Wednesday, December 28, 2011

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi:Serikali Ya Zanzibar imejizatiti Kuongeza Uzalishaji Wa Miti Mipya Ya Karafuu

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Bw Ali Mchumo ambae Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko wa pamoja na masuala ya bidhaa{cfc ulio chini ya Shirika la kimataifa la Unctad hapo afisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais Wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimueleza mipango ya Smz katika kukusudia kuimarisha zao la karafuu Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko wa pamoja wa masuala ya bidhaa {cfc } uliochini ya Shirika la kimataifa la Unctad.
---
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejizatiti kuongeza uzalishaji wa Miti mipya ya mikarafuu katika mfumo wa kitaalamu zaidi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo ambalo ndio muhimili mkuu wa Uchumi wa Taifa.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo hapo ofisini kwake Vuga wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa pamoja wa masuala ya bidhaa { CFC } Balozi Ali Mchumo ulio chini ya shirika la Umoja wa Mataifa la UNCTAD wenye makao makuu yake Mjini Amsterdam Nchini Uholanzi.


Balozi Seif alisema Serikali pia inaangalia uwezekano wa kuimarisha Miembe iliyopo ambayo embe zake zinaweza kurejea katika soko la kimataifa iwapo zitashughulikiwa Kitaalamu.

Makamu wa Pili wa Rais alieleza kwamba kumekuwa na upungufu mkubwa wa Zao la karafuu kutokana na mingi kuzeeka wakati mengine ilikuwa ikikatwa ovyo kwa ajili ya kuni na Mkaa.

Balozi Seif alimuomba Balozi Mchumo kupitia Taasisi yake kuangalia uwezekano wa kusaidia Elimu na Fedha kwa Wakulima ili kuwapa uwezo wa kuzalisha katika kiwango kinachokubalika Kimataifa.



“ Tumekuwa na maeneo mengi ya miti ya mikarafuu ambayo ina rutba ya kutosha. Hivyo tunalazimika kuyajaza lakini katika mfumo wa Kitaalamu zaidi ”. Alisisitiza Balozi Seif.

Alimpongeza Balozi Ali Mchumo kwa kazi yake nzuri inayoleta tija kwa Taifa katika masuala ya Bidhaa na kumuomba aendelee kuitangaza Karafuu kama Zao la Taifa la Zanzibar Kimataifa.



Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa pamoja wa masuala ya bidhaa { CFC } Balozi Ali Mchumo alisema Taasisi yake imekuwa ikitoa Taaluma na kusaidia katika Mazao ya Katani, Pamba, Korosho pamoja na Miembe.

Balozi Mchumo alisema Taasisi hiyo imejipanga kusaidia Taaaluma na Harakati za Kilimo cha Umwagiliaji Maji ambapo inaangaliwa uwezekano wa kujumuisha pia Zanzibar.

Mkurugeni Mtendaji huyo wa CFC ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutekeleza majukumu yake katika mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.



Alisema Dunia imeshuhudia utulivu uliopo Zanzibar hivi sasa kutokana na mfumo huo. Hivyo amesisitiza haja ya kuendelezwa amani iliyopo ambayo ndio Sera ya Taifa la Tanzania.

Katika mazungunzo hayo Balozi Ali Mchumo amekabidhi ubani wa Shilingi milioni mbili kama mchango wake binafsi na Familia yake kusaidia mchango wa Maafa kutokana na ajali ya Meli ya M.V Spice Islanders iliyotokea mwezi Septemba mwaka huu.



Balozi Ali Mchumo anatarajiwa kumaliza utumishi wake wa nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa pamoja wa masuala ya bidhaa {CFC} ulio chini ya UNCTAD mwezi Agosti Mwaka 2012.



Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar






No comments: