Friday, December 2, 2011

TAMASHA LA STREET UNIVERSITY ARUSHA


-MAMBO 5 YA KUKUMBUKWA
Na Mwandishi Wetu
Tamasha kubwa la ujasiriamali la Street University lililofanyika kwa kishindo Jumapili iliyopita ndani ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na kusindikizwa na burudani kabambe kutoka kwa wasanii kibao, limeacha historia lakini kuna mambo makubwa matano ambayo yatakumbukwa.
1.MADA ZA UJASIRIAMALI
Mada motomoto za ujasiriamali kama namna ya kupata wazo la kibiashara, kupata mbinu za kujitajirisha, kujifunza kuwa mwajiri badala ya mwajiriwa, jinsi ya kuomba mikopo mikubwa benki, kupanua mitaji na mada nyingine kemkemu zilitolewa na watoa mada, Eric Shigongo na James Mwang’amba na kuwakomboa wengi kiakili.
2.BURUDANI YA ‘KUFA MTU’
Burudani ya kukata na mundu iliyoporomoshwa na wasanii wa muziki wa Injili na wa kizazi kipya Bongo, Christina Shusho, Bonny Mwaitege, Pastor Wambura, Abbas Hamis Kinzasa ‘20%’, Kundi la Waimbaji la Glorious Singer, Dot Com Generation na wengine wengi ilizikonga vilivyo nyoyo za wote waliohudhuria.
3.WAGENI WAALIKWA
Uwepo wa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliyekaa meza moja na watoa mada, Shigongo na Mwang’amba sambamba na uwepo wa Askofu wa Huduma ya Ngurumo ya Upako, Geor Davie ulifanya tamasha hilo kuwa la aina yake.
Walikuwepo pia viongozi wengi wa kiroho na wa kiserikali ambao kwa nyakati tofauti walikiri kujifunza mengi kwenye tamasha hilo.
4.JUKWAA NA VYOMBO VYA MUZIKI
Jukwaa la kisasa lililofungwa kwenye uwanja huo na kunakshiwa kipekee sambamba na vyombo vya muziki vilivyokuwa vimefungwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ni jambo lingine la kukumbukwa. Kila aliyehudhuria alikiri kushangazwa na ubora wa hali ya juu wa vifaa hivyo vya kisasa. Pia uwepo wa kamera za kisasa zilizokuwa zinanasa matukio yote uwanjani hapo na kuyarusha kwenye website ya Kampuni ya Global Publishers www.globalpublisherstz.com ni kivutio kingine kitakachokumbukwa.
5.UMATI ULIOHUDHURIA
Watu wengi walihudhuria tamasha hilo na kufanya lengo la Street University litimie. Wengi walipata hamasa kubwa ya kuhudhuria tamasha hilo tangu taarifa zake zilipoanza kutangazwa kwenye vyombo vya habari. Wengi kati ya waliohudhuria waliondoka viwanjani hapo wakiwa na mabadiliko makubwa kwenye akili zao kuhusu mafanikio.
Tamasha hilo limefanikiwa kwa udhamini mkubwa wa Kampuni ya Global Publishers Ltd, Malta Guiness, Airtel, Azania Bank, Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Umma (PSPF), Wauzaji na wasambazaji wa vipodozi asili wa Oriflame, Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Wafanyabiashara na Wakulima (TCCIA) na Hoteli ya Corridor Springs.
Wengine ni Hoteli ya Kibo Palace ya jijini Arusha, Tripple A Radio (88.5 FM), Sunrise Radio (94.8 FM), Mambo Jambo Radio (93.0 FM), Sauti ya Redio Injili (92.2/96.2 FM) na Redio 5 (105.7FM), zote za jijini Arusha.

No comments: