Wednesday, December 28, 2011

Naibu waziri wa maji aamuru mkandarasi aongeze nguvu
Singida.
Desemba 28,2011.
NAIBU waziri wa maji, Mhandisi, Gerson Lwenge, ameitaka kampuni ya Spencon Service Ltd ya Kenya, kukamilisha mradi wa maji hadi kufikia Juni mwakani, ili wananchi wa mji huo waweze kunufaika nao.
Mradi huo unagharimu jumla ya Sh.Bilioni 25.8, Mjini Singida,unasimamiwa na mhandisi mshauri, kampuni ya M/s Don Consult Ltd, kwa ushirikiano na Ewarema, zote za hapa nchini Tanzania.
Baada ya kupata maelezo ya Mamlaka ya Maji safi na Maji taka(SUWASA) na mhandisi mshauri (Don Cunsult), Naibu Waziri aliagiza mkandarasi huyo, akamilishe kazi hiyo Juni, mwakani, ili serikali iendelee na mipango mingine.
Mkurugenzi wa SUWASA, Kombe Mushi, alisema Mradi huo, ulioanza Novemba 2009, ulitakiwa kuwa tayari Novemba mwaka huu, lakini hadi sasa, upo nyuma asilimia 60.
Mwaka 2003, zaidi ya Sh.Bilioni 15.7, zilitolewa mkopo na Benki ya Kiarabu(BADEA) na Shirika la Mafuta Ulimwenguni(OFID),ili kutekeleza mradi huo, lakini hadi sasa ni miaka minane tangu zitolewe, fedha hizo hazijatumika ipasavyo, kutoka na sababu ambazo hazipo wazi.
Pia kiasi kingine cha zaidi ya Sh.Bilioni 10, kilitolewa na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na programu ya maendeleo ya sekta ya Maji nchini(WSDP) na kufanya jumla ya Sh.Bilioni 25.8, kwa ajili ya kuunga mkono utekelezaji wa mpango, wa mradi huo.
Na Elisante John

No comments: