Thursday, December 8, 2011

Neno La Leo: Posho Za Wabunge Kwenye Shamba La Wanyama!


Pichani nikilima shamba langu la viazi kijijini Igagala, Ulembwe, Njombe Novemba mwaka 1990


Ndugu zangu,

Nimepata kuandika, kuwa dalili za simba mzee anayekaribia kufa ni kupoteza uwezo wa kuona, kunusa na kusikia.

Ndivyo ilivyo kwa chama cha siasa kinachokaribia kufa. Hushindwa kusoma alama za nyakati. Hushindwa kuona kwa uhalisia mazingira yanayokizunguka. Hushindwa kusikia yanayosemwa mitaani na vijijini.

Katika hali hiyo, chama cha siasa huonekana kuwa mbali na watu. Hakikidhi matakwa ,mahitaji na matarajio, si tu ya wanachama wake, bali ya umma. Afrika chama cha siasa hufikwa na hali hiyo pale kinapokubali kutekwa kirahisi na wachache kwa gharama ya wengi.


Niwe mkweli kwa nchi yangu. Nahofia Chama chetu tawala, yaani CCM, kimo katika hatari ya kufikwa ya simba mzee anayekaribia kufa. Na nimepata kuandika, kuwa kwa nchi yetu, ni heri kuwa na CCM imara inayoondoka madarakani kuliko CCM dhaifu kama ilivyo sasa, maana, CCM dhaifu itazaa Serikali dhaifu kesho na kesho kutwa.


Ndugu zangu,


Nimesoma gazeti la 'Habari Leo' jana Jumatano. Habari kuu inasomeka hivi; ” Spika atetea posho mpya”. Ni posho za Wabunge. Adai zimepanda kufikia laki mbili kwa siku. Amedai pia nyongeza hiyo imesababishwa na kupanda kwa gharama za maisha. 


Ndio, na nilimsikia na kumwona kwa macho yangu Spika wetu akiongea kwenye TBC1 juzi usiku. Alidai Wabunge wana shida ya kupata nyumba za kuishi Dodoma. Kwamba kulala hotelini Dodoma kwa siku haipungui laki moja.


Na gazeti ’ Habari Leo’ la jana lilisheheni habari kweli kweli, maana, habari ya pili kubwa ilisomeka hivi; ” Ole wao wanaohonga kupata uongozi"- Mukama.


Habari hiyo ilimnukuu Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama akiyasema hayo akiwa Ujerumani. Mukama anasema; ” CCM imeamua kurudi kwa wanachama na kuwasemea wananchi wanyonge. Wakulima, Wafanyakazi na makundi mengine kama walemavu, wazee, wanawake na vijana”- Anasema Mukama.


Naam, ni habari mbili zinazokinzana kwenye gazeti moja linalomilikiwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi! Ya kwanza inaonyesha chama ’ kuwakimbia’ wanyonge na ya pili inaonyesha chama kutaka kuwa ’ kimbilio’ la wanyonge! Chama cha siasa hakipaswi kuwa na tabia za kinyonga. Chama ni itikadi na itikadi zina rangi zake. Huwa hazibadiliki badiliki kama za kinyonga.


Na inakuwaje basi itikadi inapokufa na kuzikwa?


Jibu: Ndio hayo ’ maajabu’ ya habari zinazokihusu chama kimoja lakini zinazokinzana katika gazeti moja na kwa siku moja na linalomilikiwa na serikali inayoongozwa na chama hicho hicho.


Nimebahatika kuzaliwa na kukulia katika misingi ya kiitikadi ya kijamaa. Nimeishi maisha ya jeshi ( JKT) kwa mwaka mmoja- Operesheni Kambarage- 90-91. Baada ya hapo, kwa hiyari yangu, na kwa vile sikupata kuishi maisha ya kijijini, nikaamua kuishi maisha ya kijijini kwa mwaka mmoja na nusu. Niliishi kijijini Igagala wilayani Njombe, mbali kabisa na Dar es Salaam nilikozaliwa na kukulia. Nilitaka kuishi na kujifunza maisha ya kijinini.


Ndio, nami nilikuwa mkulima kijana wa zao la viazi. Wakati huo, mbolea ya kupandia aina ya ’ DAP’ tulinunua kwa shilingi elfu tano kwa mfuko mmoja wa kilo 50. Ulitosha ekari moja. Bei ya sasa ni shilingi sabini na mbili elfu. Mbolea ya Urea na ’ CAN’ enzi hizo tulinunua kwa shilingi elfu nne. Sasa inauzwa kwa shilingi sitini na tano elfu. Gharama zote hizo bado hujaongeza gharama za kuifikisha mbolea shambani.


Hivi leo Mukama anamaanisha nini anaposema Chama chake kimeamua kurudi kwa wakulima wakati Spika wa Bunge kutoka chama chake anasema kuwa wabunge watalipwa laki mbili kwa siku. Ni sawa kabisa na kulipwa mifuko miwili ya mbolea ya kupandia kwa siku. Hivi tuna mpango wa ' Kilimo Kwanza' au ' Wabunge Kwanza!"


Tujiulize, mkulima yule wa viazi kule kijijini Igagala utamwelesha vipi akakuelewa uhalali wa mbunge wake kulipwa mifuko miwili ya mbolea ya kupandia kwa siku wakati bado mbunge huyo ana mshahara wa kila mwezi. Nahofia, kuwa laki mbili hizi wanazotaka kuongezewa wabunge kama posho ya kukaa kwa siku yaweza kuwa ni gharama ya kuchimbwa kwa haraka kaburi la Chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi ujao. Wananchi wengi wamekasirishwa na hili la Wabunge kuongezewa posho.


Ni ukweli, kuwa wananchi wengi wana hali ngumu ya kimaisha kwa sasa. Ni ukweli pia, kuwa mishahara wanayolipwa wabunge wetu ni mikubwa sana kulinganisha na hali za wananchi wengi. Wabunge hawahitaji nyongeza yeyote ya posho bali labda ifikiriwe kupunguzwa ili isaidie wengine. 


Wabunge wetu wasianze kujisahau na kujilinganisha na wabunge wa Kenya na Uingereza. Wajilinganishe na wapiga kura wao. Wananchi wa kijijini Igagala Njombe na kwingineko. Walinganishe posho wanayoipata wao kwa sasa ya shilingi elfu sabini na posho ya shilingi elfu saba na mia tano ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu pale UDOM , Mkwawa na kwingineko. Tena wanafunzi hawa mwaka jana waliandamana waongezewe shilingi elfu tano tui li wapate jumla ya shilingi elfu kumi. Serikali ikasema haina fedha. 

Badala yake Serikali ikawaongezea shilingi elfu mbili na mia tano kufanya jumla ya sh. 7, 500 kwa siku. Hakika, wabunge wetu watangulize busara na kuikataa kwa sauti moja nyongeza hii ya posho katika wakati huu mgumu tulionao. Na kwanini mbunge apewe posho ya kikao ambacho ni kazi yake wakati analipwa mshahara wa mwezi kwa kazi yake?


Kwa hali ilivyo sasa, wananchi wameanza kuonyesha kuchoshwa na hali iliyopo. Wananchi hawa hawawezi kukaa kimya daima. Ni mjinga tu atakayeamini kuwa jambo hilo linawezekana. Hali isipobadilika iko siku wananchi hawa wataamka na kusema, ‘ basi, inatosha’. Watawatosa viongozi wao kupitia masanduku ya kura. Viongozi hao waking’ang’ania madaraka kuna hatari ya kuzuka kwa vurugu.

Na kuna kisa cha ndani ya kitabu cha ’ Animal Farm’- "Shamba la Wanyama". Katika kitabu hicho;Mwandishi George Orwell anatupa taswira ya jamii tunayoishi.


Mwandishi anaandika juu ya wanyama waliochoshwa na hali ya kunyanyasika kama watumwa , adha na maovu ya kila namna waliofanyiwa na Bwana Jones, mmiliki wa shamba na binadamu wengine. Wanyama waliamua kufanya maasi. Walifanikiwa na kuwaondoa shambani wanadamu wote. Walianza kujitawala. 


Hali ilibadilika ghafla. Napolioni ambaye ndiye alikuwa Nguruwe Mkuu, alianza udikteta. Napolioni alifanya matendo ya uovu. Alijipendelea na aliwapendelea nguruwe wenzake. Shambani humu tunakutana na wanyama wa kila aina, mathalan, kuna kondoo wapumbavu, na hata mbwa wenye hasira fupi za mara kwa mara. Kuna kuku na mabata wenye hofu kubwa wakati wote. 

Inaonyesha pia ni jinsi gani, baadhi yetu wanadamu, mara tu tunapokutana na madaraka, basi, huvimba vichwa na kujiona tuna tofauti kabisa na wengine tulio nao kwenye kundi moja. Tunajibagua kutoka kwenye kundi kuu na kuunda tabaka letu. Tunalewa madaraka.


Kisa cha "Shamba La Wanyama" kinatukumbusha wajibu wetu. Kwamba siku zote tuwe macho dhidi ya wale wote wenye hulka za kidikteta. Wenye kujipendelea na kutanguliza maslahi yao mbele kuliko ya umma. Wenye kufanya maamuzi bila kutuhusisha wananchi. Bila kusubiri wala kusikiliza maoni yetu. Bila kutujali. 

Katika kitabu hiki tunaona pia jinsi wanyama wanavyoshindwa kudhibiti hali iliyoko. Kudhibiti mwelekeo wao. Wanashindwa kufanya hivyo hata kama wanaona kwa macho yao maovu yafanyikayo.


Tunaona ni jinsi gani nguruwe wasivyoaminiwa na "ndugu zao". Kwa maana ya wanyama wenzao shambani. Kwamba nguruwe wameachana na dhumuni halisi la kufanya mapinduzi, kupata uhuru wao. Dhumuni la kujitawala. Nao wamegeuka wala rushwa na wasio wakweli kama ilivyo katika mashamba ya jirani. Wamelewa madaraka. 

Nguruwe hawa wanajaribu kuficha maovu watendayo kwa wanyama wenzao kwa kuwafanya waamini, kwamba bado wanapigania itikadi na malengo yale yale yaliyowalazimisha wafanye mapinduzi. 

"Komredi!" alitamka nguruwe kwa sauti kuu. "Sidhani kama mtaweza kufikiri, kwamba sisi nguruwe tunafanya haya kwa kujali maslahi yetu ikiwemo marupurupu mengine? Kwa kweli wengi wetu (nguruwe) hatupendi maziwa na matunda. Binafsi sipendi. 

Tunakunywa maziwa na kula matunda kwa lengo moja tu, kutunza afya zetu. Komredi!, Hii imethibitishwa na wanasayansi, kwamba maziwa na matunda yana vitu muhimu ndani yake. Vitu ambavyo ni muhimu kwa afya ya nguruwe.

Mnajua, sisi nguruwe tunafanya kazi kwa kutumia ubongo. Uongozi na utawala wa shamba hili unatutegemea sisi. Hatulali. Usiku na mchana tuko macho kuyaangalia maslahi yenu. Ni kwa maslahi yenu, ndio maana tunakunywa maziwa na tunakula matunda. 

Je, mnajua kipi kitatokea kama sisi nguruwe tutashindwa kutekeleza wajibu wetu? Jones (mkoloni, kama ukipenda) atarudi tena! Ndio, mkoloni atarudi tena! Komredi, nawaambia ukweli." Alitamka nguruwe kwa sauti ya kushawishi ili aaminike huku akitingisha mkia wake. " Kweli, hivi kuna mmoja wetu anayetaka Jones ( mkoloni) arudi tena? (Animal Farm, Uk. 22)


Maelezo ya hapo juu yanaonesha ni jinsi gani nguruwe kwa kutumia hisia na hofu ya Jones (mkoloni) kurudi tena kama nyenzo ya kuendelea kuwadhibiti wanyama shambani. Kwamba wao ndio wenye kuhenyeka na hivyo basi kustahili upendeleo maalumu katika jamii. 


Cha kutisha zaidi, ni ile hali ya wanyama hawa kufikia kuchinjana wenyewe kwa wenyewe kutokana na kuchanginyiwa na kukata tamaa. ( Rwanda, Kongo) Hii inatuonyesha, kuwa hata yale ambayo kimsingi yalifanywa kwa pamoja kwa nia njema kabisa , mathalan, hili la kudai uhuru wetu kutoka kwa wakoloni, hufikia mahala watu wakachinjana katika kudai haki zao. 


Tulipo sasa ni kwa baadhi ya viongozi wetu kuiegeuza nchi yetu kuwa ni gulio la mafisadi. Kwamba kila mwenye uwezo atafute mtaji. Awahi nafasi ya uongozi itakayomsaidia kuingia gulioni. Huko ni mahala pa kufanya biashara , si kuwatumikia wananchi. Kwa bahati mbaya, hata rasilimali zetu wanazipeleka gulioni. 


Ndugu zangu, 

Ili kuinusuru nchi yetu, sote kwa pamoja. Bila kujali itikadi zetu za vyama, tuna lazima ya kulifunga gulio hili. Sasa.
Nahitimisha.

Maggid,
Iringa.
Alhamisi, Novemba 8, 2011

No comments: