Tuesday, January 31, 2012

Posho za waheshimiwa wabunge zasainiwa





KILA MMOJA KULIPWA 330,000 KWA SIKU, ZITTO, MAKAMBA, KIGWANGALA WASULUBISHWA KWA KUZIPINGA


Waandishi Wetu, Dodoma




WAZIRI
Mkuu, Mizengo Pinda amesema tayari Rais Jakaya Kikwete amesaini
kuidhinisha ongezeko la posho za vikao (sitting allowance) kwa wabunge
kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku. Kupitishwa kwa posho hizo
ambazo ziliandikwa kwa mara ya kwanza na gazeti hili, kunafanya sasa
mbunge kupokea Sh330,000 kwa siku; Sh200,000 zikiwa ni posho ya kikao,
Sh80,000 posho ya kujikimu na Sh50,000 nauli.


Taarifa
za uhakika kutoka ndani ya kikao cha utanguzi cha wabunge jana, zilidai
kuwa baada ya Pinda kutoa taarifa hiyo, wabunge walishangilia huku
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, akisimama na kudai
kuwa taarifa alizonazo ni kwamba Rais Kikwete alikuwa hajasaini
kuidhinisha posho hizo.


Hatua
hiyo ilisababisha Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Juma Nkamia (CCM),
kusimama na kuhoji iwapo Zitto ni miongoni mwa wasemaji wa Rais kabla ya
Pinda kusimama na kuthibitisha kusainiwa kwa posho hizo akisema siyo
ajabu kwani hata watumishi wa Serikali wanalipwa kati ya Sh150,000 na
Sh200,000. Hata hivyo, Zitto alitetea msimamo wake kwamba alitarajia
baada ya kusainiwa kwa posho hizo na Rais, angepewa masharti mapya ya
kazi za ubunge.


Katika
kikao hicho baadhi ya wabunge wanadaiwa kuwashambulia Zitto, Mbunge wa
Bumbuli (CCM), January Makamba na Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Khamis
Kigwangwala kwamba wamekuwa mstari wa mbele kupinga posho hizo
hadharani. Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye anadaiwa kwamba
aliungana na Pinda kuthibitisha kwamba Rais Kikwete ameidhinisha posho
hizo mpya, pia aliwashambulia wabunge wanaozipinga akisema kwamba
wanafuta umaarufu wa kisiasa.


“Wanachotafuta
ni umaarufu wa kisiasa tu, mimi ninavyojua umaarufu wa kisiasa unakuja
kwa kufanya kazi za kibunge za wananchi lakini siyo kupinga posho,”
chanzo chetu cha habari kilimnukuu Makinda.


Mbunge
wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa anadaiwa kwamba alitumia
mafumbo kuwashambulia wabunge hao ambao wamejitokeza kupinga nyongeza
hiyo ya posho. Kauli hiyo inadaiwa kuungwa mkono na Mbunge wa Sikonge
(CCM), Said Nkumba ambaye alidai kuwa hawezi kumsemea Zitto kwa sababu
ni kawaida yake kupinga, lakini akaelekeza shutuma zake kwa Makamba
kwamba ameanza kupinga baada ya kugharamiwa na CCM. “Januari anapinga
posho hizo kutokana na CCM kumpa gari, nyumba na analipwa na chama,”
kilisema chanzo chetu kikimkariri Nkumba.


Pia,
Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), anadaiwa kumshambulia
Zitto kuwa lazima apinge posho hizo kwa sababu, anapewa fedha na
wafadhili kutoka nchi za nje. “Shelukindo anasema amefanya ziara nje na
kuhakikisha kuna wahisani wanamfadhili Zitto kwa hiyo ana haki ya
kupinga posho hizo,” chanzo chetu hicho kilimkariri Shelukindo.



Hata
hivyo, inadaiwa kuwa baada ya mashambulizi hayo, Dk Kigwangwala
alisimama kutetea msimamo wake kwamba ongezeko hilo halina ‘mashiko’ na
haliwezi kuelezwa mbele ya umma likaeleweka, lakini alizomewa na wabunge
wengi huku wakimtaka kukaa chini.


Hatua
hiyo ilisababisha Zitto kusimama na kueleza kuwa tatizo la wabunge
kwamba wana fikra finyu, kauli ambayo alitakiwa na wenzake kuwaomba
radhi kuwa amewatukana. “Zitto ametumia Kiingereza kuwa tatizo la
wabunge ‘we think small’, Shelukindo na (John) Komba wakaja juu
wakitaka kuwaomba radhi kwa kuwatukana,” chanzo chetu kilieleza. Zitto
anadaiwa kusema wabunge walitakiwa kujenga hoja ya kuongeza fedha za
mafuta ya gari wanayolipwa hivi sasa Sh2.5 milioni kwa mwezi, kutokana
na kupanda kwa nishati hiyo, lakini siyo posho.


Mbunge
wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alinukuliwa akisema matatizo ya posho
yamefikia hapo baada ya kuonekana ni ya watu binafsi siyo mfumo hivyo,
wanaopinga wanaonekana kama wanatafuta umaarufu na wana vipato vya
fedha, akaitaka kamati ya uongozi ijadili na kupata mwafaka badala ya
wajumbe kutofautiana mbele ya umma. Wabunge wengine wanaodaiwa kutetea
posho hizo ni Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini na Jenister
Mhagama (Peramiho CCM).


Msimamo wa January


Alipoulizwa
kuhusu suala hilo, Makamba alijibu: “Si sahihi kwangu kutoa taarifa za
kikao cha ndani. Lakini msimamo wangu kwenye suala hilo unajulikana na
haujabadilika. Msimamo wa CCM ulishawekwa wazi na sote tunaujua.
Nitalizungumzia suala hili kwa kirefu katika siku zijazo.”


Kuhusu taarifa kwamba anagharamiwa na CCM, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na badala yake kutaka kiulizwe chama hicho.


Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu taratibu za
kuwagharamia viongozi wa chama chake ambao ni wabunge alisema: “Mbunge
au kiongozi yeyote wa chama mwenye nafasi nyingine anagharamiwa na chama
pale anapokwenda kufanya shughuli za chama tu na si vinginevyo.”


“Kwa
hiyo kama ni mbunge suala la mafuta, dereva, mahali pa kulala na
mahitaji mengine anagharamiwa na taasisi anayoifanyia kazi na siyo
chama.”




“Kwa
mfano, mimi kwenye sekretarieti hata posho za vikao huwa sichukui,
nadhani na mwenzangu January naye sidhani kama huwa anachukua posho, kwa
sababu tukifanya hivyo ni kama tunakiumiza chama, huo ndiyo msimamo
wetu na uko wazi wala siyo kificho.”


Kwa
upande wake, Zitto alisema jana kwamba hakuwa katika nafasi ya
kuzungumzia suala hilo na badala yake kuahidi kwamba atalizungumza leo
atakapokutana na waandishi wa habari.


Wabunge walia njaa




Taarifa
kutoka ndani ya kikao hicho zilisema wabunge hao walilalamikia
kucheleweshwa kulipwa posho zao za wiki mbili walizokaa Dar es Salaam
wakati wa vikao vya kamati.



Walidai hivi sasa wanaishi kwa shida huku wakihoji sababu za kucheleweshewa.



Imeelezwa
kwamba Spika Makinda alidai kuwa fedha hizo zipo na kwamba
kilichochelewesha ni uhakiki wa wabunge waliohudhuria vikao.


Makinda
alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wakilipwa posho za vikao bila
kuhudhuria, hatua ambayo imesababisha Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Serikali (CAG), kuhoji maswali mengi.




CHANZO: Mwananchi

No comments: