Kiongozi wa Ushirikiano wa kiutafiti kati ya KCMC na Chuo Kikuu cha Afya cha Duke cha nchini Marekani, Dk Elizabeth Reddy alisema jambo la msingi katika utafiti huo ni kugundulika kwa VVU kuwa wana gamba lenye protini iliyochanganyika na sukari, ambayo huvifanya kushindwa kutambuliwa na kinga za kawaida za mwili wa binadamu. Lakini, Dk Reddy alisema kuwa katika ugunduzi wao, wamebaini aina ya kinga za mwili ambazo hutambua virusi kupitia aina hiyo ya sukari kwenye gamba la nje la VVU na kuvishambulia hadi kuviua. Alisema kuwa utafiti huo ulifanyika katika Maabara ya KCMC kwa ushirikiano wa timu ya wataalamu wa afya wa Tanzania pamoja na wa Marekani.Alibainisha kuwa utafiti huo ulihusisha Watanzania kadhaa walioambukizwa VVU hapa nchini, lakini wamekuwa wakiishi bila kuathirika. Dk Reddy alisema kuwa utafiti huo umefanyika maeneo mengi duniani, lakini kituo cha KCMC ndicho kilichotoa mwanga mkubwa ambao hatua zake za mwisho zilithibitishwa na wataalamu waliobobea nchini Marekani. Kiongozi huyo wa utafiti, alisema kuwa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa inayosimamiwa na Mfuko wa Good Samaritani (GSF) ambao ndio pia unaosimamia taasisi nyingine kama vile Chuo Kikuu cha Afya cha Tumaini na Hospitali ya KCMC, ndiyo inayopaswa kupewa shukurani kwa matokeo hayo. Mkuu wa jopo la utafiti huo, Profesa Peter Kwong wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID), amesifu utafiti huo akisema kuwa umeonyesha mwanga kwa wanasayansi kupata njia rahisi ya kugundua chanjo ya Ukimwi. Profesa Kwong alisema katika dunia wamekuwepo watu wanaoambukizwa VVU, lakini wao wenyewe hawaonekani kuathirika.Alisema kuwa ugunduzi huo pia umetoa mwanga kwa wanasayansi wengine duniani wanaofanya utafiti wa dawa nyingine za chanjo na tiba ya Ukimwi. Mchunguzi huyo nguli katika baiolojia ya chembe za urithi za mwili wa binadamu, alisema utafiti huo umebaini pia kwamba kuna baadhi ya watu ambao baada ya kuambukizwa VVU na kuishi navyo kwa miaka kadhaa, hujikuta wanajijengea kinga. Akielezea kuhusu kinga hiyo, Profesa Kwong alisema kuwa huwafanya watu hao kuwa tofauti na wengine ambao baada ya kuambukizwa VVU, mfumo wao wa kinga huathirika na kujikuta CD4 zao zikipungua siku hadi siku. Alieleza kuwa kupungua huko kwa kinga ndiko kunakosababisha muathirika kushambuliwa kirahisi na magonjwa mengine na asipotumia dawa za kurefusha maisha, hukonda hadi kufa. Jinsi utafiti ulivyofanyika Dk Reddy anasema walifanya kazi kubwa ya kutafuta watu walioambukizwa VVU lakini hawaathiriki na huweza kuishi kwa muda mrefu wakiwa na afya njema.“Tulichukua damu zao tukaziainisha chembechembe zote zilizomo kupitia maabara zetu…: Tuligundua wana chembechembe kinga za ziada,” alisema Reddy. Alisema kuwa kimsingi binadamu yeyote anapoambukizwa VVU hutengeneza kinga za kushambulia VVU.Alibainisha kuwa pamoja na hali hiyo, lakini kwa bahati mbaya kinga nyingi zinazotengenezwa huwa hafifu katika kukabili VVU aliosema, wana kawaida ya kujibadilisha. “Hali hiyo huifanya kinga ya mwili iliyotengenezwa kushindwa kukabiliana na virusi. Kwa kawaida kinga hizi huwa hafifu…; Baadhi ya vipimo vya VVU ni vile ambavyo hutambua uwepo wa virusi hawa kwa kuangalia uwepo wa kinga hizi kwenye damu,” alisema Dk Reddy. Alisema kuwa baadhi ya watu ambao huweza kutengeneza kinga imara, ndiyo ambao huonekana kuwa na virusi vichache, lakini huwa haviwezi kumuathiri kiafya muhusika.Alipoulizwa kama watu hao ndio ambao huzungumziwa mitaani kuwa wana virusi visivyooneka kuwaathiri lakini huweza kuwaambukiza watu wengi, Dk Reddy alisema “hapana!” Alieleza kuwa watu hali ya waliobainika kuwa na VVU lakini haviwaathiri hutokana na kinga yao na kwamba walibaini hata uwezo wa kuambukiza wengine ni mdogo.“Inatokana na ukweli kwamba wanakuwa na idadi ndogo ya virusi katika miili yao kwa sababu chembechembe kinga walizo nazo huviua virusi,” alisema. Alisema VVU vinadhibitiwa na chembechembe hizo za kinga hivyo hushindwa kupata fursa ya kushambulia CD4 za mwili ili kuzaliana. Alidokeza kuwa mazingira hayo ndiyo yanayosababisha baadhi ya wanandoa, mmoja kukutwa ameathirika na mwingine kuendelea kuwa na afya njema, ingawa ameambukizwa.Kuhusu sababu za baadhi ya watu kuwa na uwezo huo, Dk Reddy alisema kisayansi bado wanaendelea na utafiti. Sifa kwa Tanzania Dk Reddy alisema ugunduzi huo unawapa akili ya kutafuta namna ya kutengeneza chanjo itakayowezesha binadamu wote kuwa na chembechembe hizo kinga.Alisema kwa kiwango cha chini watahitaji miaka mitano kuweza kufanikisha upatikanaji wa chanjo hiyo. Dk Reddy alisema kitendo cha wataalamu wa Tanzania kutoa mchango mkubwa katika kufanikisha ugunduzi huo, kutalifanya taifa lipewe kipaumbele katika kutumia chanjo hiyo.Alisema kuwa chanjo hiyo itaweza kuwasaidia watu ambao bado hawajaathirika kwa kuwatengenezea kinga ambayo pia itaweza kuwa tiba kwa wale walioathirika. “Wakati wote tunapotafuta chanjo, tunajitahidi pia kutafuta tiba,” alisema Dk Reddy akisema upo uwezekano mkubwa wa kupata tiba pamoja na chanjo.Alisema muoainisho wa chembechembe hizo kinga, ulifanywa na maabara za Kimarekani kwa kuwa Tanzania haina mashine zenye uwezo huo wa juu katika kuchunguza virusi kwa undani. Ugunduzi wa kuwa VVU wana gamba lenye sukari linalowafanyia kinga ya kutogundulika kuwa ni adui ndani ya mwili wa binadamu, iliainishwa na wataalamu nchini Marekani.Kuhusu mpango wa kutengeneza chanjo hiyo, nguli huyo alisema utafanyika nchini Marekani, lakini KCMC itakuwa moja ya vituo vya kuendeleza utafiti huo duniani hadi kupatikana kwa chanjo kamili. Baadhi ya wataalamu wa Tanzania waliohusika katika utafiti huo ni Profesa Noel Sam, Profesa Saidi Kapiga na Sarah Chiduo.Wanasayansi wengine walioshiriki kwenye utafiti huo kutoka nje ya nchi ni Profesa John Bartlelt na Profesa John Crump.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment