Saturday, January 14, 2012

Ajira za walimu kutangazwa wiki ijayo

Walimu wakihakikiwa ajira zao juzi mjini singida

Gedius Rwiza
SERIKALI inatarajia kutoa tamko kuhusu ajira za walimu 25,015 waliohitimu mafunzo ya ngazi mbalimbali katika vyuo vya ualimu nchini wiki ijayo.

Kati ya hao, walimu wa sekondari ni 13,636 wa shahada wakiwa 6,649 na stashahada ni 6,987 na walimu wa shule za msingi ngazi ya cheti ni 11,379.

Hatua hiyo itaondoa hofu kwa wahitimu wa mafunzo ya ualimu ambao wamekaa nyumbani kwa zaidi ya miezi saba wakisubiri ajira, kinyume cha ahadi ya Serikali kwamba wangeajiriwa mara tu baada ya kuhitimu masomo yao.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassim Majaliwa alisema jana kuwa mwanzoni mwa wiki ijayo, Serikali itatoa tamko la ajira hizo.

Majaliwa alisema ajira hizo ni kwa ajili ya walimu waliohitimu vyuo mbalimbali vya ualimu kuanzia Mei, 2011 katika ngazi za cheti, stashahada na shahada.

“Napenda kuwataarifu walimu kwamba hakuna mwalimu atakayebaki bila kupata ajira na hatutaki mwalimu afike kituo cha kazi akose mahitaji muhimu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, kwa hiyo mwanzoni mwa wiki ijayo majina yatakuwa kwenye tovuti za Wizara ya Elimu na Tamisemi,” alisema Majaliwa..soma zaidi www.mwananchi.co.tz.

No comments: