Friday, January 27, 2012

Madaktari wagoma kumfuata Pinda ofisini


Thursday, 26 January 2012 21:13

Waandishi Wetu
WAKATI mgomo wa madaktari ukizidi kusambaa nchini, wanataaluma hao wamesema hawako tayari kumfuata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ofisini kwake, badala yake yeye awafuate wanakofanyia mikutano yao.

Juzi, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Pinda aliwaangukia madaktari hao kuwa yupo tayari kukutana nao wakati wowote na kuwataka waende ofisini kwake kuonana naye ili wazungumze kuhusu madai yao.

Mgomo huo wa madaktari ambao ulianzia katika hospitali za Muhimbili na Ocean Road, hadi jana ulikuwa umesambaa katika hospitali nyingine nchini ambazo ni pamoja na Bugando ya Mwanza, KCMC Moshi, Bunda mkoani Mara na Meta mkoani Mbeya na Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

'Pinda njoo wewe'

Akijibu ombi hilo la Pinda, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayoongoza mgomo huo, Dk Stephen Ulimboka alisema hatua ilipofikia madaktari hawatakuwa tayari kumtafuta Waziri Mkuu.
“Kwa sasa mtu yeyote anayetutaka atufuata hapa, hatuwezi kumtafuta tena Waziri Mkuu sababu tulishafanya juhudi hizo bila ya mafanikio,” alisema Ulimboka ambaye pamoja na wenzake wanafanya mikutano yao ukumbi wa Starlight.

Wizara yahaha

Madaktari wakimtaka Pinda awafuate, wizara yenye dhamana na afya jana ilitoa tamko kuhusu mgomo huo ikisema madaktari watapewa nyumba za kuishi karibu na vituo vya kutolea huduma.
Tamko hilo lilitolewa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya na Usatawi wa Jamii Dk Hadji Mponda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Mponda akijibu dai moja baada ya jingine la madaktari hao, alisema serikali kupitia wizara hiyo Menejimenti ya Utumishi wa Umma na wizara ya Fedha, inaendelea na kazi ya kurekebisha waraka utakaoruhusu madaktari kupewa nyumba bila kujali madaraja yao na mishahara.
Akifafanua kuhusu rufaa za wagonjwa hususani vigogo kusafirishwa nje ya nchi kwa matibabu, alisema wizara hugharamia watanzania wote bila kuangalia ni wa aina gani ili mradi watimize vigezo vya kwenda kutibiwa nje.

Muhimbili hali mbaya

Katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jana wagonjwa waliambiwa warudi nyumbani hadi watakapopata taarifa za kumalizika kwa mgomo kupitia vyombo vya habari.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wagonjwa hao walisema walipewa taarifa na baadhi ya wafanya kazi katika vitengo tofauti, vinavyotoa huduma za kliniki hospitalini hapo.
Vitengo vilivyodaiwa kuwatangazia habari hiyo wagonjwa hao ni Taasisi ya Mifupa (MOI), kitengo cha kuhudumia watoto wenye matatizo ya upungufu wa damu na kitengo cha Kliniki ya matatizo ya moyo.
Mmoja wa wagonjwa hao, Rukia Hamisi alisema alipofika MOI alitokea mmoja wa wafanya kazi katika taasisi hiyo na kuwatangazia kuwa wagonjwa wote waondoke eneo hilo hadi watakapotangaziwa kuwa mgomo umekwisha.
“Mimi nimekuja tangu asubuhi, lakini ilipofika saa tatu asubuhi alikuja mfanyakazi mmoja na kututangazia kuwa tuondoke katika eneo hilo hadi tutakapo tangaziwa kuwa mgomo umekwisha kupitia vyombo vya habari,” alisema Hamisi.
Mmoja wa wafanya kazi wa MOI ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alikiri kutoa taarifa hizo na kusisitiza kuwa hali hiyo imetokana na madaktari wanaotakiwa kuwahudumia wagonjwa hawakuwapo kazini.
Muhonewa Mfaume ambaye alikwenda hosptalini kwa ajili ya kutaka barua yake aliyopewa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iweze kusainiwa na daktari ili aweze kwenda kutibiwa nje ya nchi, alisema alipofika katika kitengo hicho aliambiwa na mmoja wa wafanyakazi wa idara ya mapokezi kwamba, arudi nyumbani
Afisa Habari Mwandamizi wa Hosptali ya Taifa Muhimbili Aminiel Aligaesha alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alijibu kwa kifupi kuwa hana taarifa na pia akasisitiza kuwa, huduma zinazoendelea vizuri.
KCMC nako mambo yaharibika

Mgomo huo umezidi kutikisa nchi na kuvuruga huduma za utabibu baada ya madaktari katika hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi nao kujiunga rasmi kwenye mgomo.

Hata hivyo, madaktari hao wamekubaliana kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura tu wakiwamo wa ajali, wanaohitaji kujifungua na walioko wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu(ICU).

Katika tamko lao hilo, madaktari hao waliokutana katika ukumbi wa maktaba walisema katika kipindi chote cha mgomo hawatapokea wagonjwa wa nje na kwamba kliniki zote hazitafanya kazi.

Ingawa hospitali hiyo inamilikiwa na Shirika la Msamaria mwema (GSF) lakini wapo madaktari ambao mikataba yao ya ajira ipo chini ya shirika hilo na wapo ambao ajira zao ziko moja kwa moja serikalini.

Bugando

Jana madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando waliungana na wenzao katika mgomo unaoendelea kusambaa nchi nzima hivi sasa.

Madaktari hao walianza mgomo kwa kukataa kuwapokea wagonjwa wapya isipokuwa wagonjwa wa dharura tu.

Wakizungumza wakati wa mkutano wao uliofanyika katika hosteli ya madaktari wanafunzi, walisema kurudi kwao kazini kutategemea maelekezo kutoka kwa uongozi wa kamati maalum waliyoiunda kuratibu mgomo huo.

Juhudi za uongozi wa hospitali hiyo chini ya Mkurugenzi wake, Dk Charles Majinge kuzuia mgomo huo ziligonga mwamba baada ya madaktari hao kumweleza kuwa mgomo huo haujaitishwa dhidi ya hospitali hiyo wala uongozi wake na kwamba, madai yao yako nje ya uwezo wa utawala wa Bugando.

Dk Majinge alikataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mgomo wa madaktari katika hospitali yake.

Bunda

Huduma ya tiba kwenye baadhi ya vituo vya afya wilayani Bunda, jana zilidorora kufuatia baadhi ya madaktari na wahudumu kuitisha mgomo.

Mwananchi imebaini kuwa ingawa wahudumu na madaktari hao wamefika kazini kwa wakati lakini walikataa kuwahudumia wagonjwa.

“Mimi nimefika hapa saa 3:00 asubuhi lakini sijahudumiwa. Wanaingia (wahudumu) wanakaa ndani kisha wanatoka bila kuwaita wagonjwa," alisema mmoja hospitalini hapo saa 8:00 mchana jana.

Kaimu mganga mkuu wa wilaya hiyo Dk Fransic Mayengera alikana uwepo wa mgomo hospitalini hapo na huku aiita hatua hiyo kuwa ni kutokana na uzembe wa watumishi wa hospitali na kwamba uongozi wake umeanza kuwashughulikia."

Wajawazito wateseka Mbeya

Mgomo wa madaktari katika Hospitali ya Meta mkoani jana uliwaathiri zaidi kina mama wajawazito huku wengine wao wakiambiwa kuwa waende katika hospitali nyingine kwa vile hospitalini hapo hakuna huduma.

Kila mgonjwa aliyefika hospitalini hapo jana alielezwa kuwa hakukuwa na huduma hivyo, akatafute hospitali nyingine huku baadhi ya wauguzi wakijibizana na wagonjwa.

Baadhi ya Waandishi wa habari waliofika katika kituo hicho cha Meta walishuhudia mama mjamzito, Sarah Christopher akiambiwa aende kwenye hospitali nyingine huku hali yake ikionyesha ni mbaya.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo ya Meta Dk Leter Msafiri alisema kutokana na mgomo unaoendelea, kuna baadhi ya huduma zimesitishwa ila wanatoa huduma za dharura ambazo ni pamoja na upasuaji unaofanywa na madaktari bingwa.

Dk Msafiri alisema huduma zilizositishwa ni kliniki na huduma ambazo wagonjwa wanaonekana kuwa hali zao siyo mbaya.


Kilaini
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilani alisema inasikitisha kuona wagonjwa wakiteseka hospitalini kutokana na mgomo huo.
"Kwa namna yoyote ile, wagonjwa wanapaswa kuhudumiwa kwa sababu suala la matibabu linahusisha ni uhai," alisisitiza na kuongeza:
"Inaleta shida kidogo kujua kwa nini Serikali haitatui madai ya madaktari ambayo ni ya msingi, au haina fedha? Kama Serikali haina fedha iseme ili wahusika na Watanzania wote wajue.’’
Baregu LHRC
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimemtaka Pinda, kwenda kuonana na madaktari hao badala ya kusubiri wamfuate ofisini.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba alisema haiwezekani Waziri Mkuu aendelee kukaa ofisini wakati anajua kuwa madaktari wanagoma na wagonjwa wanataabika.
“Hakuna haja ya Pinda kusema madaktari wakiwa tayari waende kuonana naye kwa sababu huu ni ubabaishaji. Wao (madaktari) wako tayari na ndio maana wakagoma hadi pale madai yao yatakaposikilizwa sasa yeye (Pinda) akiendelea kuwasubiri ofisini maana yake nini kama sio kuleta vifo?"
Imeandaliwa na Geofrey Nyang’oro, Onesmo Alfred Daniel Mwingira, Ibrahim Yamola, Christopher Maregesi, Bunda, Ray Naluyaga, Godfrey Kahango, Mbeya, Daniel Mjema na Rehema Matowo,Moshi
Chanzo Gazeti la Mwananchi

No comments: