Saturday, January 14, 2012

CCM yaomboleza kifo cha Mbunge regia wa Chadema


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa majonzi makubwa taarifa za kifo cha Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chadema Marehemu REGIA MTEMA kilichotokea leo kwa ajali ya gari katika wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

Chama Cha Mapinduzi kinatoa salamu za pole kwa CHADEMA, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki pamojan na watanzania wote kwa ujumla.

Marehemu MTEMA amekuwa na mchango mkubwa kwa wananchi wa kada zote wakiwemo watu wenye ulemavu ambao kwa sehemu kubwa alikuwa akiwatetea na kuwasemea katika mijadala mbalimbali ndani na nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Alikuwa ni Kiongozi aliyetetea na kuusimamia Utaifa hata pale masuala ya kiitikadi yalipokuwa yakitaka kuchukua nafasi kubwa, jambo ambalo lilisukumwa na kiwango cha uzalendo alichokuwa nacho.

Chama Cha Mapinduzi kinaungana na watanzania wote kuomboleza msiba huu mkubwa, kwa familia yake, Chadema, siasa ya Tanzania na kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambakoi ndiko alikokuwa akitumikia jukumu la uwakilishi wa wananchi.

Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.

Nape M. Nnauye

Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa

Itikadi na Uenezi

Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM

14-01-2012

No comments: