkuu wa Mkoa Joseph Sura, hakimu mfawdihi wa mkoa Bw. Chuma na msajili wa mahakama kuu kanda ya Tanga Bw. Benedict Mwingwa.
Msajili wa Mahakama kuu Kanda ya Tanga, Bw. Benedict Mwingwa (kulia) akimweleza Mkuu wa mkoa wa Tanga,Chiku Gallawa (mwenye kilemba) eneo ambalo kesi za mahakama kuu zinapofanyika, wengine kutoka kulia kwa msajili ni Jaji Musa Kipenka, Jaji Rose Teemba na wa kwanza kushoto ni Hakimu mfawidhi wa mkoa RMA Chuma.
Mkuu wa mkoa wa Tang,Chiku Gallawa akiwa ameshika mbegu ya mti wa mwembe ambayo alipewa ili aupande kama kumbukumbu katika eneo hilo alilotembelea leo asubuhi huku wenyeji wake wakimtazama.

Na Mashaka Mhando,Tanga

IDARA ya mahakama mkoani Tanga, imesema kuwa kutokuwepo kwa mahakama za wilaya za Kilindi na Mkinga, kumesababisha wananchi katika wilaya hizo kutembea umbali mrefu kufuata mashauri mbalimbali ya kisheria katika wilaya jirani.

Msajili wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga, Bw. Benedict Mwingwa alimweleza Mkuu wa mkoa wa Tanga, Luteni (Mstaafu) Chiku Gallawa, alipotembelea leo idara hiyo kuona namna wanavyokabiliana na changamoto mbalimbali za kisheria.

Bw. Mwingwa alisema kwa wilaya ya Kilindi ambapo wamepewa jengo lililokuwa ofisi ya zamani ya Mkuu wa wilaya hiyo, lakini sasa linahitaji kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 35 gharama za ukarabati wa jengo hilo ikiwemo kuzungusha uzio kwa vile jengo hilo lipo jirani na makazi ya watu halikadhalika wilaya ya Mkinga nako wanahitaji kujenga jengo jipya.

“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa kwa vile umekuja kutembelea, tunashida kubwa wananchi katika wilaya za Kilindi na Mkinga hawana mahakama wanalazimika kutembea umbali mrefu za zaidi ya kilomita 130 kufuata huduma ya kimahakama, tunaomba suala hili utasaidie kama kiongozi wetu hapa mkoani,” alisema Msajili huyo.

Awali Jaji Mfawidhi wa mahakama Kuu kanda ya Tanga, Jaji Mussa Kipenka, alisema kuwa idara ya mahakama mkoani humo, imekuwa ikihudumia kesi mbalimbali zikiwemo za mabaraza ya ardhi, mauaji pamoja na kesi zinazoonekana kutamalaki za madawa ya kulevya ambazo zimekuwepo kutokana na mkoa huo, kuwa na watu wengi wanaopitisha kutoka mpakani.

Alisema kwa sasa wanazo kesi kubwa mbili za madawa ya kulevya ambazo pamoja na kesi nyingine zimefikia katika hatua ya kusubiri upelelezi wa polisi ili zifikie tamati.

Mkuu wa mkoa ambaye alipata fursa ya kupanda mti wa kumbukumbu katika eneo la mahakama hiyo, alisema idara ya mahakama ni sehemu muhimu katika kutoa haki kwa wananchi hivyo alishukuru na kuwasihi waendelee kufuata sheria.

No comments: