Saturday, January 14, 2012

KADA WA CCM ALIYEMWAGIWA TINDIKALI IGUNGA AREJEA NCHINI KUTOKA INDIA BAADA YA MATIBABU

MKAZI wa Igunga, Kada wa CCM, Mussa Tesha aliyekuwa katika matibabu India baada ya kumwagiwa tindikali usoni na watu wanaodaiwa kuwa wa CHADAEMA, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo jimboni humo mwaka jana, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, baada ya kurejea nchini. Kulia ni Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Mwigulu Nchemba ambaye alikuwa Meneja wa Kampeni za CCM jimboni humo.


Na Mwandishi Wetu
KADA wa CCM, mkazi wa Igunga, Tabora, Mussa Tesha (24) aliyekuwa akipatiwa matibabu India, baada ya kuwagia tindikali na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema wakati wa kampeni za uchagfuzi mdogo jimboni humo mwaka jana, amerejea nchini.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Uchumi na Fedha Mwigulu Nchemba alisema leo kwamba, Tesha amerejea juzi, akiwa amepona kiasi cha kuweza kuzungumza na kuona jicho moja huku lingine likiwa bado halioni vizuri kutokana na athari alkizopata
Akizungumza nyumbani kwake Tegeta Mwisho, Dar es Salaam, Mwigulu ambaye alikuwa Meneja wa Kampeni za CCM Igunga, alisema amemhifadhi Tesha nyumbani kwake wakati akisubiri kwenda tena India kuendelea kuendelea na matibabu madogo yaliyosalia.
Mwigulu alisema, Chama Cha Mapinduzi ambacho kiligharamia matibabu yote, hadi sasa kinaendelea kumhudumia Tesha mpaka atakapopona kabisa na kuwa na uwezo wa kufanya kazi.
"Hadi sasa tunashukuru kwamba amepona anaweza kuzungumza, kusikia na kuona walau jicho moja, tofauti na mwanzo alivyokuwa mara alipomwagiwa tindikali, hata hivyo hali yake haijaweza kuwa ya kufanya kazi mbalimbali kama za juani, hivyo CCM tunaendelea kumsaidia mpaka ajenge uwezo wa kujitegemea", alisema.
Alisema, CCM imefanya mpango wa kuwaugnanisha wabunge wa CCM kumtayarishia mtaji ambao utamsaidia Tesha kuendesha maisha yake baada ya kukumbwa na madhara hayo.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu amwagiwe tindikali, Tesha amewashukuru Watanzania kwa kumuombea wakati wote alipokuwa mgonjwa na kwamba anaamini dua zao ndizo zimemwezesha kubakia hai hadi sasa.
Tesha alisema, baada ya kumwagiwa tindikali Septemba 9, mwaka jana, hakujitambua hadi alipokuwa katika hospitali ya KCMC ambako alipatiwa matibabu na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alikaa wiki tatu kabla ya kupelekwa India.

Akiwa India kwenye Hospitali ya Apollo, Tesha alikuwa chini ya uangalizi wa baba yake mdogo, Samwel Bethwel ambaye pia gharama za kuwa huko zimebebwa na CCM. Anatarajia kwenda tena India baada ya miezi mitatu.

No comments: